Habari njema wauzaji bora kabisa kuwahi kutokea,

Karibuni kwenye mfululizo wa masomo yetu ya CHUO CHA MAUZO, kwenye eneo la maendeleo binafsi. Kupitia CHUO CHA MAUZO unapata fursa ya kujifunza kuwa muuzaji bora kuwahi kutokea na kufanya mauzo makubwa zaidi.

Kitu kimoja ambacho watu wote tunakipenda ni USHINDI. Na kama tukikosa ushindi kwenye maisha yetu, huwa tunatafuta ushindi kwenye mambo mengine ambayo tunaweza kujihusisha nayo.

Ndiyo maana kumekuwa na ushabiki mkubwa sana wa michezo kwa watu walio wengi. Ukiwasikiliza mashabiki wa michezo pale timu zao zinaposhinda, huwa wanasema wao wameshinda. Wakati hata hawakuwa kwenye uwanja wa michezo. Pale timu inaposhinda, mashabiki wake huwa wanajisikia vizuri, wanajivunia na hata kuvaa jezi za timu zao. Lakini timu ikishindwa, mashabiki huwa hawajisikii vizuri na wengi wanakuwa hawapo tayari hata kuvaa jezi za timu zao.

Huo ni mfano mmoja ambao unaonyesha jinsi ambavyo hitaji la ushindi lipo kwa kila mtu. Kadiri mtu anavyokuwa na ushindi mdogo kwenye maisha yake, ndivyo anavyokuwa na ushabiki mwingi, ili apate ushindi wa nje.

Kwa bahati nzuri sana, wewe kama muuzaji unayo fursa ya kupata ushindi mkubwa kupitia mauzo kiasi kwamba huhitaji kutafuta ushindi wa nje kwenye michezo na vitu vingine.

Wewe kama muuzaji unayo fursa kubwa ya kutumia USHINDI kuwa muuzaji bora na kufanya mauzo makubwa zaidi. Karibu ujifunze kwenye somo hili ili uweze kunufaika.

USHINDI NI WEWE.

Ushindi wowote kwenye maisha, huwa unaanzia ndani ya mtu. Timu mbili zinapoenda uwanjani, ushindi hauamuliwi pale kwenye uwanja, bali unakuwa umeamuliwa kwenye fikra na mitazamo ya wachezaji, kabla hata hawajafika kwenye uwanja wa mapambano. Ni wachezaji ambao wamejitoa kushinda kweli, ambao hawajaweka nafasi ya kushindwa ndiyo wanaoshinda kwa uhakika. Wachezaji ambao wanaingia uwanjani kinyonge, wanashindwa kirahisi sana.

Ushindi wako kwenye mauzo unaanza kabla hata hujakutana na mteja. Kwa kujiamini, kuwa na shauku na kuijua biashara yako, vinakupa ushindi kabla hata ya kukutana na mteja. Kwa kuona hakuna namna mteja anaweza kuendesha maisha yake bila ya kuwa na kile unachouza, inakupa ushawishi mkubwa wa kushinda kwenye mauzo. Mara zote jifikirie wewe kama mshindi na utaweza kupata ushindi mkubwa kwenye mauzo.

USHINDI NI MCHAKATO.

Watu wengi wanakosa ushindi kwa sababu wanachukulia ushindi kama matokeo ya mwisho, ya kupata kile wanachotaka. Na pale wanapokutana na changamoto inayowachelewesha kupata wanachotaka, wanajiona hawawezi tena kupata ushindi. Ukihesabu ushindi kama matokeo makubwa ya mwisho, unajiweka kwenye nafasi ya kuukosa ushindi, kwa sababu matokeo huwa yanachelewa kuliko yanavyotegemewa.

Wewe ufanye ushindi kuwa mchakato. Jihesabie ushindi pale unapokamilisha mchakato wako wa mauzo. Hata kama matokeo uliyotegemea hayajatokea, kama umekamilisha mchakato, huo ndiyo ushindi. Kwa mfano mchakato wako unapokuwa kupiga simu 100 kwa siku, ushindi wako ni kukamilisha simu hizo 100. Iwe umefikia lengo lako la mauzo au la, kama umekamilisha simu 100, huo ni ushindi. Hiyo ni kwa sababu kama utaweza kukamilisha mchakato huo kwa muda mrefu zaidi, matokeo ya mwisho yatakuja tu yenyewe. Hakuna namna unaweza kutekeleza mchakato kwa uhakika kwa muda mrefu na usipate matokeo mazuri.

USHINDI NI KUTOKUACHA KUFANYA.

Safari ya mafanikio kwenye kila eneo la maisha ni ndefu na yenye changamoto za kila aina. Huwa tunaweka mipango yetu ya jinsi tutakavyofanya na matokeo tutakayopata. Lakini uhalisia huwa unakuja tofauti kabisa na mipango tuliyoweka. Wanaoshinda na wanaoshindwa huwa wanatofautisha na nini kinachotokea baada ya mtu kukutana na vikwazo au changamoto. Wanaoshindwa ni wale ambao wanapokutana na vikwazo wanaacha kufanya. Washindi ni wale ambao wanapokutana na vikwazo huwa wanaendelea kufanya bila ya kuacha. Kwa kuendelea kufanya inawasogeza karibu zaidi na ushindi wanaokuwa wanautaka.

Hesabu ushindi kwako kuwa ni kutokuacha kufanya. Mara zote kaa kwenye mchakato ambao umeuchagua bila ya kuacha. Haijalishi unakutana na vikwazo na changamoto za aina gani, wewe endelea kufanya. Ni kufanya kwa muda mrefu bila kuacha ndiyo kunakupa matokeo unayoyataka. Ushindi unakuwa siyo matokeo hayo ya mwisho, bali uwezo wa kuendelea kufanya bila kuacha.

SOMA; Kuwa Mtu Wa Vitendo Na Siyo Maneno Ili Uwe Muuzaji Bora Na Kufanya Mauzo Makubwa.

USHINDI NI KUZUNGUKWA NA WASHINDI.

Tunajua jinsi ambavyo wale wanaotuzunguka walivyo na athari kwenye maisha yetu. Na pia tumeona hapo juu jinsi ambavyo timu ikishinda mashabiki wake wanajivunia na ikishindwa wanajificha. Inakuwa rahisi kwako kupata ushindi pale unapokuwa unazungukwa na washindi. Washindi wanakutia moyo wewe ushindi na wanakufanya uone ushindi unawezekana. Walioshindwa wanakukatisha tamaa na kukuzuia usipate ushindi, kwa sababu wataonekana ni wazembe.

Zungukwa na washindi ili upate msukumo wa kushinda. Shirikiana na wale ambao wanakufanya upate msukumo wa kufanya zaidi. Chagua watu wa mfano na mamenta ambao wanakufanya utake kupata ushindi mkubwa zaidi. Kwa njia hiyo utapata ushindi kwa uhakika.

USHINDI NI KILA SIKU.

Ushindi siyo matokeo ya siku moja, yaani kulala masikini na kuamka tajiri. Unapotaka kupanda mlima, huamki siku moja na kujikuta kileleni. Bali unapiga hatua moja baada ya nyingine na hatimaye unajikuta ukiwa kwenye kilele cha mlima. Hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye ushindi wa kila eneo la maisha, ni jinsi unavyoiishi kila siku ndiyo inaamua ushindi unaoupata. Ushindi kwenye maisha ni mkusanyiko wa siku nyingi ambazo mtu umeziishi kwa ushindi.

Ipangilie kila siku yako kuwa ya ushindi, kisha hakikisha unaiishi kila siku yako kwa mpango huo wa ushindi. Ushindi unaanza na wewe kuipangilia kila siku yako tangu kuianza mpaka kuimaliza, kisha kufuata mpango huo bila kuacha. Kuwa na orodha ya mambo unayoyafanya kila siku, ambao ndiyo utaratibu wako wa kila siku. Kisha hakikisha unafuata utaratibu huo kila siku. Pale unapokutana na mambo yanayokutoa kwenye utaratibu, hakikisha unarudi kwenye utaratibu wako kama ulivyoweka. Kadiri unavyoweza kuiishi kila siku kwa ushindi, ndivyo unavyopata ushindi kwenye yote unayofanya.

Ushindi kwenye maisha na mauzo kwa ujumla unaanza na wewe mwenyewe kuwa na mpango wa ushindi. Fanyia kazi haya uliyojifunza hapa ili uweze kutumia ushindi kuwa muuzaji bora na kufanya mauzo makubwa.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.