Habari njema Matajiri Wawekezaji,

Karibuni kwenye mfululizo wa masomo yetu ya programu ya NGUVU YA BUKU, programu yenye lengo la kutuwezesha kujenga utajiri na uhuru wa kifedha. Tunafanya hilo kupitia uwekezaji kwa msimamo na muda mrefu bila kuacha au kuvuruga.

Inapokuja kwenye kujenga utajiri na uhuru wa kifedha, uwekezaji ambao ndiyo njia yetu kuu, ni kitu cha mwisho kabisa. Kabla ya kufika kwenye uwekezaji, kuna hatua za msingi ambazo mtu unapaswa kuzipitia ili uweze kuwekeza kwa ukubwa na kujenga utajiri kwa uhakika.

Kama hatua za awali hazitafanyiwa kazi kwa uhakika, hatua ya mwisho ya uwekezaji itakuwa ya kusua sua na hivyo kukwamisha kujenga utajiri mkubwa.

Ili tuweze kuwekeza kwa uhakika na kwa muda mrefu kisha kunufaika, ni lazima tuwe na mpango mzima wa usimamizi wa fedha binafsi.

1. ONGEZA KIPATO.

Kipato chochote ambacho mtu unakuwa nacho, huwa hakitoshelezi kuishi maisha ambayo mtu unataka. Udogo wa kipato huwa unaathiri ubora wa maisha, uwezo wa kuweka akiba na hata kufanya uwekezaji. Hivyo ili kuhakikisha unaweza kuweka uwekezaji kwa mwendelezo, huku maisha yako yakiwa bora, unapaswa kuwa unaongeza kipato kadiri muda unavyokwenda.

Ukiwa umeajiriwa, ongezeko la kipato linakuwa nje ya uwezo wako, hivyo unapaswa kuwa na shughuli za kuingiza kipato nje ya ajira. Ukiwa umejiajiri au kufanya biashara, unapaswa kufikia watu wengi zaidi ili kuweza kukuza kipato chako zaidi. Kwa kila kipato unachoongeza, usikimbilie kuongeza matumizi, badala yake ongeza kwanza akiba na uwekezaji unaofanya.

2. DHIBITI MATUMIZI.

Tunaendelea kukumbushana kwamba msingi wa kwanza wa kujenga utajiri ni matumizi kuwa pungufu ya kipato. Haijalishi kipato chako ni kidogo au kikubwa kiasi gani, matumizi yako yanapaswa kuwa pungufu ya kipato chako. Hivyo kila wakati unapaswa kudhibiti matumizi yako ili yawe chini ya kipato chako. Kamwe usitumie zaidi ya kipato chako, kwa sababu gharama yake ni kubwa. Na pia usiache kuweka akiba kwa sababu kipato ni kidogo.

Kama kipato chako hakikutoshelezi, hata usipoweka akiba, bado hakitoshelezi. Hivyo suluhisho siyo kutokuweka akiba, badala yake weka akiba na kazana kukuza kipato chako. Ili kudhibiti matumizi, hakikisha unakuwa na bajeti ambayo inatimiza yale ya msingi zaidi na kisha kufanya matumizi kwa bajeti hiyo. Hakikisha hutoki nje ya bajeti kwa namna yoyote ile.

3. WEKA AKIBA.

Kwenye kila kipato unachoingiza, unapaswa kuweka akiba kwanza kabla ya kufanya matumizi. Hiyo ni kwa sababu matumizi huwa hayaishi, kadiri fedha zinapokuwepo, matumizi huwa yanaendelea kujitokeza. Akiba ndiyo mbegu kuu ya kujenga utajiri, kama hutaweza kuweka akiba, hakuna kitu kingine kitakachoweza kukusaidia kujenga utajiri. Lakini pia kuweka akiba ni tabia na siyo kipato, kazana kuijenga hiyo kuwa tabia yako ili kuweza kujenga utajiri.

Kwenye kila kipato chako, fanya kuweka akiba kuwa kipaumbele cha kwanza kwako. Weka kwanza akiba kabla ya matumizi. Jifunze kuendesha maisha yako kwenye kipato kinachobaki baada ya kuweka akiba. Unahitaji kuwa na akiba za aina mbalimbali, kulingana na maisha yako, lakini akiba ya dharura na ya malengo ya maendeleo uliyonayo ni muhimu kuweka ili uweze kutimiza hayo.

SOMA; Mpango Wa Uwekezaji Kwenye Mifuko Ya Pamoja Kulingana Na Umri.

4. ONDOKA KWENYE MADENI.

Kukosa nidhamu nzuri ya kifedha imepelekea watu wengi kuingia kwenye madeni ambayo yanakuwa mzigo mkubwa kwao kujenga utajiri. Madeni mengi huwa yana riba kubwa na hivyo mtu kujikuta anapoteza fedha nyingi kwenye kulipa madeni kuliko manufaa ambayo aliyepata kwenye kutumia fedha hizo. Hivyo kwenye mpango wako wa usimamizi wa fedha binafsi, kuondoka kwenye madeni ni kipaumbele kikubwa. Hiyo ni kwa sababu riba unayoweza kuwa unalipa kwenye madeni inaweza kuwa kubwa kuliko riba unayopata kwenye uwekezaji. Chukua mfano una mkopo ambao unalipa kwa riba ya asilimia 18 kwa mwaka, halafu unafanya uwekezaji ambao unapata asilimia 10 kwa mwaka, bado unapoteza fedha nyingi kuliko unazoingiza.

Kwenye mpango wako wa usimamizi wa fedha binafsi, kama upo kwenye madeni kwanza acha kabisa kukopa. Baada ya hapo weka mpango wa kulipa madeni yote uliyonayo, ukianza na madeni yenye riba kubwa ili uzibe matundu yanayopoteza fedha.

5. FANYA UWEKEZAJI.

Uwekezaji ndiyo njia yetu ya kujenga utajiri kwa muda mrefu na kwa uhakika. Uwekezaji unatokana na akiba ambazo unakuwa umezitenga kwenye kipato unachoingiza. Na uwekezaji unapaswa kufanyika kwenye maeneo ambayo yanakupa faida (gawio) na pia yanakuwa thamani. Wakati wa kukuza uwekezaji, ambapo bado unakuwa unafanya shughuli za kukuingizia kipato, gawio unalopata linapaswa kurudi kwenye uwekezaji na siyo kutumia.

Kwenye mpango wako wa usimamizi wa fedha binafsi, uwekezaji wa kiasi kidogo kidogo mara kwa mara una manufaa kuliko kusubiri mpaka upate kiasi kikubwa na kuwekeza mara moja. Hivyo kwa kila kipato, hakikisha unawekeza. Pia kwa kila kiasi cha fedha unachopata ambacho hakikuwa kwenye mipango yako, chote peleka kwenye uwekezaji. Pale unapokuwa unalipa madeni na ukayamaliza, kile kiasi ulichokuwa unalipa kwenye deni, chote kipeleke kwenye uwekezaji. Yote hayo ni kuhakikisha kadiri muda unavyokwenda kiasi unachowekeza kinaendelea kukua.

MJADALA WA SOMO.

Karibu kwenye mjadala wa somo kama sehemu ya kuthibitisha umesoma na kuelewa somo hili. Jibu maswali yafuatayo;

1. Upi mpango wa kuongeza kipato unaoufanyia kazi kwa sasa ili uweze kuwekeza kwa ukubwa zaidi?

2. Unadhibitije matumizi yako ili kuhakikisha hayazidi kipato chako? Unafanya nini pale mahitaji yanapokuwa makubwa kuliko kipato chako?

3. Unatumia kanuni gani kuweka akiba na uwekezaji kwa kila kipato? Je ni kiasi fulani au asilimia fulani ya kipato? Eleza kwa nini umechagua njia unayotumia na unahakikishaje kadiri muda unavyokwenda akiba na uwekezaji wako vinakua?

4. Je kuna madeni ambayo unayo sasa? Una mpango gani wa kuyalipa kwa haraka ili uache kupoteza fedha kupitia riba unazolipa? Kama haupo kwenye madeni unajizuiaje usiingie?

5. Karibu uulize swali lolote au mapendekezo yoyote uliyonayo juu ya programu hii ya NGUVU YA BUKU ili tuendelee kunufaika nayo zaidi.

Shirikisha majibu ya maswali haya kwenye maoni hapo chini kama sehemu ya ushiriki wako kikamilifu kwenye programu hii ya NGUVU YA BUKU.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.