Habari njema muuzaji bora kabisa kuwahi kutokea,

Karibu sana kwenye mwendelezo wa makala zetu za ukamilishaji ambazo ni mwendelezo wa makala kutoka CHUO CHA MAUZO.

Hongera sana kwa kuendelea kujifunza na kuchukua hatua kwa haya unayoendelea kujifunza hapa.

Leo ni jumatano ya ukamilishaji tukiongozwa na kauli mbiu inayosema ABC ALWAYS BE CLOSING-MARA ZOTE KUWA UNAKAMILISHA WATEJA.

Kama kauli mbiu inavyosema, mara zote unapaswa kukamilisha wateja na wewe pia unapaswa kukamilisha wateja. Na kukamilisha ndiyo wajibu wako namba moja kwenye biashara yako.
Wajibu wako namba moja ni kuuza na unapokuwa umemuuzia mteja maana yake umemkamilisha.
Hivyo basi, kila wakati wageuze wateja tarajiwa uliokuwa nao na waweze kununua na kuwa wateja kamili.

Ukamilishaji ndiyo kitu muhimu sana kwenye mauzo kwa sababu ndiyo kitu pekee kinacholeta fedha kwenye biashara kupitia kile unachouza iwe ni bidhaa au huduma.

Kwenye somo letu lililopita tulijifunza mbinu mbili za uhakika za ukamilishaji wa mauzo nayo ni mbinu namba 31 na 32.
Kwenye mbinu namba 31 tulijifunza ukamilishaji wa bajeti namba moja.
Na kwenye ukamilishaji wa namba 32 tulijifunza ukamilishaji wa bajeti namba mbili.

Kama ulienda kuzifanyia kazi na kupata matokeo basi karibu sana utushirikishe namna ulivyonufaika nazo mbinu hizo.

SOMA; Mbinu Mbili Za Uhakika Za Ukamilishaji Wa Mauzo 31-32

Leo kwenye jumatano ya ukamilishaji tukiongozwa na kauli mbiu yetu inayosema ABC ALWAYS BE CLOSING-MARA ZOTE KUWA UNAKAMILISHA WATEJA, tunakwenda kujifunza mbinu nyingine mbili za uhakika za ukamilishaji wa mauzo nazo ni mbinu namba 33 na 34

Zifuatazo ni mbinu mbili za uhakika za ukamilishaji wa mauzo ambazo tunakwenda kujifunza hapa;

33. Ukamilishaji wa bajeti – 5.

Mteja anakuja na kukuambia kwamba yuko juu ya bajeti,
Unamwambia hivi;

“Asilimia 90 ya wateja ninaowauzia huwa wanakuwa juu ya bajeti wanapofika hapa. Kwa sababu ulifanya maamuzi ya manunuzi ya nyuma, ambayo huenda hayakuwa sahihi kwako, haimaanishi ujiadhibu sasa kwa kukosa kitu hiki kizuri unachokihitaji sasa.
Tukamilishe hili….”

Muuzaji bora kuwahi kutokea, hata serikali za nchi huwa zina madeni, lakini haziachi kufanya kazi. Hivyo hakikisha pingamizi la bajeti halikuzuii kukamilisha mauzo, mwonyeshe mteja kuwa juu ya bajeti ni kawaida kwa kila mtu, kisha kamilisha mauzo.

34. Ukamilishaji wa kusali.

Ukamilishaji huu ni wa kuheshimu imani ya mteja na kushirikiana naye wakati anasali. Wauzaji wengi huona eneo la imani ni mwiko kulitumia, lakini siyo kweli. Kama mteja ametaja kuhusu imani yake na kusali, basi ungana naye katika hilo mpaka afanye maamuzi ya kununua.

Unaona mteja amekuwa mgumu kukamilisha mauzo na ni mtu wa imani fulani, mwambie;
“Ndugu, nathamini hilo. Huwa nasali kwa kila maamuzi ninayofanya. Je wewe pia huwa unasali? Tusali pamoja, naamini Mungu hawezi kutudanganya wote wawili. Nitakubali matakwa ya Mungu kwetu wawili.”

Baada ya hapo, mwambie mteja tukamilishe hili. Na watu huwa wanapenda na kuthamini sana mambo ya kiimani, hivyo yatumie kukusaidia kukamilisha mauzo.

Mauzo ni vita isiyoruhusu umwagaji wa damu. Hivyo usikubali mteja akuuzie kwa kukupa sababu, bali tumia mapingamizi mbalimbali anayokupa kumshawishi kununua.

Kutoka kwa muuzaji mwenzako, rafiki anayekupenda na kukujali,

Mwl.Deogratius Kessy

Mwalimu/Mwandishi/Mkufunzi wa mauzo.
Makamu Mkuu wa CHUO CHA MAUZO.
makamu@mauzo.tz, 📞0717101505 //0767101504