Habari njema muuzaji bora kuwahi kutokea,
Hongera na karibu sana kwenye mwendelezo wa makala zetu za ushawishi kutoka kwenye programu yetu ya CHUO CHA MAUZO.
Kwenye jumamosi ya ushawishi tunaongozwa na kauli mbiu yetu inayosema HUPATI UNACHOSTAHILI BALI UNACHOSHAWISHI.
Wiki iliyopita tulifanikiwa kujifunza jinsi ya kuwafanya watu wakubaliane na mawazo yako kanuni ya nane ambayo ni jiweke kwenye nafasi ya mtu mwingine.
Na kwenye kanuni ya nane tulifanikiwa kuondoka na kitu kimoja ambacho ni Kabla hujamtaka mtu afanye kitu chochote kile, jiweke kwanza kwenye nafasi yake, jua nini kinaweza kumsukuma afanye unachotaka afanye. Iwe ni kitu unauza au mchango unaomba, usifikirie wewe unataka nini, bali yule unayemshawishi anataka nini. Kwa kujiweka kwenye nafasi yake, na kuwa na mtazamo wake, utapata njia sahihi ya kumshawishi afanye unachotaka afanye.
Kama ulipaswa kundoka na kitu kimoja kwenye kanuni ya nane ni, mara zote fikiria kwa kujiweka kwenye nafasi na mtazamo wa mtu mwingine, ona vitu kama anavyoona yeye na kisha kama unavyoona wewe, na hilo litakusaidia kwenye kuwashawishi watu na kupata unachotaka.
Habari njema ni kwamba leo kwenye jumamosi ya ushawishi, tunakwenda kujifunza jinsi ya kuwafanya watu wakubaliane na mawazo yako kanuni ya TISA ambayo ni wahurumie wengine kwa mawazo na matakwa yao.
SOMA; Jinsi Ya Kuwafanya Watu Wakubaliane Na Mawazo Yako Kanuni Ya Saba
Mpendwa muuzaji bora kuwahi kutokea,
Sisi binadamu ni viumbe vya hisia, huwa tunaguswa na vitu vya kihisia zaidi kuliko hata vya mantiki. Na kupitia hisia, ndiyo ubinadamu wenyewe upo. Tuna hisia mbalimbali kama vile hisia za upendo, huruma, wivu nk. Hisia ndiyo huwa zinatukusukuma sisi binadamu kuchukua hatua. Hata manunuzi mengi ambayo watu wanakuwa wanafanya ni kwa sababu ya hisia ziliwasukuma kufanya hivyo.
Kwenye hisia za watu, ndiyo mahali ambapo maumivu ya mtu yalipo. Na kila hisia anayokuwa nayo mtu juu ya kitu fulani, jua kuna kitu anakihitaji kupitia hisia hiyo, kwenye kila hisia ya mtu, kuna hali ya matarajio fulani anategemea kupata.

Kinachosababisha hata sisi binadamu kutofautiana ni kwa sababu ya hisia tulizokuwa nazo. Hisia tulizonazo, zinapelekea kuwa na mtazamo tofauti katika mambo fulani.
Kuna wakati unaweza kupitia hali ya magumu (tough time) kiasi cha kuhitaji msaada kutoka kwa wengine hata tu wa kusikia pole, au mtu wa kukusikiliza na kumwelezea hisia ulizonazo juu ya kitu fulani. Na ukitaka kuwa muuzaji bora katika eneo la kusikiliza pale mtu anapopitia changamoto fulani na anahitaji kusikia huruma yako ili uwahurumie wengine kadiri ya mawazo au matakwa yao, ipo kauli moja ambayo ukiitumia itamfanya mtu yeyote yule atulie na kukusikiliza, hata kama angekuwa na hasira au huzuni kiasi gani.
Kauli hiyo inamfanya mtu ajisikie vizuri licha ya hali anayopitia, aache ubishi na kukusikiliza kwa umakini. Je, kauli hiyo ni kauli gani?
Kauli yenyewe ni hii; ” sikulaumu hata kidogo kwa jinsi unavyojisikia, hata mimi ningekuwa wewe, ningejisikia kama unavyojisikia sasa”
Hii ni kauli ya kihisia, ambayo inapenya ndani ya akili za mtu, ni kauli ambayo inakusaidia kuvaa viatu vya mwingine. Kwa mfano, wewe kama muuzaji, mteja wako anapokuwa anapitia changamoto fulani, utakavyomwambia pole, sikulaumu hata kidogo kwa jinsi unavyojisikia, hata mimi ningekuwa wewe ningejisikia kama unavyojisikia sasa.
Kwa kauli hiyo, ni rahisi kujenga ushawishi kwa mtu huyo na kupendekeza mawazo ya na mwisho akakubaliana na wewe.
Kauli hiyo ina nguvu ya kumbadili mtu yeyote bila ya kujali yuko kwenye hali gani, kwa sababu umeonesha kujali hali aliyonayo au anayopitia. Unapaswa kusema hivyo ukiwa ukiwa na uhakika wa asilimia 100 kwa sababu ni kweli, ungekuwa kama mtu huyo, ungefikiri na kufanya kama alivyofanya yeye.
Unafikiri kwa nini wewe siyo ng’ombe? Jibu ni kwa sababu wazazi wako hawakuwa ng’ombe. Hivyo unatofautiana na kila mtu kwa sababu mmezaliwa na kukulia kwenye mazingira ya tofauti. Mtu aliyezaliwa na kukulia kwenye mazingira ambayo hakuna uaminifu, anajifunza tangu mdogo kutokuwa mwaminifu.
Hivyo kabla hujamlaumu mtu kwa kukosa uaminifu, jua hata wewe ungekulia kwenye mazingira aliyokulia yeye, ungekuwa na tabia kama yake.
Kauli hiyo inamfanya mtu aone unamthamini, hujioni wewe ni bora kuliko yeye, bali mnatofautiana. Kwa kuchukulia hivyo, anakuwa tayari kukusikiliza na kujaribu kubadilika ili asiendelee kuwa kwenye hali aliyonayo.
Pia kauli hiyo ina nguvu kwa sababu humhukumu mtu kama wengi wanavyofanya, badala yake unamuonea huruma. Unajua ugumu anaopitia na hilo linamfanya afarijike zaidi.
Tambua kwamba watu unaokutana nao ambao wana hasira, ghadhabu, wamevurugwa na mengi na hisia nyingine za aina hiyo hawapendi kuwa nazo. Waonee huruma na wasikilize, watakuwa tayari, kukubaliana na wewe kwa kuwapokea hivyo walivyo kuliko kuwahukumu.
Kitu kimoja zaidi, wewe kama muuzaji bora kuwahi kutokea, unatakiwa kujua kwamba, sehemu kubwa ya watu unaokutana nao, wana kiu ya huruma, wape huruma na watakupenda na kukubali. Kwa mfano, hata kwenye mahusiano yetu ya kawaida, watu wanakuwa na visirani vyao wewe waonee huruma, wape huruma kwa kile wanachopitia na utakua na nguvu ya ushawishi kwao.
Hata mtu anapokuja kwako akiwa na hasira na maneno makali, akikulaumu kwa kitu ulichofanya, usikimbilie kujitetea au kuwahukumu, badala yake waonee huruma, waambie unaelewa kwa nini wamefikia kwenye hali hiyo.
Mwisho watakosa cha kuendelea kupambana na wewe na mtasikilizana na mwisho mtakubaliana.
Kwa mfano, hivi karibuni nilikutana na mtu ambaye amevurugwa kweli, ni mteja ambaye nilimpata kupitia matangazo ya Metabusiness, mteja huyo alikuwa anapitia changamoto fulani, baada ya kuwasiliana kwa simu, aliniongelesha kwa maneno makali kweli, nilimuonea huruma kwa hali anayopitia na kumpa pole nikakata simu, baada ya muda alikuja kunipigia na kuniomba msamaha kwa kwamba alikuwa amevurugwa kweli na kitu fulani ndiyo maana alinijibu vibaya na kwa maneno makali.
Mwandishi Dale Carnegie anamnukuu mwanasaikolojia Arthur I. Gates ambaye amewahi kuandika kila binadamu anataka zaidi huruma. Watoto huwa wanaonesha vidonda vyao na hata mara nyingine kujiumiza ili wapate huruma. Hata watu wazima, huwa wanaeleza matatizo yao, kuonesha majeraha yao au kuelezea magonjwa waliyonayo ili kupata huruma ya wengine.
Kwa mfano, hivi unafikiri kwa nini watu wanakimbilia kwa wachungaji, manabii na wengine wanaofanana na hao? Ni kwa sababu ya kwenda kutafuta huruma, wakimweleza mtu matatizo yao na akiwaonea huruma na kuwafariji basi wanaridhika kiasi cha kusahau shida walizonazo.
Hatua ya kuchukua leo; kama unataka kuwashawishi watu wengine wakubaliane na wewe ,iwe kwenye mauzo hata mahusiano wakubaliane na wewe, wahurumie kwa kile wanachopitia.
Na wape muda wa kuwasikiliza, kuvaa viatu vyao na watajisikia vizuri.
Mwl.Deogratius Kessy
Mwalimu/Mwandishi/Mjasiriamali
Makamu Mkuu wa CHUO CHA MAUZO.
makamu@mauzo.tz, 📞0717101505//0767101504