3400; Unajiumiza mwenyewe.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Kama umechagua kufanya kitu, basi hakikisha unakifanya kweli kutoka ndani yako.
Jitoe kwa kila namna kuhakikisha unakifanya kwa juhudi kubwa na ubora wa hali ya juu kabisa.
Hata kama utashindwa kwenye kukifanya kitu hicho, basi hakikisha huna cha kujilaumu kwa upande wako, kwa sababu umeweka kila ulichopaswa kuweka.
Yanayokuwa yamekukwamisha ni ambayo yapo nje ya uwezo wako.
Kama utaingia kwenye kufanya kitu huku hujajitoa kisawasawa, kama utaingia kufanya kitu kwa kujaribu tu na usiweka juhudi kubwa, utaishia kujiumiza wewe mwenyewe.
Unajiumiza kwa sababu kwa huo ufanyaji wako utaishia kushindwa. Kushindwa huko kutakuumiza kwa sababu utaona wazi kwamba kama ungeweka juhudi, huenda matokeo yangekuja tofauti.
Hata kama kilichopelekea ushindwe ni kilicho nje ya uwezo wako, bado utaona kama ungeweka juhudi kubwa zaidi, ungeweza kubadili matokeo hayo.
Majuto huwa ni kitu ambacho kinaumiza sana, tena kwenye wakati ambao huna tena cha kufanya.
Pambana sana usije ukawa na majuto kwenye eneo lolote la maisha yako.
Na njia pekee ya kuepuka majuto ni kuisikiliza nafsi yako na kuingia mazima kwenye kile ambacho unachagua kufanya.
Kama unaanza na maji baridi na lengo ni kuwa na maji moto ili yaweze kukamilisha jukumu fulani, kuyapasha maji hayo haitasaidia.
Kwa sababu utakuwa umetumia nguvu kwenye kuyapasha, lakini yanakuwa hayana moto wa kutosha kuwa na matumizi.
Unaishia tu kuumia kwa kazi uliyoweka kwenye kuyapasha, lakini bado hayana matumizi.
Chemsha maji mpaka yachemke, kama yatashindwa kutumika kwa sababu ya kuchemka kwake, unaweza kuyaacha yapoke.
Lakini kuyapasha halafu yakawa hayana matumizi, huku pia ukiwa huna tena rasilimali za kuyachemsha, ni kujiumiza.
Kama umeamua kujifunza kitu, basi hakikisha umejifunza kwa kina na kuelewa kwa undani.
Kwa sababu kujua kwa juu juu tu, utaishia kujiumiza mwenyewe.
Utakuwa hujui kwa kiasi cha kutosha kuleta mabadiliko mazuri, lakini pia unakuwa unajua kama ungejua zaidi ingekusaidia.
Kama umeamua kutafuta pesa na utajiri, basi jitoe kweli kweli kupata pesa nyingi na utajiri mkubwa.
Kuweka juhudi kidogo huku ukiona utajiri kidogo unakutosha haitakusaidia, zaidi itakuumiza.
Kwa sababu hutapata pesa na utajiri wa kukosa, lakini pia utaona wazi kama ungeongeza juhudi, ungeweza kufanya na kupata zaidi.
Kwenye jambo lolote lile, ukishachagua kuweka juhudi, basi kuwa tayari kufanya kila kinachohitajika kufanyika ili kupata unachotaka.
Kuweka juhudi kidogo kwa sababu hutaki kujichosha, unaishia kujiumiza zaidi na aina ya matokeo ambayo utayapata.
Hakuna kitu kinachoumiza kama fikra kwamba kwa kufanya zaidi ungeweza kubadili matokeo uliyopata.
Wewe fanya kiasi kwamba huwi na majuto yoyote kwenye matokeo unayopata.
Ni labda yanakuwa matokeo makubwa sana kulingana na juhudi ulizoweka.
Au unakuwa umejifunza nini hakifanyi kazi na kipi kinachofanya kazi.
Weka kila kinachohitajika ili baadaye usiwe na majuto ya kama ninge….
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe