3427; Usife Kirahisi…
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Kuna baadhi ya michezo na hadithi tulizokuwa tunapenda utotoni ambazo zina funzo kubwa sana kwenye maisha.
Chukua mfano wa kombolela, ambapo mnajificha na mmoja anakuwa na wajibu wa kuwatafuta kule mlikojificha.
Kwenye mchezo huo, kadiri unavyoonekana mapema, ndivyo unavyotoka kwenye mchezo na kuondoa kabisa nafasi ya ushindi.
Mafanikio kwenye mchezo huo ni kujificha sehemu ambayo ni vigumu kuonekana, lakini pia unaweza kuwakomboa wengine kwa kumzidi ujanja mtafutaji.
Hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye maisha, ushindi ni kudumu kwenye kile unachofanya kwa muda mrefu zaidi kuliko wengine wote.
Wajibu wako wa kwanza ni kuhakikisha hufi kirahisi.
Kuwa mgumu kuuawa na utajiweka kwenye nafasi ya mafanikio makubwa.
Na hapo kwenye kufa haimaanishi tu kifo cha maisha, bali kifo cha chochote unachofanya.
Mfano, jenga biashara ambayo ni ngumu kufa na hiyo itaweza kupata mafanikio makubwa.
Maana biashara ikishakufa, hakuna namna inaweza kupata mafanikio.
Hata kama unashindwa leo, hakikisha unaendelea kuwa hai kesho ili upate nafasi ya kupambana zaidi.
Pambana kwa kila namna ubaki kwenye mchezo, ukijua wa mwisho ndiyo mshindi.
Kama hutakufa haraka, kitu ambacho kinawezekana kama utajipanga vizuri, basi mafanikio yanakuwa uhakika kwako.
Wengi hawaelewi wala kuzingatia hilo, hivyo kulipa kipaumbele ni kujitofautisha na wengine wengi.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr Makirita Amani.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe