Rafiki yangu mpendwa,

Karibu kwenye mwendelezo wa masomo ya NJIA KUMI ZA KUJENGA UTAJIRI kutoka kitabu kinachoitwa THE TEN ROADS TO RICHES kilichoandikwa na Ken Fisher.

Kwenye masomo yaliyopita tumejifunza njia sita kati ya 10 za kujenga utajiri. Kwenye somo hili tunakwenda kujifunza njia ya saba na ya nane katika njia 10 za kujenga utajiri. Karibu ujifunze.

NJIA YA SABA; KUTUMIA FEDHA ZA WENGINE.

Kama unapenda kuwaambia watu nini wanapaswa kufanya na upo imara kukabiliana na hatari, njia ya kusimamia fedha za wengine inakufaa.

Hii ni njia ya kutoza ada kwa kusimamia fedha za wengine kama wakala, benki, bima, uwekezaji na nyingine.

Kwenye njia hii unapata utajiri kwa kuwawezesha wengine kupata utajiri, hivyo ni bahati ya kipekee kabisa.

Hii ndiyo njia inayozalisha matajiri wakubwa kwenye orodha za matajiri. Lakini pia ni njia yenye mitego mingi ya kuvunja sheria na kupelekea mtu kuishia jela.

Kufanikiwa kwenye njia hii unapaswa ujifunze na kuwa vizuri kwenye mauzo kwanza kabla hata ya kuwa vizuri kwenye fedha. Mauzo unaweza kujifunza haraka na mapema kuliko fedha.

Ukianza kwa kujifunza na kubobea kwenye mauzo, ambayo ni rahisi, unaweza kuingia kwenye njia hii na kuuza huduma zilizopo. Kisha kadiri muda unavyokwenda unaendelea kujenga uzoefu kwenye upande wa fedha na hivyo kupiga hatua kubwa zaidi.

Kuna njia mbili za kulipwa kwenye usimamizi wa fedha za wengine;

Moja ni kamisheni, ambapo unalipwa pale mtu anapofanya manunuzi ya bidhaa au huduma husika. Haya huwa ni malipo ya mara moja na hivyo inakutaka uendelee kutafuta wateja zaidi.

Mbili ni ada, ambapo mtu analipa ada ya kupata bidhaa au huduma husika. Malipo ya ada huwa ni ya kujirudia, hivyo mteja anapotunzwa vizuri, kipato huwa ni endelevu.

Zipo aina mbalimbali za usimamizi wa fedha binafsi kwenye uwekezaji. Kubwa mbili ni kama ifuatavyo;

1. Mfuko wa uwekezaji (Hedge Fund).

Hapa unaanzisha mfuko wa uwekezaji ambapo unawashawishi watu kuwekeza mitaji yao kwenye mfuko wako na wewe kwenda kuwekeza kwenye soko la hisa. Hapa unawaahidi watapata faida kubwa kupitia mfuko huo kuliko wakienda kuwekeza wenyewe sokoni ambapo changamoto ni nyingi.

Kwenye njia hii malipo huwa ni 2 na 20. Mfuko unatoza asilimia 2 ya mali iliyopo kwa mwaka na asilimia 20 ya ongezeko la mwaka.

Hii mifuko huwa ni hatari na huishia kupata hasara na kushindwa kulizidi soko. Hivyo siyo sehemu ya mtu kuweka utegemezi mkubwa.

2. Mitaji binafsi (Private Equity).

Kwa njia hii, uwekezaji unafanyika kwenye makampuni kwa lengo la kuyauza kwa faida baadaye. Kwa njia hii, makampuni ambayo hayafanyi vizuri yananunuliwa, kwa bei ndogo, yanaboreshwa na kufanya vizuri kisha kuuzwa kwa bei kubwa.

Njia ya mitaji binafsi inafanya vizuri na ni ya uhakika zaidi pale inapofanyiwa kazi vizuri. Kwa sababu biashara zinapoboreshwa, wengi wananufaika. Japo siyo njia yenye sifa nzuri kwa wengi, kwa sababu ya faida yake kubwa. Ili uweze kudumu na kufanikiwa kwenye njia hii, unapaswa kuupenda sana ubepari.

Kufanikiwa kwenye njia ya usimamizi wa fedha za wengine, epuka sana kuvunja sheria. Epuka ushawishi wa kutumia fedha za wengine tofauti na malengo na mipango iliyopo.

Hata kama unaona kuna uhakika wa faida kubwa, epuka sana kushawishika kwenda kinyume na sheria au mipango. Wote waliopita njia hizo hawakuishia pazuri. Epuka sana njia hizo.

Njia ya usimamizi wa fedha za wengine imejaa utapeli mwingi. Wapo watu wanaokuja na mipango inayoonekana ni mizuri na yenye faida, lakini inaishia kuwaumiza watu.

Kuwajua matapeli kwenye fedha, angalia yafuatayo;

1. Ahadi ya faida kubwa na ya uhakika bila ya kuwepo kwa hatari ya kupoteza.

2. Usimamizi wa mali na fedha unakuwa juu ya hao matapeli, wewe unayetapeliwa hupewi nafasi katika maamuzi yoyote.

3. Mikakati migumu kueleweka na matumizi ya misamiati migumu.

4. Kujisifia na kujionyesha wanajulikana na watu mashuhuri.

Unapoona viashiria hivyo, kuwa na tahadhari ili usiishie kutapeliwa.

JINSI YA KUTUMIA NJIA HII.

Kama unapenda uwekezaji na wewe mwenyewe umeweza kusimamia fedha zako vizuri, unaweza kutumia njia hii kuanzisha mfuko wa uwekezaji. Jua sheria zinazosimamia hilo na chukua hatua sahihi.

Hata kama hutaanzisha mfuko wako, unaweza kuwa muuzaji wa bidhaa na huduma za fedha na uwekezaji za makampuni na taasisi nyingine. Kwa kuwa una uelewa na wewe mwenyewe ni mwekezaji, utaweza kuuza vizuri na kulipwa kamisheni.

Kwa upande wako, waepuke wale wanaokuja kwako na utapeli uliojificha nyuma ya uwekezaji. Zingatia vigezo vya kujua matapeli ulivyojifunza hapa ili usiishie kuwanufaisha wengine.

SOMA; Kujenga Utajiri Kupitia Ndoa Na Kesi.

NJIA YA NANE; GUNDUA KIPATO.

Kama una ubunifu wa kipekee au unaweza kuja na wazo la tofauti na likaingiza kipato endelevu, basi njia ya kugundua kipato ni yako.

Kwenye njia hii unatengeneza kipato endelevu kupitia kitu ambacho umetengeneza na kukimiliki au una hatimiliki yake na kuwaruhusu wengine kutumia kwa kukulipa. Vitu hivyo vinaweza kuwa vitabu, nyimbo, sinema, programu za kompyuta, n.k.

Kwenye njia hii, ukishakuwa na umiliki au hati miliki ya kitu, unalipwa kila mara mtu anapokinunua au kukitumia, japokuwa unakuwa hufanyi kazi ya moja kwa moja kwenye kitu hicho. Unakuwa umefanya kazi mara moja lakini unalipwa milele.

Wachache sana ndiyo walioweza kujenga utajiri mkubwa kwenye njia hii. Na hawa walikuwa na ugunduzi wa njia nyingi za aina hiyo badala ya moja pekee. Yaani wanakuwa wamezalisha vitu vingi hivyo wanapolipwa kidogo kidogo kwenye kila kimoja, wanajenga utajiri mkubwa.

Kwenye njia hii unaweza kudhani kazi yako ni kugundua tu kitu kisha kulipwa milele. Lakini siyo, baada ya ugunduzi kuna kazi kubwa ya kukitangaza kitu ili kijulikane na wengi na watake kukitumia au wawe nacho. Hivyo ni lazima uwe vizuri sana kwenye masoko kuhakikisha ulichogundua kinajulikana na wengi na wanashawishika kukitumia.

Uzuri ni kwamba ukiwa vizuri kwenye ugunduzi na masoko, lakini njia hii ikakushinda kujenga utajiri, unaweza kwenda kwenye njia ya kwanza na kugeuza ugunduzi wako kuwa biashara. Pia unaweza kwenda kwenye njia ya kumi na kuweka akiba na kuwekeza kila unachopata ili kujenga utajiri.

JINSI YA KUTUMIA NJIA HII.

Kwa mawazo yoyote uliyonayo ya kufanya vitu kuwa bora zaidi, yafanyie kazi ili kuja na bidhaa au huduma ambayo inaboresha maisha ya watu. Unapaswa kuiweka kwa mfumo ambao ukishafanya kazi mara moja umemaliza, wewe unaendelea kulipwa milele.

Njia rahisi ni kuandika kitabu au kuandaa mafunzo ya sauti na video ambayo yanaweza kuuzwa kwa watu kwa muda mrefu na ukawa unaingiza kipato japo hufanyi tena kazi ya moja kwa moja.

Ugunduzi wowote unaoweza kuja nao ambao utafanya maisha ya watu kuwa bora, utaweza kukuingizia kipato hata kama siyo kikubwa, lakini ukikiwekeza vizuri kwa njia ya 10, utaweza kujenga utajiri.

Kwenye somo hili tumeona njia ya saba na ya nane ya kujenga utajiri kwa uhakika. Masomo ya njia zote kumi za kujenga utajiri kutoka kitabu THE TEN ROADS TO RICHES yanapatikana kwa KUBONYEZA MAANDISHI HAYA.

Tumekuwa na mjadala mzuri wa somo hili kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA. Karibu uweze kusikiliza kipindi hicho ujifunze mengine mengi ambayo yapo kwenye kitabu ila hapa hayajapata nafasi. Pia usikie maoni ya wengine juu ya njia hizi za kujenga utajiri.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.