Rafiki yangu mpendwa,

Kile ambacho watu wanakiona kwa nje kama utajiri, siyo utajiri halisi. Na ndiyo maana masikini wengi wanaowaiga matajiri, huwa hawapati utajiri, badala yake wanazidi kuzama kwenye umasikini.

Kwa kuangalia kwa nje, wengi hudhani wale wenye matumizi makubwa na ya kifahari ndiyo matajiri. Lakini huo siyo ukweli, kuwa na kipato kikubwa siyo sawa na kuwa na utajiri mkubwa.

Watu wengi wenye matumizi makubwa ni kweli huwa wana kipato kikubwa. Lakini kutokana na matumizi hayo makubwa, wanashindwa kutumia kipato hicho kikubwa kujenga utajiri.

Matokeo yake ni watu wengi wenye kipato kikubwa wanaishia kuwa masikini. Kwa maana hiyo, kuangalia matumizi makubwa ya watu na kudhani ndiyo utajiri ni kujipoteza.

Waandishi Thomas J. Stanley na William D. Danko, baada ya kufanya utafiti kwa miaka mingi, wakiwahoji matajiri, walipata picha ya tofauti na iliyozoeleka na wengi. Walichokiona ni kwamba matajiri wengi wana maisha ya kawaida kabisa, ambapo kwa nje hawawezi kudhaniwa kama ni matajiri. Huku wale ambao kwa nje wanaonekana matajiri kwa matumizi yao, wakiwa hawana utajiri mkubwa.

Ni kutokana na matokeo ya tafiti zao ndiyo waliweza kuandika kitabu walichokiita The Millionaire Next Door: The Surprising Secrets of America’s Wealthy. Kwenye kitabu hicho wameonyesha jini ambavyo wale wenye utajiri mkubwa wanavyokuwa na maisha ya kawaida.

SIFA KUU SABA ZA MATAJIRI WA KAWAIDA.

Kitabu The Millionaire Next Door kimeleta pamoja sifa kuu saba ambazo waandishi waliziona zikijirudia kwa matajiri wengi ambao wana maisha ya kawaida. Sifa hizo ni rahisi, ambazo kila mtu anaweza kujijengea, lakini kwa wengi inakuwa vigumu.

Sifa hizo saba ni kama ifuatavyo;

1. Kuishi chini ya kipato.

Matajiri wa kawaida huwa ni mabahili, ambao wanahakikisha matumizi yao hayazidi kipato chao. Wengi wanaweka akiba ya angalau asilimia 15 ya kipato chao. Ubahili ndiyo msingi mkuu wa kujenga utajiri mkubwa.

2. Kuwekeza muda, nguvu na fedha kwenye kujenga utajiri.

Matajiri wanawekeza katika kujenga utajiri wao. Wanatumia muda wao mwingi, nguvu zao na hata fedha kuhakikisha wanajenga utajiri mkubwa kwao. Kwa juhudi wanazoweka, wanapata matokeo mazuri. Masikini hawahangaiki kujenga utajiri, wanadhani ni kitu kinachotokea chenyewe kama bahati. Matokeo yake ni wanabaki kwenye umasikini.

3. Kuamini uhuru wa kifedha ni muhimu kuliko maonyesho ya nje.

Matajiri hawajali sana wanaonekana au kuchukuliwaje na wengine, hivyo hawahangaiki kufanya vitu ili kuonekana. Kilicho muhimu kwao ni kujenga utajiri ili wawe na uhuru wa kifedha. Kufikia uhuru wa kifedha ndiyo kipaumbele namba moja kwao na hawapo tayari kukikwamisha kwa namna yoyote ile. Masikini wanajali sana wanaonekanaje, hivyo wanakuwa na matumizi mengi ya kuonekana ambayo yanawakwamisha kujenga utajiri.

4. Kutokupewa misaada ya kiuchumi na wazazi wao.

Matajiri wengi hawakupewa msaada wa kiuchumi na wazazi wao, kwa sababu wazazi wao hawakuwa na uwezo mkubwa. Wale ambao wazazi wao ni matajiri, wamekuwa wanakuwa masikini kwa sababu ya utegemezi wa wazazi kwenye misaada ya kiuchumi.

SOMA; Kwa Nini Ongezeko La Kipato Limekuwa Halileti Utajiri Kwa Wengi.

5. Kuwa na watoto wanaojitegemea kiuchumi baada ya kuwa watu wazima.

Matajiri wanaodumu kwenye utajiri wao kwa muda mrefu ni wale wanaolea watoto wao kwa namna ambayo wanaweza kujitegemea wakiwa watu wazima. Hilo linawapunguzia mzigo wa kuwasaidia kiuchumi. Wale ambao wanategemewa na watoto wao hata wakiwa watu wazima, utajiri wao hushuka kwa kasi.

6. Kuwa hodari kwenye kuchangamkia fursa.

Matajiri huwa wanachangamkia fursa nzuri zinazojitokeza mbele yao na kuzitumia kujenga utajiri mkubwa zaidi. Masikini huchelewa kuchangamkia fursa na kupitwa.

7. Kuchagua kazi/biashara sahihi kwao.

Matajiri wanapenda sana kile wanachofanya kiasi kwamba ndiyo chanzo kikubwa cha furaha kwao. Hilo linawafanya wasiwe na matumizi makubwa wala kutafuta njia za kutoroka kwenye hicho wanachofanya. Kwa kupenda wanachofanya, wanakifanya kwa kujituma sana na kwa muda mrefu, kitu kinachowapelekea kufanikiwa zaidi. Masikini huwa hawapendi wanachofanya na hivyo hawakifanyi kwa ubora, kitu kinachowafanya wazidi kubaki kwenye umasikini.

Hizi ndiyo sifa kuu saba za matajiri wa kawaida. Sifa ambazo kila mtu anaweza kuwa nazo, lakini wengi hawana kwa sababu kuna vitu vitatu muhimu vinavyohitajika kwenye kujenga utajiri;

i. Nidhamu binafsi.

ii. Kujinyima/Kujitoa kafara.

iii. Kufanya kazi kwa juhudi kubwa.

Tutapata mfululizo wa masomo ya kitabu hiki kwa lengo la kujijengea sifa hizo ili tuweze kujenga utajiri mkubwa kwa kuishi maisha ya kawaida. Masomo yote ya kitabu hiki cha The Millionaire Next Door yanapatikana kwa KUBONYEZA MAANDISHI HAYA.

Karibu kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA ambapo tumekuwa na mjadala mpana juu ya somo hili la kujenga utajiri mkubwa kwa kuishi maisha ya kawaida. Fungua hapo chini kujifunza.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

0678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.