Habari njema Matajiri Wawekezaji,

Kwenye somo lililopita kuhusu kujenga ujasiri ili kuweza kujenga utajiri kupitia uwekezaji, mrejesho wa wengi ulikuwa ni kukosa ujasiri wa kusema HAPANA.

Kusema HAPANA ni moja mahitaji muhimu sana ili kufanikiwa kwenye kila eneo la maisha yako. Hiyo ni kwa sababu bila ya HAPANA, utaishia kutawanya nguvu na rasilimali zako kwa mambo yasiyo na tija.

Kutokana na mrejesho wa wengi kushindwa kusema HAPANA ili kujenga utajiri wanaoutaka, kwenye somo hili tunakwenda kujifunza jinsi ya kufanya hivyo kwa uhakika.

HAPANA NI SENTENSI ILIYOKAMILIKA.

Kitu kimoja kinachowafanya wengi washindwe kwenye hapana ni kudhani wanahitaji kuwa na maelezo mengi kuhusu hapana zao. Ukweli ni kwamba neno HAPANA ni sentensi iliyokamilika, ambapo hulazimiki kutoa maelezo mengine ya ziada.

Pale unapokuwa hukubaliani na jambo, sema HAPANA na ishia hapo. Hulazimiki kutoa maelezo yoyote ya ziada. Na hata mtu akikuuliza kwa nini umesema hapana, mjibu haiwezekani.

Majibu mafupi huwa yana nguvu na hupunguza majadiliano yasiyokuwa na tija. Ukianza kutoa maelezo marefu unawafanya watu waone hapana yako haina nguvu na kukushawishi ubadilike na kusema ndiyo.

LAZIMIKA KUSEMA HAPANA.

Kama wewe mwenyewe unakosa ujasiri wa kusema HAPANA, tengeneza mazingira ambayo yatakulazimisha kusema hapana. Kwa mfano kama unashindwa kusema hapana kwenye fedha, hakikisha huwi na fedha ambazo hazina matumizi. Kuwa na bajeti na kisha baki na fedha ya bajeti hiyo tu. Fedha nyingine yote iweke mbali na wewe kwa namna ambayo huwezi kuifikia.

Kwa njia hiyo, mtu anapokuja kwako akitaka fedha, kwa sababu huna, utalazimika kusema hapana. Na wala hutaumia kwa sababu unajua ni kweli huna, hivyo hutakuwa na hatia yoyote.

Kadhalika kwenye mambo mengine unayokubali kirahisi, tengeneza mazingira ambayo yanakulazimisha kusema hapana na utazuia udhaifu wako kwenye hapana usikukwamishe.

HAPANA KAMA JIBU LA MOJA KWA MOJA.

Watu wanapokuja na maombi au mapendekezo yoyote kwako, usijiambie utayafikiria na kuona kama unaweza kukubaliana nayo. Watu wakishajua uko hivyo, watakuja kwako wamejipanga kwa namna ambayo utashawishika na kile wanachotaka.

Unatakiwa kuwa mtu ambaye jibu lako la moja kwa moja ni hapana na una vigezo vya nini kitakubadili kutoka hapana kwenda ndiyo. Ukiwa umeyaandaa hayo kabla ya wakati wa kufanya maamuzi, itakusaidia. Kwa sababu ukiwa huna maandalizi na misingi ya kusimamia, watu watakujaza hisia ambazo zitakusukuma kukubali, kisha baadaye unakuja kujutia.

Kwenye kila kitu anzia kwenye hapana na kuwa na vigezo vya kubadilika na kwenda ndiyo, na badilika pale tu vigezo vinapokuwa vimefikiwa na siyo kwa kusukumwa na hisia.

SOMA; 3029; Msimu wa HAPANA.

WAWEKEE WATU UGUMU FULANI.

Watu huwa wanapenda urahisi kwenye kila jambo wanalofanya. Kwa mfano kama mpo ndugu wawili, ambao mnategemewa na ndugu wengine wengi, kama ndugu mmoja akiombwa kitu anatoa hapo hapo na mwingine akiombwa anahoji kwanza, waombaji watakimbilia kwa anayetoa bila kuhoji. Ndiyo binadamu walivyo, hawapendi ugumu wowote.

Kwa kujua hilo, wawekee watu ugumu kwenye maombi na mapendekezo wanayoyaleta kwako. Anza kwa kuwahoji kwenye kile wanachoomba au kupendekeza. Watake watu wajieleze kwenye vile wanavyoomba au kupendekeza. Wahoji maswali mbalimbali ambayo yanawataka kweli waonyeshe wanamaanisha na wamejiandaa.

Ukifanya hivyo utaona maombi na mapendekezo kwako yanapungua. Watu watakuja kwako pale wanapokuwa na mahitaji ya msingi kweli na ambayo wanaweza kuyatetea. Nyuma yako watakusema vibaya, lakini hilo halipaswi kukusumbua, kwa sababu hujutii kukubaliana na usiyoyataka.

BORA KUHESHIMIWA KULIKO KUPENDWA.

Kitu kinachowafanya wengi kusema NDIYO hata kama hawataki ni kutaka kupendwa na watu wengine. Watu huona wakisema HAPANA watawaudhi wengine na hilo litafanya wasipendwe.

Pale unapofanya kitu chochote ili watu wakupende, huwa upendo huo haudumu muda mrefu. Na hivyo kulazimika kuendelea kufanya ili kuendelea kupendwa. Hilo linamfanya mtu kuwa kwenye utumwa ambao unakuwa mzigo kwake.

Unachopaswa kutafuta kwenye maisha siyo kupendwa, bali kuheshimiwa. Unaposema hapana, wengi hawatakupenda, lakini watakuheshimu kwa maamuzi yako. Na kwa sababu HAPANA yako ya sasa itakuwa na matokeo mazuri baadaye, utaheshimika kwa muda mrefu zaidi.

Usifanye chochote kutaka kupendwa, bali fanya kila kitu ili kuheshimika, kwa kusimamia yale yaliyo sahihi na yenye manufaa kwa wote.

NDIYO NAYO NI HAPANA.

Unapokuwa unahofia kusema HAPANA, ni kwa sababu tu unakuwa hujatafakari vizuri na kuona kushindwa kusema hapana nayo ni hapana. Pale unaposema NDIYO kwa wengine kwa sababu unakosa ujasiri, maana yake umesema HAPANA kwako mwenyewe. Unapowakubalia wengine kile ambacho hukuwa unataka, maana yake umejikatalia wewe kile ulichokuwa unataka.

Hivyo ni wajibu wako kuamua nani upo tayari kumwambia hapana, wewe au wengine. Chagua ni majuto gani yatakayokuumiza zaidi, kuwakatalia wengine au kujikatalia wewe mwenyewe?

Ukitafakari kwa kina, utaona wazi jinsi ambavyo ni wajibu wako wa msingi kabisa kusema HAPANA kwa wengine ili uweze kusema NDIYO kwako mwenyewe na uweze kufanya makubwa kwenye maisha yako.

MREJESHO WA SOMO.

Karibu kwenye mrejesho wa somo, kama sehemu ya kuthibitisha umesoma, kuelewa na kwenda kufanyia kazi. Karibu ujibu maswali yafuatayo;

1. Ni kitu gani hasa ambacho kimekuwa kinakufanya ushindwe kusema HAPANA, hata pale unapojua kabisa unapaswa kufanya hivyo?

2. Ni mazingira gani unayoenda kujitengenezea ambayo yatakulazimisha kusema hapana?

3. Ni ugumu gani unaenda kuwawekea wengine kwenye eneo la fedha ili usiwe rahisi kusema ndiyo?

4. Ni ndiyo gani kubwa kwako ambayo haupo tayari kuivunja kwa kushindwa kuwaambia wengine hapana?

5. Karibu uulize swali lolote ulilonalo kuhusu somo hili na progamu nzima ya NGUVU YA BUKU.

Tuma majibu ya maswali hayo kama sehemu ya kushiriki somo hili kwa ukamilifu na kwenda kuchukua hatua kwenye haya uliyojifunza.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.