3420; Inachukua muda zaidi.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,
Kwenye mambo yote tunayoyafanya kwenye maisha yetu, yale ambayo ni muhimu zaidi, huwa yanachukua muda mrefu zaidi.
Haijalishi tumeyapa mambo hayo muda mwingi kiasi gani, bado yatachukua muda mwingi kuliko ambao umepanga.

Kujua ukweli huu kuhusu muda wa kufanya mambo muhimu kuwa mwingi zaidi, unatusaidia kwa njia mbili;

Moja ni kuanza mapema.
Mara nyingi huwa tunachelewa kuanza kufanya mambo kwa sababu tunaona muda tunao mwingi.
Tunapokuja kuanza na muda kwenda mwingi kuliko tulivyotarajia, tunaona tunachelewa.
Kama tungeanza mapema, hata kama muda unahitajika zaidi, hatuwi na haraka maana muda tunao.

Mbili ni kufanya bila kuangalia muda.
Unapopanga muda ambao utahitaji kufanya kitu na kisha kufanya ukiwa unaangalia muda, ni rahisi kukata tamaa pale muda unapoisha na matokeo uliyotegemea hayajapatikana.
Usifanye kitu kwa kuangalia muda, bali angalia umuhimu wake. Anza kufanya vitu ambavyo ni muhimu zaidi na nenda navyo mpaka utakapokamilisha.
Hiyo ni kwa sababu matokeo yanazalishwa na vitu ulivyokamilisha kufanya na siyo muda ambao umeweka kwenye kufanya kitu.

Kama kitu ni muhimu, unakifanya mpaka kukikamilisha na matokeo mazuri yanatokana na kukamilisha siyo muda uliofanya.
Hivyo peleka muda wako wote kwenye kufanya mambo ambayo ni muhimu mpaka yakamilike.
Ni yale yaliyokamilika ndiyo yanayoleta mabadiliko kwenye maisha yako.

Anza kufanya mapema na fanya bila ya kuangalia muda, hayo ndiyo ya msingi kuzingatia kwenye ufanyaji wa mambo ambayo ni muhimu zaidi kwenye maisha yako na kupata matokeo makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe