Rafiki yangu mpendwa,

Tunaishi kwenye zama ambazo zinashangaza sana.

Ni zama ambazo maarifa mengi sana kuhusu mafanikio yanapatikana kwa urahisi kabisa. Vitabu vingi sana vimeandikwa kuhusu mafanikio, vikieleza kila siri ya mafanikio.

Hadithi nzuri za mafanikio ni nyingi sana. Wengi ambao walianzia chini kabisa, wakapambana mpaka kufanikiwa wamekuwa wanatoa hadithi zao, kupitia vitabu na mafunzo mbalimbali.

Kuna vipindi vya mahojiano ambapo wale waliofanikiwa hueleza hadithi zao, jinsi walivyoanzia chini kabisa na kupambana mpaka kufanikiwa.

Lakini pamoja na mafunzo na hadithi hizo nyingi sana za mafanikio, bado wanaofanikiwa ni wachache sana. Wengi wanabaki kuwa na maisha ya kawaida.

Na siyo kwamba wakipata maarifa hayo na hadithi hizo hawachukui hatua, wanafanya sana tu. Ila maarifa na hadithi zenyewe za mafanikio ndiyo zimekuwa zinawakwamisha watu wasifanikiwe.

Ndiyo, umenisoma vizuri kabisa hapo rafiki. Hayo maarifa na hadithi nyingi zinazopatikana kuhusu mafanikio ndiyo zimekuwa zinawakwamisha watu.

Unajua kwa nini?

Kwa sababu maarifa na hadithi hizo vimekuwa havielezi ule uhalisia wa safari ya mafanikio. Nyingi zinagusa juu juu tu, kwamba mtu alianzia chini kabisa, akaweka juhudi na kufanikiwa. Rafiki, hakuna mafanikio yaliyonyooka hivyo, na kurahisishwa huko kwa mafanikio ndiyo kumewafanya watu wengi kushindwa.

Sikia rafiki, mafanikio makubwa ni magumu mno. Ni safari yenye maumivu makubwa sana, yenye kuchosha, kukatisha tamaa na kuvunja mahusiano na watu wengi. Ni safari ya kujikana wewe mwenyewe na kuzaliwa mtu mpya kabisa.

SOMA; Ubatizo Wa Moto Unaohitajika Ili Ufanikiwe.

Kufikia mafanikio makubwa ni lazima upite kwenye moto mkali sana, ambao utaondoa kila aina ya uchafu unaokuzuia kufanikiwa ulio ndani yako.

Sasa basi, wale wanaofanikiwa huwa hawapo tayari kuweka wazi yale mateso na magumu waliyopitia. Wengi kwa nia njema tu ya kutokuwakatisha wengine tamaa.

Lakini kutokutaka kuwakatisha wengine tamaa, wanaishia kuwanyima kabisa mafanikio. Unajua kwa nini? Angalia hili.

Kuna mtu aliyefanikiwa, ambaye umemchagua kuwa wa mfano kwako. Umesoma vitabu kumhusu yeye na kusikiliza hadithi yake ambapo umekariri yote aliyopitia. Alianzia chini, akaweka juhudi na kufanikiwa.

Unapata msukumo wa wewe kuanzia chini ulipo na kuweka juhudi ili ufanikiwe. Unaweka juhudi kweli, lakini huoni matokeo. Unaona labda unahitaji uvumilivu, unajipa muda zaidi, bado hakuna kitu.

Unadhani kwenye hali kama hiyo ni nini kitafuata? Utaona kuna mahali unakosea, mbona yeye alifanikiwa na wewe hufanikiwi? Unaishia kukata tamaa na kwenda kwenye mambo mengine au kurudi kwenye mazoea yako.

Unakuwa umeshindwa kuendelea kwa sababu hukupata uhalisia wa ugumu wa safari ya mafanikio, hata kutoka kwa mtu wako wa mfano. Kama ungeyaona mateso makubwa ambayo hata yeye aliyapitia, ungeona jinsi mara kwa mara alikaribia kukata tamaa, ungeona bado upo kwenye njia sahihi.

Kuna upande mwingine wa mafanikio ambao huwa hauelezewi, ambao ni mtu kukutana na bahati. Ni kweli kwamba juhudi zinahitajika sana ili mtu kufanikiwa. Lakini pia kuna nafasi ya bahati. Kuna mtu anaweza kuweka juhudi kubwa sana, akakutana na bahati mbaya na akashindwa. Mwingine akaweka juhudi kubwa, akakutana na bahati nzuri na kufanikiwa.

Sisemi bahati uwe ndiyo mkakati wako wa kufanikiwa, weka juhudi sana, lakini pia jiweke kwenye mazingira ambayo ni rahisi kukutana na bahati mbalimbali zinazoweza kujitokeza.

Rafiki, sikuambii haya yote ili kukukatisha tamaa, bali nakusaidia uupate uhalisia na kuepuka kukata tamaa pale mambo yanapokuwa magumu kuliko ulivyokuwa unategemea.

Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA hapo chini nimekueleza kwa kina jinsi ambavyo mafanikio ni tofauti kabisa na kile kinachoonekana. Karibu ujifunze ili uwe na maandalizi sahihi na upambane mpaka ufanikiwe kwa uhakika.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.