Rafiki yangu mpendwa,

Karibu kwenye #HadithiZaKocha ambapo tunakwenda kupata hadithi ya Kuku anayetaga mayai ya dhahabu. Soma hadithi hii kwa kina kisha weka maoni yako ni nini umejifunza kutoka na hadithi hii na jinsi unavyokwenda kufanyia kazi kwenye maisha yako.

Mkulima mmoja alikuwa anafuga kuku. Siku moja alipoenda kwenye banda la kuku, alikuta kuku ametaga yai ambao ni la tofauti. Alipoliangalia, aliona ni kama dhahabu.

Alitoka na yai lile mpaka kwa sonara, ambaye baada ya kulichunguza alikuta ni dhahabu tupu. Aliweza kuuza yai lile kwa bei kubwa na kupata fedha nyingi. Aliweza kutumia fedha hizo kununua vitu mbalimbali alivyokuwa anavihitaji.

Maisha yaliendelea na baada ya wiki yule kuku alitaga tena yai jingine, ambalo pia lilikuwa la dhahabu. Mkulima akaenda kuuza yai na kufanya matumizi makubwa. Maisha yake yalibadilika sana na kuwa ya hadhi ya juu kutokana na fedha alizopata.

Huo ukawa ndiyo utaratibu, kila wiki, kwenye siku ile ile, kuku alitaga yai la dhahabu, mkulima alienda kuuza, alipata fedha nyingi na kufanya matumizi makubwa.

Kila alivyokuwa anapata fedha, matumizi yake yalikuwa makubwa zaidi. Kwa sababu alikuwa ameshajipa uhakika kila wiki anapata yai la dhahabu, alianza kufanya matumizi kabla hata ya kupata yai.

Hivyo alianza kukopa fedha na kufanya matumizi akijua siku ya wiki ikifika, atapata yai la dhahabu, ataliuza na kulipa madeni hayo. Hilo nalo lilienda kwa muda, alifika hatua ya kuwa na madeni makubwa kuliko hata fedha anayopata kutoka kwenye yai la dhahabu analopata kila wiki.

Wiki moja alipata shida kubwa ambayo ilihitaji fedha za haraka. Alitafuta mahali pa kukopa fedha hiyo lakini hakupata. Ilikuwa ni siku moja kabla ya siku ya kupata yai, lakini hakuwa anaweza kusubiri kwa sababu ya shida kubwa aliyokuwa nayo.

Hapo ndipo wazo likamjia kwamba kwa sababu siku inayofuata huyo kuku atataga yai, lazima litakuwa tumboni. Pia akafikiria huko tumboni kwa kuku kutakuwa na mayai mengi ambayo akiyapata kwa pamoja atamaliza shida zake zote.

Hilo lilimpelekea afanye maamuzi ya kumchinja yule kuku ili ayapate mayai hayo na kutimiza mahitaji yake. Mkulima alipigwa na butwaa baada ya kumchinja kuku, kwani hakukuta yai hata moja tumboni kwa yule kuku.

Mwisho ukawa kilio kikubwa, kwa sababu kuku ameshamchinja, mayai hajapata na kuku hana tena.

Rafiki, karibu kwenye maoni hapo chini ushirikishe umejifunza nini kwenye hadithi hii fupi na unakwenda kutumiaje hayo uliyojifunza kwenye kujenga maisha ya mafanikio.

Hapo chini ni kipindi cha ONGEA NA KOCHA ambapo nimesimulia hadithi hii. Unaweza kufungua na kuangalia kisha kuweka maoni yako kwenye kipindi hicho. Karibu ujifunze, uchukue hatua na kuboresha maisha yako.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.