Rafiki yangu mpendwa,
Kila kitu ambacho tunafanya kwenye maisha yetu, huwa ni sahihi kabisa kwa upande wetu.
Hata kama kwa wengine kinaonekana ni cha ajabu, lakini kwetu kinakuwa sahihi na ndiyo maana tumekifanya.
Inakuwa hivyo kwa sababu kabla hatujafanya kitu chochote, huwa kuna hadithi ambazo tunajiambia sisi wenyewe.
Na hivyo chochote tunachofanya, kinakuwa kinaendana na hadithi tunazojiambia sisi wenyewe.
Ndiyo maana kitu kinaweza kuwa sahihi kwetu na kwa wengine kisiwe sahihi, kwa sababu tunatofautiana hadithi ambazo tunajiambia.

Mwandishi Morgan Housel kwenye kitabu chake kinachoitwa THE PSYCHOLOGY OF MONEY anatufundisha nguvu ya hadithi kwenye kujenga au kuvunja utajiri.
Kwenye kitabu hicho, Housel ametupa masomo 20 ya msingi kuhusu fedha, utajiri, tamaa na furaha. Kupitia masomo hayo tunapata nafasi ya kujifunza mambo ya kuzingatia ili kufanya maamuzi bora kifedha kwetu na kujenga utajiri na furaha.
Kwenye makala ziliyopita, tumepata masomo 16 kati ya hayo 20. Kwenye makala hii tunakwenda kupata masomo manne ya mwisho na hatua za kuchukua ili tujenge na kudumu kwenye utajiri.
17. Hadaa Ya Taarifa Mbaya Na Kukata Tamaa.
Katika kuyachukulia mambo, huwa kuna hali mbili; moja ni kuwa na matumaini (optimism) kwamba mambo yatakwenda vizuri. Mbili ni kukata tamaa (pessimism) kwamba mambo yatakuwa mabaya zaidi.
Katika hali hizo mbili, matumaini ndiyo hali bora kabisa kwa binadamu. Na pia ndiyo uhalisia wa maisha yetu hapa duniani. Ukiangalia maendeleo ambayo yanatokea, hali ya maisha inaenda ikiwa bora kadiri muda unavyokwenda.
Kwa hali kama hiyo ungetegemea watu tuwe na matumaini zaidi kuliko hali ya kukata tamaa. Lakini huo siyo ukweli. Fuatilia habari zozote na utaona jinsi ambavyo habari hasi ndiyo zinapewa kipaumbele kikubwa zaidi.
Ukifuatilia habari kwa muda mrefu, unaweza kuona dunia inaelekea mwisho kabisa. Unakosa matumaini na kuona maisha yanazidi kuwa magumu na mabaya.
Ni asili yetu binadamu kupenda kufuatilia habari hasi kwa sababu kupoteza kunaumiza kuliko kupata. Pale kunapokuwa na ukuaji mdogo wa uchumi, labda asilimia 1, haiwi habari kubwa. Kukiwa na anguko la kiasi hicho hicho la uchumi, inakuwa ni habari kubwa sana.
Watabiri ambao wanasema mambo yatakuwa mazuri, huwa wanapuuzwa na kuonekana wanadanganya.
Lakini watabiri ambao wanasema mambo yatakuwa mabaya, wanazingatiwa na kuonekana wanasema ukweli.
Hilo ndiyo limepelekea habari hasi na utabiri wa mambo mabaya kupata nafasi zaidi kuliko habari nzuri na mambo mazuri yanayoendelea.
Hatua ya kuchukua;
Mara zote kuwa na matumaini kwamba mambo yatakwenda vizuri. Matumaini hayo siyo tu kwa kujiambia, bali kwa kuchukua hatua kuyafanya mambo kuwa mazuri. Puuza habari hasi za mambo kuwa mabaya na weka juhudi kuyafanya maisha yako kuwa bora na yatakuwa bora.
18. Nguvu Ya Hadithi.
Uchumi huwa unaathiriwa sana na hadithi ambazo watu tunajiambia. Kila kitu kinaweza kuwa vile vile, lakini hadithi inapobadilika, matokeo yanabadilika kabisa.
Hivyo ndivyo uchumi huwa unayumba, kwa kubadilika hadithi ambazo watu wanajiambia. Kwa mfano pale soko la hisa linapofanya vizuri, watu wanajipa hadithi kwamba mambo ni mazuri na wanawekeza, hilo linapelekea soko kufanya vizuri zaidi. Na pale soko linapofanya vibaya, watu wanajipa hadithi kwamba mambo ni mabaya na kuuza uwekezaji wao, kitu ambacho kinashusha soko zaidi.
Hapo kunaweza kuwa hakuna mabadiliko yoyote kwenye miundombinu, kampuni ni zile zile, uzalishaji ni ule ule na wateja wale wale, lakini uchumi utayumba sana kutokana na hadithi ambazo watu wanajiambia.
Hadithi tunazojiambia huwa zinaathiriwa na mambo mawili;
1. Pale tunapokuwa na uhitaji sana wa kitu, huwa tunaamini hadithi yoyote ambayo inahusiana na kitu hicho kuwa kweli.
2. Maamuzi mengi tunayoyafanya huwa hatuna taarifa za kutosha, hivyo huwa tunajazia na hadithi zetu sisi wenyewe.
Mambo hayo mawili ndiyo yamekuwa yanafanya tujipe hadithi ambazo siyo sahihi na hivyo kuathiri maamuzi tunayoyafanya.
Lakini pia hadithi ndiyo zimekuwa zinatumika sana kwenye utabiri ambao watu wanafanya, ambao kwa sehemu kubwa huwa unaishia kutokuwa sahihi.
Hatua ya kuchukua;
Tambua maamuzi mengi unayoyafanya ni kutokana na hadithi unazojiambia au kusikia kutoka kwa wengine. Hakikisha unajitengenezea hadithi sahihi kwako ambazo zitakuwezesha kuchukua hatua za kujenga utajiri unaoutaka. Achana na hadithi zinazokukatisha tamaa, maana siyo za kweli.
19. Yote Kwa Pamoja.
Mwandishi anasema ushauri wa fedha huwa haufanyi kazi kwa watu wengi kwa sababu watu wanatofautiana sana. Lakini kuna misingi ya kifedha ambayo mtu yeyote akiifuata ataweza kupata matokeo mazuri kwenye kujenga utajiri. Misingi hiyo ni kama ifuatavyo;
1. Mambo siyo mazuri wala mabaya kama yanavyoonekana. Kuwa mnyenyekevu mambo yanapokuwa mazuri na shukuru mambo yanapokuwa mabaya.
2. Bahati na hatari huwa vinaathiri matokeo unayopata.
3. Msingi wa kwanza wa kujenga utajiri ni kuweka akiba. Haijalishi una kipato kikubwa kiasi gani, kama huweki akiba, huwezi kujenga utajiri.
4. Pangilia na simamia fedha zako kwa namna ambayo utapata usingizi usiku.
5. Jipe muda wa kutosha, kila kitu kinakua pale kinapopewa muda mrefu.
6. Kuwa tayari kukosea na endelea kufanya, utafanikiwa.
7. Tumia fedha kupata udhibiti wa muda, ambao utakupa uhuru na furaha.
8. Tambua watu hawavutiwi na wewe kuwa na vitu vya kifahari, bali wanavutiwa na vitu vya kifahari unavyokuwa navyo. Hivyo usifanye matumizi ya kifahari ili kuwavutia watu.
9. Jua gharama za mafanikio unayoyataka kisha zilipe ili kufanikiwa.
10. Jipe nafasi kubwa ya kukosea ili pale unapokosea usipotee kabisa kwenye mchezo.
11. Jua mchezo unaocheza wewe na weka mkazo kwenye huo, usiige michezo ya wengine.
12. Hakuna jibu moja sahihi kwa watu wote, bali kila mtu ana majibu sahihi kwake.
Hatua ya kuchukua;
Elewa misingi hiyo sahihi kwenye fedha na utajiri na iishi ili uweze kunufaika.
20. Ungamo La Mwandishi.
Mwandishi anatushirikisha saikolojia yake mwenyewe ya fedha, jinsi anavyopangilia na kusimamia fedha zake. Anachoshirikisha ndiyo kinafanya kazi kwake, japo siyo sahihi kwa watu wote.
1. Lengo kuu ni kuwa huru na siyo anasa wala maonyesho.
2. Kuishi chini ya kipato na kuweka akiba sehemu kubwa.
3. Kuchagua kuishi maisha ya kawaida na kutokuongeza matumizi kipato kinapoongezeka.
4. Kuwa na mfuko wa dharura na ongezeko lote la kipato kwenda huko.
5. Kupata raha kwenye vitu visivyo na gharama kama matembezi, kusoma vitabu n.k.
6. Kumiliki nyumba ya kuishi bila ya mkopo.
7. Kuwa na kiasi kikubwa cha ukwasi, 20% ya utajiri wake.
8. Kufanya uwekezaji kwenye mifuko ya pamoja ya uwekezaji badala ya kwenye hisa moja kwa moja.
9. Kuwekeza kwa muda mrefu (miongo) bila ya kuingilia uwekezaji.
10. Mkakati mkuu wa uwekezaji; AKIBA KUBWA, UVUMILIVU na MATUMAINI.
Hatua ya kuchukua;
Tengeneza mkakati wako wa uwekezaji unaoendana na wewe na kisha ufanyie kazi. Usiige wengine, bali fanya maamuzi yako mwenyewe kwa namna ambavyo utapata utulivu mkubwa ndani yako na kudumu kwenye mchezo kwa muda mrefu zaidi.
Tumehitimisha masomo 20 ya UTAJIRI NA FURAHA kutoka kitabu THE PSYCHOLOGY OF MONEY kilichoandikwa na Morgan Housel. Yaweke masomo haya kwenye vitendo ili uweze kujenga tabia sahihi na kudhibiti hisia zako ili kupata utajiri mkubwa. Kwa rejea ya makala za masomo yote 20, BONYEZA MAANDISHI HAYA.
Hapo chini kuna mjadala mzuri ambao tumekuwa nao juu ya masomo haya kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA. Fungua kipindi uweze kujifunza kutoka kwa mifano na shuhuda za wengine.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.