Rafiki yangu mpendwa,

Huwa kuna kauli kwamba mtoto halali na hela.

Upande wa pili wa kauli hiyo ni mpumbavu hashindi na hela.

Hiyo ina maana kwamba, mpumbavu akiwa na fedha, anatenganishwa nazo haraka sana.

Swali ni nani ni mpumbavu na kwa jinsi gani anatenganishwa na fedha zake haraka? Hayo unakwenda kujifunza hapa ili usiwe mpumbavu na kutenganishwa na fedha zako.

Rafiki, maana ya mpumbavu ni mtu ambaye hajui, lakini hajui kwamba hajui. Au hajui, lakini anaamini anajua. Au anaona tayari anajua kila kitu hivyo hana haja ya kujifunza.

Kwa njia hiyo, mpumbavu anakuwa anapata matokeo yale yale ambayo siyo mazuri, lakini bado habadiliki. Anarudia kufanya vile vile, huku akitegemea matokeo ya tofauti. Matokeo yakija vile vile, anarudia tena kile kile. Ah inachosha kweli kuwa mpumbavu.

Inapokuja kwenye fedha, mpumbavu ni mtu ambaye amekuwa anafanya shughuli ya kumwingizia kipato, kwa miaka zaidi ya 10, lakini hana akiba wala uwekezaji wowote. Zaidi anakuwa na madeni ambayo ni makubwa kuliko hata alipokuwa hana kipato.

Mpumbavu haoni haja ya kujifunza kuhusu fedha na utajiri, yeye anachojua ni PATA PESA, TUMIA PESA. Ndiyo anakuwa anafanya hivyo kwa maisha yake yote na kushangaa kwa nini maisha yanakuwa magumu kwake. Akipata fursa ya kujifunza chochote kuhusu fedha, anasema tayari anajua. Lakini maisha yake hayaonyeshi kama anajua chochote kuhusu fedha.

Kwa kutokujua misingi sahihi ya fedha na utajiri, wapumbavu huwa wanatenganishwa na fedha zao haraka sana. Yaani hata ile fedha kidogo wanayokuwa nayo, huwa wanaipoteza haraka kwa kukosa misingi sahihi ya kifedha.

Kwa kuwa hawana misingi sahihi ya kifedha na wanataka sana fedha, wapumbavu wa kifedha huwa ni rahisi kuamini njia za mkato za kujenga utajiri. Anaposikia kuna njia ya mkato ya kujenga utajiri wa haraka bila ya kufanya kazi, huwa wanaikimbilia haraka. Mwishowe ni wanaishia kutapeliwa na kupoteza hata pesa kidogo waliyonayo.

SOMA; Kanuni Ya Kukokotoa Utajiri Unaotakiwa Kuwa Nao Kulingana Na Umri Wako.

Rafiki, usiniamini mimi, bali amini tafiti mbalimbali na uhalisia ambao upo. Tukianza na tafiti, zinaonyesha kwamba watu wengi wanaocheza michezo ya bahati nasibu huwa ni masikini. Na kama wangewekeza kiasi wanachopoteza kwenye michezo hiyo, wangekuwa na unafuu kifedha.

Tukienda kwenye uhalisia, jiulize watu unaowafahamu ambao walipata fedha nyingi kwa pamoja. Labda walishinda bahati nasibu, walipata urithi, walipokea mafao au kulipwa fidia. Ukiwaangalia miaka miwili baada ya kupata fedha hizo nyingi maisha yao yanakuwaje?

Unajua kwamba wengi sana wa wanaopata fedha nyingi kwa mkupuo, huwa wanaishia kuzipoteza zote kwa haraka sana. Huo ndiyo mfano halisi wa jinsi mpumbavu anavyotenganishwa na fedha zake haraka sana.

Rafiki, wewe usikubali kuwa mpumbavu kwenye fedha na kutenganishwa na fedha zako haraka. Badala yake jifunze msingi wa USIMAMIZI WA FEDHA BINAFSI ili uweze kutumia fedha zako vizuri na kujenga utajiri mkubwa kwenye maisha yako.

Karibu kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA hapo chini ujifunze kuepuka kuwa mpumbavu na kupoteza fedha zako unazozipata kwa taabu sana.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.