Habari njema muuzaji bora  kuwahi kutokea,

Hongera na karibu sana kwenye mwendelezo wa makala zetu za ushawishi kutoka kwenye programu yetu ya CHUO CHA MAUZO.

Kwenye jumamosi ya ushawishi tunaongozwa na kauli mbiu inayosema HUPATI UNACHOSTAHILI BALI UNACHOSHAWISHI.

Wiki iliyopita tulifanikiwa kujifunza jinsi ya kuwafanya watu wakubaliane na mawazo yako kanuni ya NNE.
Na kwenye kanuni ya NNE tulifanikiwa kuondoka na kitu kimoja ambacho ni mara zote unapokabiliana na wengine, tumia upole na urafiki na siyo hasira na nguvu.

SOMA; Jinsi Ya Kuwafanya Watu Wakubaliane Na Mawazo Yako Kanuni Ya Nne

Habari njema ni kwamba leo kwenye jumamosi yetu ya ushawishi, tunakwenda kujifunza jinsi ya kuwafanya watu wakubaliane na mawazo yako kanuni ya TANO ambayo ni Mfanye mwingine aseme ndiyo, ndiyo mapema.

Rafiki yangu muuzaji bora kuwahi kutokea, pale tunapoongea na watu wengine, tunapaswa kuanza kuongelea yale mambo ambayo wanakubaliana na sisi kabla hatujaanza kuongelea yale mambo ambayo tunatofautiana nao.
Anza kwa kuweka mkazo kwenye yale mambo mnayokubaliana na onesha kwamba wote mko upande mmoja.

Kwa kufanya hivi mapema na kumweka mtu kwenye hali ya kukubaliana na wewe mapema, inakuwa rahisi kukubaliana na wewe na hata kwa yale ambayo mnatofautiana. 

Kanuni hapa ni moja, ni kumfanya mtu aanze kusema NDIYO, mapema na mara nyingi kabla hujafika kwenye kile mnachotofautiana.
Mtu anapoanza kwa kusema ndiyo, kisha akasema ndiyo, anakuwa katika hali ya kuendelea kusema ndiyo zaidi.

Hakuna hali ngumu utakayokutana nayo kama kuanza mazungumzo na mtu kwenye kile ambacho mnatofautiana.
Mtu akishaanza na HAPANA, ataendelea kusema hapana kwa mengine yanayofuata.
Unajua ni kwa nini ? Kwa sababu sisi binadamu tunapenda msimamo na hatupendi kuona tunakosea, hivyo tukishafanya jambo, tunaendelea kulisimamia.
Kwa mfano mtu aliyeanza na kusema NDIYO, ataendelea kusema NDIYO ili kulinda msimamo wake.
Kadhalika, aliyeanza kwa kusema HAPANA, ataendelea kusema hapana ili asionekane hana msimamo.

Kwenye nyenzo au silaha ya ushawishi ya msimamo (consistency) tulijifunza jinsi nguvu ya msimamo inavyochochea mtu kuwa na mwendelezo wa kufanya.
Pale mtu anapodhamiria kufanya kitu, hapo ndipo msimamo wake unapoanzia, atahakikisha anakifanya kama alivyodhamiria kufanya na ataendelea kufanya.
Kwa mfano, ukimuuzia mteja bidhaa au huduma, akaridhika kiasi cha kusema asante, ukimuomba mteja wa rufaa hawezi kukunyima na mwingine akanufaike kama yeye.
Au ukimuuzia mauzo ya kwanza na akalipia, hawezi kukataa mauzo ya ziada yaani upsell ya kitu kingine kwa bei ndogo kabisa hawezi kukataa, ataona kukataa ni kama kuvunja dhamira yake hivyo atakubali ili kuonesha msimamo aliokuwa nao.

Mtu anaposema HAPANA, mwili wake wote unabadilika, atakaa mbali na wewe? Atakunja sehemu za mwili na hatasikiliza tena kwa makini, kwa sababu akili imeshajifunga kwa kusema hapana. Kadhalika mtu anaposema NDIYO, mwili wote unabadilika, atasogea karibu na wewe, anakunjua sehemu za mwili na anasikiliza kwa umakini.

Watu wote wanaotegemea ushawishi kwenye kazi zao, kama wauzaji, wanasiasa na wahubiri, huwa wanaanza kutafuta ndiyo kwa wale wanaowasikiliza mapema kabisa ili kile kinachoendelea kipokelewe.

Mwandishi Dale Carnegie anatushirikisha siri ya mwanafalsa Socrates kuweza kuwa na ushawishi kwa wengi kwenye mijadala yake. Ni kwa sababu hakuwahi kubishana na mtu katika mijadala.
Badala yake alikuwa anatumia maswali. Alianza kwa kumuuliza mtu maswali ambayo wanakubaliana na mtu alisema ndiyo, aliendelea kupata hivyo ndiyo na kufika mwisho, mtu anajikuta amesema ndiyo kwenye kitu ambacho awali alikuwa hakubaliani nacho.

Hatua ya kuchukua leo; pale unapotaka kumshawishi mtu akubaliane na wewe kwenye eneo lolote kama mauzo au mahusiano, anza na yale maeneo ambayo wote mnakubaliana, pata ndiyo msingi nyingi mapema kisha penyeza kile ambacho unataka akubaliane na wewe, kwa namna ambayo kinaendana na  yale ambayo mnakubaliana na mtu ameshasema ndiyo.

Mwisho, wachina wa kale walikuwa na usemi, yule aendaye kwa upole hufika mbali.
Tumia dhana hiyo kwenye makubaliano na watu, usikimbilie kwenye yale mnayotofautiana, bali anzia kwenye yale mnayokubaliana kisha nenda taratibu ukipata ndiyo mpaka unafika kwenye yale mnayopingana na kuyapa ndiyo pia.

Kutoka kwa muuzaji mwenzako, rafiki anayekupenda na kukujali,

Mwl.Deogratius Kessy

Mwalimu/Mwandishi/Mjasiriamali
Makamu Mkuu wa CHUO CHA MAUZO.
makamu@mauzo.tz, 📞0717101505//0767101504