Rafiki yangu mpendwa,

Kinachowakwamisha watu wengi kujenga utajiri kwenye maisha yao ni kukosa elimu ya USIMAMIZI WA FEDHA BINAFSI.

Hii ni elimu muhimu sana ambayo imekuwa haitolewi kwa uhakika.

Mtu hawezi kuendesha gari kama hana leseni ambayo ni kiashiria amesoma na kufuzu kuendesha gari.

Lakini mtu anaruhusiwa kutumia fedha zake bila ya kuwa na cheti chochote cha kuwa amepata elimu ya matumizi sahihi ya fedha.

Inapokuja kwenye fedha na utajiri, kuna makundi matatu ya watu kulingana na kiwango cha elimu ya USIMAMIZI WA FEDHA BINAFSI waliyopata.

Kundi la kwanza ni wale wanaobaki kwenye umasikini.

Kundi hili huwa halina elimu kabisa ya USIMAMIZI WA FEDHA BINAFSI. Kitu ambacho kundi hili linajua ni PATA PESA, TUMIA PESA. Hawa wakipata pesa huwa wanatumia mpaka iishe. Na kama bado wana matumizi, wanatumia zaidi hata ya pesa waliyopata. Matokeo yake wanajikuta kwenye madeni ambayo yanawadidimiza zaidi kwenye umasikini.

Kundi la pili ni wale ambao wanatoka kwenye umasikini, lakini hawapati utajiri.

Kundi hili huwa lina elimu kiasi ya USIMAMIZI WA FEDHA BINAFSI. Wanakuwa wanajua kuhusu KUPATA, KUTUMIA NA KUWEKA AKIBA. Wanachokuwa wamewazidi kundi la kwanza ni wao kuweza kuweka akiba, kitu ambacho kinawaondoa kwenye umasikini. Kundi hili huwa linakuwa na matumizi ambayo ni pungufu ya kipato na kuweza kubaki na akiba.

Kundi hili huwa linatoka kwenye umasikini kwa sababu fedha haitumiwi yote. Kunakuwa na akiba iliyowekwa ambayo inawasaidia kwenye mambo mbalimbali ya kifedha.

Kinachozuia kundi hili kujenga utajiri ni fedha inayowekwa akiba huwa inapoteza thamani kadiri muda unavyokwenda. Hivyo akiba ikiwekwa kwa muda mrefu, inakuwa na thamani ndogo zaidi. Kama kundi hili litaishia kwenye akiba pekee, mwishowe linarudi kwenye umasikini.

SOMA; Mpango Wa Usimamizi Wa Fedha Binafsi (Personal Finance Management Plan)

Kundi la tatu ni wale ambao wanajenga utajiri.

Kundi hili huwa wanapata elimu kamili ya USIMAMIZI WA FEDHA BINAFSI. Ambapo wanajua kuhusu KUPATA, KUTUMIA, AKIBA NA UWEKEZAJI. Ni kupitia uwekezaji ndiyo kundi hili huweza kujenga utajiri mkubwa. Kwa sababu kwenye uwekezaji, fedha inafanya kazi na kuingiza faida huku pia uwekezaji ukikua thamani.

Wakati akiba pekee inaishia kupoteza thamani, uwekezaji unakuza zaidi thamani. Ndiyo maana wanaoishia kwenye akiba, hawajengi utajiri na wanakuwa na hatari ya kurudi kwenye umasikini.

Ni wale wanaofanya uwekezaji, tena kwa muda mrefu bila ya kuuvuruga ndiyo wanaofanikiwa kujenga utajiri mkubwa kwenye maisha yao. Kwa bahati nzuri sana, hicho ni kitu ambacho kila anayeingiza kipato anaweza kukifanya.

Ndiyo, wewe hapo rafiki yangu, kama tu una njia ya kuingiza kipato, unaweza kufanya uwekezaji utakaokujengea utajiri kupitia fursa mbalimbali zilizopo.

Tunayo programu ya NGUVU YA BUKU, ambapo kwa fedha ndogo ndogo ambazo umekuwa unapoteza kila siku, unaweza kuziwekeza na zikakuingizia kipato kikubwa sana. Karibu upate nafasi ya kujiunga na NGUVU YA BUKU kwa kuwasiliana na namba 0678 977 007.

Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA hapo chini nimefafanua kwa kina kuhusu dhana hii ya kuweka akiba kuwa chanzo cha kujenga umasikini. Karibu ujifunze ili ukamilishe elimu yako ya USIMAMIZI WA FEDHA BINAFSI ili uweze kujenga utajiri mkubwa na wa uhakika kwenye maisha yako, kwa kuanzia hapo hapo ulipo sasa. Fungua hapo chini kujifunza.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.