Habari njema wauzaji bora kuwahi kutokea.

Karibuni kwenye mfululizo wa masomo yetu ya programu ya CHUO CHA MAUZO, yenye lengo la kutujenga kuwa wauzaji bora na kufanya mauzo makubwa.

Mkakati wetu mkuu kwenye CHUO CHA MAUZO ni kutengeneza wateja tarajiwa na kuwafuatilia wateja mara zote. Kwa kufanya hayo mawili, kufanya mauzo makubwa inakuwa ni matokeo ya uhakika.

Kwenye kutengeneza wateja tarajiwa, hatua ya kwanza ni kuwafikia kule walipo, ili kujua kuhusu uwepo wa biashara. Kwa sababu kikwazo cha kwanza cha mauzo ni wateja kutokujua kuhusu uwepo wa biashara.

Tumekuwa tunajifunza njia nyingi za kuwafikia wateja. Kwenye somo hili tunakwenda kujifunza matumizi ya Alama (logo) ya biashara na kadi za biashara (business cards) kuweza kuwafikia wateja wengi zaidi.

Alama na kadi ni vitu ambavyo vinakwenda pamoja, kwa sababu alama inaitambulisha biashara na kadi inakuwa na alama, ikimtambulisha mtu aliye ndani ya biashara.

MATUMIZI YA ALAMA (LOGO).

Alama ya biashara (Logo) huwa ndiyo utambulisho wa biashara. Ni kitu ambacho watu wanapokiona, wanajua kinahusika na biashara gani au kuwakilisha nini.

Alama inatengenezwa na biashara, ikiwakilisha yale ambayo yanafanyika kwenye biashara. Alama inaweza kuwa na maneno na/au viashiria vya biashara. Kwa mfano alama ya biashara ya ujenzi, inaweza kuwa na vifaa vya ujenzi au mfano wa jengo.

Alama pia huwa inaambatana na rangi kuu ambazo biashara inatumia na hivyo muunganiko wa alama na rangi, inafanya biashara kuweza kutambulika kwa haraka.

Baada ya biashara kuwa na alama, inapaswa kuitumia alama hiyo kwenye vitu vinavyohusiana na biashara ili kuwafanya watu waijue na kuizoea.

Kwenye mawasiliano yote ambayo biashara inafanya, alama inapaswa kuwepo. Kwenye mavazi ya biashara, alama inapaswa kuwepo. Kwenye matangazo, mabango na vifungashio, alama inapaswa kuwepo.

Ni muhimu alama itumiwe kwenye kila kitu ili wateja waizoee na kuihusianisha na biashara. Kwa watu kuizoea alama kwenye biashara, hata wanapokuja kukutana na alama yenyewe bila ya maelezo mengine, wanajua kabisa inahusiana na biashara fulani.

Makampuni makubwa huwa yana alama na rangi ambazo ukiziona tu, hata kama hujaambiwa ni kampuni gani na wala hakuna jina lake, tayari unajua ni kampuni ipi. Hilo ndiyo linapaswa kufanywa na kila biashara, kuizoesha alama yake kwa wengi zaidi.

SOMA; Kufikia Wateja Wengi Kwa Kutumia Matangazo Ya Kuchapa.

MATUMIZI YA KADI.

Kadi za biashara (business cards) zinatumika kuwatambulisha watu kwenye biashara. Kadi inakuwa na jina la biashara, alama ya biashara, rangi za biashara na mawasiliano ya biashara. Pia inakuwa na jina la mhusika wa kadi na cheo chake kwenye biashara.

Kadi huwa inatolewa kama sehemu ya kubadilishana mawasiliano kwa watu wanaokutana. Kuwa na kadi ya biashara na kuitoa kwa watu huwa inajenga hali ya kuaminika zaidi, kwa biashara kuonekana iko makini. Lakini pia matumizi ya kadi yanafanya mtu aaminike kweli anahusika na biashara na siyo tapeli anayetumia jina la biashara kutaka kujinufaisha.

Matumizi ya kadi kwenye kuwafikia wengi zaidi ni kuzigawa kwa watu ambao mtu unakutana nao kwenye maeneo mbalimbali. Pia kuziacha kadi kwenye maeneo ambayo ni rahisi watu kuzichukua. Kwa mfano kwenye mikutano au maonyesho, kadi zinaweza kuwekwa kwenye meza ambayo watu wanapita na kuvutiwa kuzichukua ili wawe na mawasiliano.

Kadi pia zinaweza kutumika kuwapa watu wanaokuletea wateja na kupata kamisheni. Pale unapowapa wateja fursa ya kupata kamisheni kama wataleta wateja na wakanunua, unaweza kuwapa kadi za biashara, ambazo watapaswa kuwapa wateja wanaowaambia waje na wakija na kadi hizo basi unawapa kamisheni kama watanunua. Hapa itahitaji kadi iwekewe alama au sahihi maalumu ya kugundua ni sahihi ili watu wasitumie fursa hiyo kujinufaisha.

MATUMIZI YA KADI KWENYE ZAMA ZA KIDIJITALI.

Kadi za biashara zilikuwa na nguvu kwenye zama ambazo teknolojia ya mawasiliano ilikuwa haijaboreshwa mpaka sasa. Watu hawakuwa na simu janja wala mitandao ya kijamii hivyo kupata mawasiliano ya watu haikuwa rahisi. Hiyo ililazimu biashara kuwa zinatumia kadi kutoa na kupata mawasiliano. Pia zilitunza kadi nyingi kama sehemu ya kanzi data ya wateja.

Kwa zama hizi za kidijitali, ambapo kupata na kutunza mawasiliano imekuwa rahisi, kadi zimekuwa zinaonekana hazina umuhimu mkubwa.

Pamoja na maendeleo hayo ya teknolojia, bado kadi zina umuhimu mkubwa kwenye biashara. Hivyo hakikisha wewe kama muuzaji unakuwa na kadi za biashara ili pale unapokutana na watu wengine, uweze kuwapa, hasa kama nao pia wanakupa kadi.

Lakini pia kadi hizo za biashara zinaweza kuandaliwa na kusambazwa kwa njia ya kidijitali, hivyo siyo lazima mpaka zichapwe na kugawiwa ana kwa ana. Kadi za biashara zinaweza kutumwa kwa njia za mawasiliano na mtandao na zikaweza kuwafikia wengi zaidi.

Kila biashara inapaswa kuwa na alama ambayo inaisambaza kwa ukubwa ili iweze kuhusianishwa na biashara hiyo. Na kila muuzaji aliyepo kwenye biashara anapaswa kuwa na kadi za biashara ambazo zitakuwa zimechapwa na pia zipo kidijitali ili aweze kuwasambazia watu wengi zaidi.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.