3422; Binafsi ina nguvu kubwa.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,
Maneno yanayoishia na binafsi yana nguvu kubwa sana kwenye mafanikio ambayo mtu unayapata.
Maneno hayo ni kama;
Maendeleo binafsi
Elimu binafsi
Majaribio binafsi
Ubobezi binafsi
Utegemezi binafsi.

Sehemu kubwa sana ya mafanikio inaanza na mambo ambayo mtu unafanya binafsi.
Namna unavyoyapambania mafanikio wewe mwenyewe, ndivyo unavyoweza kuyaathiri moja kwa moja.

Na hilo limekuwa sababu ya wengi kushindwa, kwa sababu wamekuwa wanapuuza mambo binafsi na kuhangaika kuiga ya wengine.

Huwa ni rahisi sana kufuata mkumbo wa yale ambayo wengine wanafanya.
Lakini ni nadra sana mambo hayo ya wengine yakawa yanaendana na sisi.
Hivyo tunaweza kuhangaika nayo, lakini hayawezi kuwa na mchango mzuri kwetu.

Mafanikio makubwa na ya kweli yanaanza na mambo binafsi.
Mambo binafsi ndiyo yanatumia vizuri kile kilicho ndani yako, ambacho ni cha kipekee na hakipatikani kwa wengine.

Hakuna ambaye amewahi kupata mafanikio makubwa kwa kuiga mambo ya wengine.
Kwa sababu kuiga ya wengine kunapuuza ule upekee ambao unao wewe tu.

Ni kwa kuanza na binafsi ndiyo unaweza kufanya makubwa sana kwenye maisha yako.

Maendeleo binafsi unajiendeleza wewe mwenyewe, kwa kuboresha yale ambayo yanakutofautisha kabisa na wengine.
Usiige ya wengine, kwa sababu huma uimara nayo.

Elimu binafsi ni kuchukua hatamu ya kujielimisha, kwenye yale ambayo yanaongeza tija kwako. Elimu binafsi inatumia maarifa mengi yaliyopo kujinoa kwenye maeneo ya msingi zaidi kwako.

Majaribio binafsi ni kufanya vitu ambavyo hujawahi kufanya ili kujifunza na kuboresha zaidi kile unachofanya. Ni kupitia majaribio ndiyo unajifunza njia mpya zinazokupa matokeo bora na ya tofauti.

Ubobezi binafsi binafsi ni kujitambua wewe binafsi na kujua uimara wako uko wapi na udhaifu uko wapi. Hapo unabobea zaidi kwenye uimara ulionao na kupuuza madhaifu uliyonayo.

Utegemezi binafsi ni kuhakikisha kwenye yale muhimu unayofanya huwezi kukwamishwa na wengine unaokuwa unawategemea. Haimaanishi kutokushirikiana na wengine, bado utashirikiana nao sana, lakini huweki nafasi ya kukwamishwa na hao wengine.

Zingatia sana neno binafsi kwenye yote unayofanya ili uweze kufanya makubwa zaidi kwenye maisha yako.
Wewe ni wa pekee, hayupo wa kufanana na wewe.
Unapofanyia kazi yale binafsi yanayokutofautisha na wengine ndiyo unajiweka kwenye nafasi ya kujenga mafanikio makubwa zaidi.

Kama hupigi hatua kubwa kama unavyotaka, hebu jichunguze ni juhudi kiasi gani unazoweka kwenye eneo la binafsi.
Ongeza hizo juhudi na utaweza kupiga hatua kubwa zaidi.
Uzuri ni una udhibiti wa asilimia 100 kwenye mambo yote binafsi hivyo huna wa kumlaumu kama hupigi hatua kubwa unazotaka.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe