3421; Matatizo kama kichocheo.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Watu wengi ambao wanashindwa kupata mafanikio makubwa kwenye maisha yao, huwa wanasingizia matatizo makubwa waliyonayo kama ndiyo kikwazo kilichowazuia.
Lakini unapowaangalia wale wachache ambao wameweza kujenga mafanikio makubwa sana, huwa wana matatizo makubwa sana kuliko watu wengine.
Yaani wale wanaofanikiwa sana, huwa wana matatizo makubwa sana kwenye maisha yao kiasi kwamba kufanikiwa inakuwa rahisi kwao kuliko kutatua matatizo waliyonayo.
Kwa maneno mengine, wale wanaofanikiwa sana huwa kuna matatizo makubwa wanayokuwa nayo, ambayo ndiyo yanakuwa kichocheo kwao kufanikiwa.
Kwa jinsi matatizo yao yanavyokuwa makubwa, kufanikiwa kinakuwa kipengele kidogo zaidi kwao.
Hivyo wale wanaotumia matatizo kama kikwazo kwao kufanikiwa, ni kama wanashindwa kutumia kichocheo ambacho ni sahihi kwao.
Yaani mtu anakuwa na kichocheo cha kufanikiwa, lakini anashindwa kukitumia kufanikiwa.
Lakini pia wengi wanajikuta wakihangaika kuyatatua matatizo waliyonayo na hilo kuwachukulia rasilimali zao nyingi, kitu kinachowazuia kujenga mafanikio makubwa.
Hapa mtu anayaona matatizo kama kikwazo na hivyo kuyatatua.
Kwa ukubwa wa matatizo hayo na kuwa yanahusisha mambo mengi, kuyatatua inakuwa kazi kubwa zaidi kuliko kufanikiwa.
Kilicho sahihi ni mtu kuyatumia kwanza matatizo anayopitia kama kichocheo cha kupata mafanikio makubwa zaidi.
Halafu kuja kuyatatua matatizo hayo baadaye, baada ya mtu kuwa ameshajenga mafanikio makubwa.
Hivyo kipaumbele cha kwanza kwako kinapaswa kuwa ni kufanikiwa.
Na kila unachopitia au kukutana nacho, unapaswa kukitumia kama msukuko wa kujenga mafanikio makubwa.
Hata kama kitu kinaonekana kuwa ni kikwazo kikubwa kiasi gani, usiruhusu kikayaingilia mafanikio yako.
Tumia kila unachokutana nacho kama rasilimali.
Chukulia mafanikio unayojenga kama kuwasha moto mkubwa.
Kadiri moto unavyochochewa, ndivyo kila kinachowekwa kwenye moto huo kinavyozidi kuuchochea.
Maji ambayo yanaweza kuzima moto mdogo, yanachochea moto mkubwa kuwaka zaidi.
Yote unayolalamikia kuwa kikwazo kwako kufanikiwa, ndiyo sababu kwa nini unapaswa kufanikiwa. Ndiyo unayopaswa kuyatumia kama kichocheo kikuu cha mafanikio yako makubwa.
Usipoteze fursa zote nzuri ulizonazo, zinazoonekana kwako kama matatizo.
Usikimbilie kuyatatua matatizo unayokuwa nayo. Yatumie kwanza kama kichocheo cha kujenga mafanikio makubwa. Ukishayajenga hayo mafanikio ndiyo unaweza kuyatatua.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe