Habari Matajiri Wawekezaji,
Karibuni kwenye mfululizo wa masomo ya uwekezaji kwenye programu yetu ya NGUVU YA BUKU. Kupitia programu hii tunajifunza na kufanya uwekezaji kwa vitendo. Huku tukiwa tumechagua uwekezaji wa mifuko ya pamoja wa UTT AMIS kama nguzo yetu kuu ya uwekezaji.
Kwenye mfululizo wa masomo ya mifuko iliyo chini ya UTT AMIS (Masomo yote yako hapa; https://amkamtanzania.wordpress.com/category/utt/), tumejifunza kwa kina mifuko sita. Mifuko hiyo ni UMOJA, WATOTO, WEKEZA MAISHA, UKWASI, JIKIMU na HATIFUNGANI.
Kwenye somo la kila mfuko tuliona sifa zake, faida zake na mpango wake wa uwekezaji. Tunapaswa kuendelea kurejea masomo hayo mara kwa mara ili tuboreshe uwekezaji wetu kadiri tunavyokwenda.
Swali kubwa ambalo watu wengi wanalo ni uwekezeje kwenye mifuko hiyo ambayo tayari ni mingi?
Kuna ambao wanafanya uwekezaji kwenye mifuko yote au mingi zaidi. Na kuna ambao wanafanya uwekezaji kwenye mfuko mmoja pekee.
Inapokuja kwenye fedha, hakuna jibu moja linalowafaa watu wote. Hiyo ni kwa sababu watu tunatofautiana kwenye mambo mengi, kuanzia kipato, umri, mahitaji na hata kiasi cha utajiri tunachohitaji ili kuwa na maisha huru.
Hivyo mpangilio sahihi wa mifuko ya uwekezaji ya UTT AMIS itategemea na hali za kila mtu. Kwenye somo hili tutakwenda kujifunza mpango wa msingi kabisa ambao kwa wengi unaweza kufaa au kuboreshwa kidogo na kufaa.

MIFUKO YA MSINGI KUWA NAYO WAKATI UNAANZA.
Kwa wawekezaji ambao wanaanza na bado wana nguvu ya kufanya kazi za kuingiza kipato, wanapaswa kuanza na mifuko mikuu miwili; UMOJA na UKWASI.
Umoja ni kwa ajili ya uwekezaji wa muda mrefu bila ya kutoa kabisa. Huku ukwasi ukiwa kwa ajili ya uwekezaji wa malengo maalumu.
Kwenye mfuko wa UMOJA (https://amkamtanzania.wordpress.com/2024/02/05/mfuko-wa-uwekezaji-wa-pamoja-wa-umoja-wa-utt-amis/) unafanya uwekezaji na kusahau, ukishawekeza huko hugusi hata iweje. Hata pale unapokuwa na changamoto mbalimbali, unachukulia ni kama fedha ambayo tayari ulishaitumia na huwezi kuipata tena. Kwa kuwa na nidhamu kali kwenye huu mfuko, utaweza kupata manufaa makubwa kwa riba mkusanyiko.
Kwenye mfumo wa UKWASI (https://amkamtanzania.wordpress.com/2024/02/19/uwekezaji-kupitia-mfuko-wa-pamoja-wa-ukwasi-wa-utt-amis/) unafanya uwekezaji kwa malengo maalumu. Kwa mfano kama unataka kukusanya fedha kukamilisha mpango fulani ulionao, ambapo itakuchukua muda mrefu kukusanya fedha hizo, ukikaa na fedha taslimu au kuweka benki inapoteza thamani kwa mfumuko wa bei. Hivyo unakuwa na mfuko wa UKWASI ambapo unakusanya fedha hizo, huku ukiendelea kunufaika na ukuaji unaokuwa unapatikana. Na pale unapokamilisha unaitoa na kutekeleza jambo lako.
Kwa wawekezaji wote ambao tayari wanaendelea na shughuli zao nyingine za kuingiza kipato, hakikisha unakuwa na mifuko hiyo miwili.
MIFUKO YA KUWA NAYO KWENYE MAHITAJI YA ZIADA.
Pale unapokuwa na mahitaji ya ziada, unaweza kuwa na mifuko mingine kulingana na mahitaji hayo.
Kama una watoto na unataka kuanza kuwafundisha na kuwafanyia uwekezaji mapema, unapaswa kuwafungulia mfumo wa WATOTO (https://amkamtanzania.wordpress.com/2024/02/12/mfuko-wa-uwekezaji-wa-pamoja-wa-watoto-kwenye-utt-amis/). Japo mfuko ni kwa ajili ya watoto, utakayefungua na kuendesha ni wewe mzazi.
Kama unataka kupata bima ya maisha na majanga mengine, mfuko wa WEKEZA MAISHA (https://amkamtanzania.wordpress.com/2024/02/09/mfuko-wa-uwekezaji-wa-pamoja-wa-wekeza-maisha-utt-amis/) utakufaa sana. Hapo unafanya uwekezaji ambao unakua thamani, lakini pia unakulinda pale unapopata majanga mbalimbali, ikiwepo ulemavu au kifo.
Angalia ni mahitaji gani ya ziada uliyonayo kwenye maisha yako kisha yafungulie mfuko sahihi wa uwekezaji.
MFUKO WA KUWA NAO KWENYE UHURU WA KIFEDHA.
Lengo kubwa la uwekezaji ni kuwa na uhuru wa kifedha. Uhuru wa kifedha ukiwa ni kuweza kuyaendesha maisha yako hata kama hufanyi kazi ya kuingiza kipato moja kwa moja. Yaani fedha ya kuendesha maisha inaingia hata kama hufanyi shughuli yoyote.
Harakati zote tunazofanya sasa ni katika kufikia huo uhuru wa kifedha. Kwa sababu kadiri muda unavyokwenda nguvu zetu za kufanya kazi zinapungua, wakati mahitaji ya maisha yetu yakiongezeka. Hivyo kama hatutaandaa mapema mazingira ya kuweza kuingiza fedha hata kama hatufanyi kazi, tutateseka sana baadaye.
Pale unapofikia uhuru wa kifedha, yaani kuwa na uwekezaji ambao unaweza kukuingizia kipato cha uhakika hata kama hufanyi kazi moja kwa moja, unapaswa kuwa na mfuko wa HATIFUNGANI wa UTT (https://amkamtanzania.wordpress.com/2024/03/04/uwekezaji-kupitia-mfuko-wa-pamoja-wa-hatifungani-wa-utt-amis/).
Uzuri wa mfuko wa HATIFUNGANI ni huu; KILA MWEZI UNALIPWA MAREJESHO KUTOKA KWENYE UWEKEZAJI WAKO. Pamoja na kulipwa marejesho hayo kila mwezi, uwekezaji wako unakuwa unaendelea kukua thamani.
Hiyo ni tofauti na wewe mwenyewe kuwa unauza uwekezaji wako ili upate hela ya kuendesha maisha, kwani unakuwa unaingilia ukuaji wake. Lakini kwa mfuko wa hatifungani, unapata marejesho, huku msingi ukiendelea kukua.
Unachohitaji ni kuwa na kiasi cha kutosha kwenye mfuko huo ili marejesho unayopata kila mwezi yakuwezeshe kuendesha maisha yako.
Kwa mfano kama gharama za kuendesha maisha yako kwa mwezi ni milioni 5 na mfuko wa hatifungani unatoa rejesho la asilimia 1 ya uwekezaji kila mwezi, unahitaji kuwa na uwekezaji wa milioni 500. Ina maana ukiwa na huo uwekezaji, kila mwezi unaingiza kipato bila kufanya kazi yoyote. Kadhalika kama mahitaji yako ni milioni 1 kwa mwezi, ukiwa na uwekezaji wa milioni 100, kila mwezi unapata rejesho lako bila hata kufanya kazi.
Kwa kuwa na kiasi kikubwa cha uwekezaji kwenye mfuko wa hatifungani, unakuwa umejitengenezea mfumo wako mbadala wa kukuingizia mshahara wa kila mwezi bila ya kulazimika kufanya kazi yoyote.
KUHAMA MFUKO MMOJA KWENDA MWINGINE.
Tumeona hapo mpango wa uwekezaji unahusisha mifuko mbalimbali, lakini mfuko wa mwisho kabisa ni wa HATIFUNGANI. Swali ni je uanze na mifuko yote kwa pamoja kwa sababu hizo mbalimbali?
Jibu ni hapana, anza na ile mifuko ya msingi kwako na fanya uwekezaji mkubwa kwako. Baadaye, kadiri unavyokwenda na mahitaji kubadilika, unaweza kuhamisha uwekezaji wako kutoka mfuko mmoja kwenda mfuko mwingine.
UTT AMIS wanatoa nafasi ya kuhamisha uwekezaji wako kwa mifuko yote kasoro mfuko wa WEKEZA MAISHA. Hivyo unaweza kuanza na mipango yako kwenye mifuko mingine, halafu mwisho ukaja kuhamishia kwenye mfuko unaohitaji katika hicho kipindi.
Kwa maana hiyo, mfuko wako wa mwisho, pale unapokuwa umefikia kustaafu ni wa HATIFUNGANI. Hivyo utaweza kuhamisha uwekezaji wako kutoka kwenye mifuko mingine na kupeleka kwenye mfuko wa hatifungani na kisha kuanza kunufaika na marejesho ya kila mwezi.
Swali unaloweza kuwa unajiuliza ni kwa nini usianze na mfuko wa HATIFUNGANI moja kwa moja? Jibu ni kama una uwezo wa kufanya uwekezaji mkubwa, unaweza kuanza nao.
Lakini kwa uwekezaji mdogo mdogo, mfuko wa HATIFUNGANI hutaweza kunufaika nao sana. Hata mpango wa gawio la kila mwezi, ni pale uwekezaji unapokuwa zaidi ya Milioni 10.
Na zaidi, unapokuwa unaanza unataka uwekezaji wako na marejesho viendelee kukuzalishia badala ya kutoa. Hivyo kupata marejesho wakati bado unaendelea kuwekeza siyo mpango sahihi.
Weka mpango wako sahihi wa uwekezaji kupitia mifuko ya UTT AMIS na ufuate ili kuweza kufikia lengo la utajiri na uhuru wa kifedha.
MJADALA WA SOMO.
Karibu kwenye mjadala wa somo hili, kama uthibitisho wa kusoma somo na kulielewa. Jibu maswali haya;
1. Ipi mifuko ya kila mwekezaji kuanza nayo na kwa sababu gani?
2. Upi mfuko wa kuwa nao pale unapofikia uhuru wa kifedha na kustaafu? Kwa nini uje uhamie kwenye mfuko huo badala ya kuanza nao?
3. Shirikisha mpango wako wa mifuko ya uwekezaji ya UTT AMIS ambao utakwenda nao kwa msimamo.
4. Karibu uulize swali lolote ulilonalo kuhusu somo hili na programu nzima ya NGUVU YA BUKU.
Shirikisha majibu ya maswali haya kama uthibitisho wa kusoma, kuelewa na kuweka kwenye matendo ambalo ni hitaji la msingi la programu hii ya NGUVU YA BUKU.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.