3405; Fikiri kwa usahihi.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,
Unayataka mafanikio makubwa, lakini je kufikiri kwako kuko sahihi kiasi gani?

Namna unavyofikiri, ina athiri sana matokeo unayoyapata.
Kufikiri kwako kuna mchango mkubwa sana kwenye matokeo unayoyapata.

Unapaswa kufikiri kwa ukubwa sana, hata kama unaanza na hatua ambazo ni ndogo. Huwezi kupata matokeo makubwa kuliko fikra ulizonazo.

Unapaswa kufikiri kwa muda mrefu, japo unachukua hatua sasa. Hupaswi kukwamisha yajayo kwa yale unayofanya sasa, hivyo kufikiri kwa muda mrefu kunakuwa na manufaa.

Unapaswa kuwekeza ndani yako mwenyewe, kwa sababu huo ndiyo uwekezaji ambao unalipa zaidi na usioweza kuupoteza hata itokee nini. Anza na uwekezaji huo kabla ya mwingine wowote.

Unapaswa kuamini kwenye mchakato ulio sahihi na kuufuata mchakato huo mara zote bila ya kujali ni matokeo gani unayoyapata.

Unapaswa kupokea mrejesho sahihi wa hatua unazochukua, ili uweze kuboresha zaidi kulingana na matokeo unayopata ukilinganisha na yale unayoyataka.

Unapaswa kuweka umakini wako wote kwenye kitu kimoja kwa wakati, mpaka ukikamilishe kwa mafanikio makubwa. Kutawanya uwekezaji wako unaishia kupata matokeo ya kawaida, ambayo ni ya chini sana ukilinganisha na uwezo wako.

Unapaswa kujifunza endelevu, bila ukomo au kuona umeshajua kila kitu. Unayojua ni machache sana ukilinganisha na yale unayopaswa kujua, endelea kujifunza.

Unapaswa kuboresha mahusiano yako na watu wengine, kwa sababu kuna nyakati utawahitaji hata wale ambao unadhani huwezi kuwahitaji.

Unapaswa kuweka uzito kwenye kile unachofanya, kama ndiyo kitu muhimu zaidi kwako na ambacho unakazana kuwa bora kuliko wengine wote wanaokifanya. Hilo litakutofautisha kabisa na wengine.

Unapaswa kuwa na msimamo kwenye ufanyaji, kuonekana mara zote, bila ya kukosa, hata iweje. Usitafute sababu za kutokufanya, bali fanya bila ya sababu.

Unapaswa kuzingatia yale ya msingi kabisa kwenye ufanyaji. Kabla ya kuhangaika na makubwa, hakikisha yale ya msingi umeyazingatia vizuri. Hayo ndiyo yatakupa matokeo ya uhakika mara zote.

Unapaswa kuelewa kwamba hakuna siri zilizofichwa kuhusu jambo lolote lile. Kila unachopaswa kujua ili kufanikiwa kipo wazi kabisa, ni wewe kujifunza na kuweka kwenye vitendo ili kupata matokeo mazuri.

Unapaswa kutokuwa na kiburi cha aina yoyote ile, hasa pale unapokuwa umeanza kupiga hatua. Kuwa mnyenyekevu mara zote na utaweza kufanya makubwa zaidi.

Unapaswa kukubali kwamba safari ni ngumu na ufafanya makosa mengi. Lakini hayo hayapaswi kukukatisha tamaa, badala yake unapaswa kuendelea kwa msimamo bila kuacha.

Rafiki, unafikiri kwa usahihi kiasi gani kwenye hayo yaliyoorodheshwa hapo?
Boresha kufikiri kwako ili uweze kukaa kwenye njia sahihi na kupata mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe