3416; Ni wa kuonewa huruma.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,
Pale tunapoona wengine wanafanya mambo yao, huwa ni rahisi kudhani wanajua kile wanachofanya au kule wanakoenda.

Kwa kuwaona jinsi ambavyo watu wametingwa na kufanya, unaweza kuwaonea wivu kwa juhudi wanazoweka na kuonekana kuwa tayari wameshajipata.

Ni mpaka pale utakapoangalia matokeo wanayozalisha ndiyo utagundua hupaswi kuwaonea wivu watu hao, bali unapaswa kuwaonea huruma.

Wengi wamekuwa wanazalisha matokeo madogo sana ukilinganisha na juhudi kubwa wanazoweka.
Licha ya kuweka juhudi na kujitoa hasa, matokeo wanayopata yanakuwa duni sana.

Sababu kubwa ya matokeo duni ambayo watu wanakuwa wanayapata ni mtazamo wanaokuwa nao.
Wanakuwa na mtazamo hasi ambao unawazuia kupata matokeo mazuri licha ya juhudi wanazokuwa wanaweka.

Watu hao ni wa kuonewa huruma kwa sababu mtazamo ukishakuwa siyo sahihi, mtu atahangaika sana, lakini hataweza kuzalisha matokeo mazuri.

Licha ya matokeo duni ambayo watu hao wanakuwa wanayazalisha, bado huwa wanajiona wako sahihi kuliko watu wengine wote.
Wanaamini zaidi kwenye njia zao kuliko njia nyingine mbadala.
Na hivyo ndivyo mtazamo mbovu wanaokuwa nao unavyozidi kuwazamisha.

Pamoja na kwamba kufanya kazi kwa juhudi ndiyo msingi mkuu wa mafanikio, tunapowaangalia wengine, tusione tu juhudi wanazoweka. Bali tuangalie na matokeo wanayopata.
Kama matokeo ni madogo sana kulinganisha na juhudi zinazowekwa, huku watu hao wakiamini zaidi kwenye njia zao, jua hapo unapaswa kuwaonea huruma.

Unawaonea huruma kwa sababu wanajikwamisha wao wenyewe, lakini hawalioni hilo. Hivyo watazidi kupotea kwa kila juhudi wanazoweka.

Tatizo la kuwa na mtazamo usio sahihi ni kujiamini kupitiliza.
Hivyo hakuna namna mtu ataweza kujifunza kile kilicho sahihi na kubadilika.
Ndiyo maana tunapaswa kuwaonea huruma, maana hakuna njia yoyote wanaweza kusaidiwa.

Swali ni je watu hao ambao wana mtazamo mbovu hakuna namna wanaweza kusaidiwa wakabadilika?
Jibu ni njia zipo, ila tatizo ni wao kukubali tatizo.
Wengi hawapo tayari kukubali kwamba wanakosea na hilo ndiyo linafanya mambo kuwa magumu.

Usiache kuwaonyesha watu pale wanapokosea na kama watakukatalia basi waonee huruma kwa aina hiyo ya maisha ambayo wamechagua.

Kwa upande wa pili, hakikisha wewe huwi mgando kama wengine wengi.
Kila wakati pitia matokeo unayozalisha na linganisha na juhudi unazoweka.
Kama kuna namna vitu hivyo haviendani, jua kuna mahali kuna makosa. Kuwa tayari kukubali makosa hayo na kuyarekebisha ili uweze kupiga hatua kubwa.

Kwa ustaarabu wa ngazi hiyo, lazima utaweza kupata chochote unachotaka.
Kwa ambao hawajaweza kufikia huo ustaarabu, unapaswa kuwaonea huruma kwa sababu wanajikwamisha sana.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr Makirita Amani.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe