Pata picha timu ya mpira wa miguu unayoishabikia imeingia uwanjani kucheza na timu nyingine. Ni mchezo wa fainali ambapo mshindi anaondoka na zawadi kubwa sana. Unatamani sana timu yako ishinde mchezo huo.

Unatenga muda na kwenda uwanjani kuangalia mchezo huo. Umejiandaa kweli kweli kushangilia ushindi wa timu yako. Lakini unapoingia uwanjani, unapigwa na butwaa, kwani uwanja hauna magoli. Ndiyo, uwanja wa kucheza mchezo upo, ila magoli hayapo.

Ikitokea hali kama hiyo, utapatwa na wasiwasi mkubwa, kwa sababu utakuwa unajiuliza ushindi utapimwaje kama hakuna magoli. Ile shauku kubwa ya kushangilia ushindi inaisha, kwa sababu hakuna njia ya kupima ushindi. Timu hizo zinaweza kuingia uwanjani na kupiga chenga nyingi, lakini inapokuja kwenye kupima ushindi, inakosekana njia sahihi ya kufanya hivyo.

Hivyo ndivyo wauzaji wengi wanavyofanya kwenye kazi yao kuu ya mauzo na ndiyo maana wamekuwa hawapati ushindi mkubwa kama ambavyo walitarajia. Watu wengi huwa wanaingia kwenye biashara au mauzo kwa sababu wanataka kuingiza kipato kizuri. Lakini wanapofanya, wanajikuta wakiwa kwenye hali ngumu kwa sababu matarajio yao hayafikiwi.

Kushindwa kwenye biashara na mauzo kunaanzia mahali pamoja, kukosekana kwa njia ya kupima kama ushindi unapatikana au la. Na kupima siyo kwenye matokeo ya mwisho pekee, bali kwenye kila hatua ambazo zinachangia kwenye hayo matokeo ya mwisho.

Wengi waliopo kwenye biashara na mauzo huwa wanapima mauzo, ambayo ndiyo namba ya mwisho. Namba hiyo inapokuwa haipo vizuri wanajisikia vibaya na pale inapokuwa vizuri wanafurahia. Wanakuwa hawana namba nyingine wanazozipima na kufuatilia katika kuelekea kwenye namba hiyo ya mwisho. Na hilo ndilo linalokuwa kikwazo kwao kufanya mauzo makubwa.

Siyo Mchezo Wa Kubahatisha.

Kutokuwa na namba za kupima kuelekea kwenye namba ya mauzo kumefanya wengi kuendesha biashara na mauzo kama kamari. Wanachofanya ni kuwa na matumaini kwamba mauzo yatakwenda vizuri. Wanafanya nini ili kujihakikishia mauzo yanaenda vizuri wanakuwa hawana mkakati wa aina hiyo.

Mauzo siyo mchezo wa kubahatisha, mauzo ni kitu kinachoweza kupangiliwa na kufuatiliwa kwa umakini na matokeo ya uhakika kupatikana. Hiyo ina maana kwamba kwenye mauzo unaweza kuamua unataka uuze kiasi gani, kisha kupanga jinsi ya kufikia kiasi hicho cha mauzo ulichopanga. Unachohitaji kufanya ni kuzijua namba sahihi kupima na kufuatilia kwenye mauzo ili kufikia lengo ulilojiwekea kwa uhakika.

Mauzo ni mchezo wa uhakika kama ilivyo michezo mingine kwenye maisha kwa sababu una namba za uhakika za kupima. Pale mauzo yanapokuwa madogo hubaki na matumaini, badala yake unaangalia kwenye namba zako ili kujua ni eneo gani ambalo halijafanyiwa kazi vizuri. Kwa sababu mauzo ni namba ya mwisho, kuna namba nyingine ambazo zinakuwa zinaisababisha. Kwa kujua namba hizo na kuzifanyia kazi, utaweza kuboresha namba hiyo ya mwisho.

Kisichopimwa Hakikui.

Kwenye kila eneo la maisha, kitu chochote ambacho hakiwezi kupimwa, huwa hakiwezi kukua. Unaweza kuangalia mfano wa watoto wadogo wanaozaliwa, kila mwezi huwa wanapelekwa kliniki kwa ajili ya kupimwa maendeleo yao. Kliniki wanapimwa uzito na urefu namba ambazo zinawekwa kwenye fomu yao maalumu inayoonyesha maendeleo yao. Fomu ya kliniki ya watoto ina namba zinazoashiria maendeleo ya mtoto. Namba nyekundu ni maendeleo mabaya, kijivu maendeleo ya wastani na kijani maendeleo mazuri. Kwa kuangalia namba na mahali zinapoangukia kwenye fomu, mtu anaweza kuona maendeleo ya mtoto.

Hivyo pia ndivyo biashara na mauzo yanavyopaswa kupimwa. Kunapaswa kuwa na namba zinazofuatiliwa kila mara na chati ya kujaza namba hizo ili mtu anapoangalia aweze kuona maendeleo kwa haraka. Kama kuna tatizo lolote kwenye biashara au mauzo, litaonekana kwa haraka kwa kuziangalia namba ambazo zinapimwa.

Kama hakuna namba zinazopimwa kwenye mauzo, hayawezi kukuzwa. Kwani inabaki kuwa kitu cha matumaini na hakuna mambo ya uhakika ya kufanyia kazi. Tukirudi kwenye mfano wa watoto na kliniki hapo juu, kama mtoto atapimwa na kuonekana uzito wake ni mdogo kuliko inavyopaswa kuwa, mzazi anashauriwa namna bora ya kumlisha mtoto ili aweze kuwa na uzito mzuri. Ushauri huo unapofanyiwa kazi, uzito unaongezeka kwa uhakika.

Ndivyo pia inavyoweza kuwa kwenye mauzo, pale mauzo yanapokuwa siyo mazuri, kama namba zinapimwa itaonekana dhahiri ni namba zipi ambazo hazifanyiwi kazi vizuri. Pale namba hizo zinapofanyiwa kazi vizuri, mauzo yanaongezeka kwa uhakika.

Ni muhimu sana kuyapima mauzo kwa namba ili kuweza kuchukua hatua sahihi za kuwezesha mauzo kukua.

SOMA; Kusaka wateja kwa njia ya utembeleaji na kukutana ana kwa ana.

Namba 10 Za Kupima Kwenye Mauzo.

Kuna namba nyingi za kuweza kupimwa kwenye mauzo ili kuweza kuyakuza zaidi. Lakini kwenye programu yetu ya CHUO CHA MAUZO kuna namba 10 ambazo zinafuatiliwa kwa uhakika. Namba hizo 10 zina nguvu kubwa ya kukuza mauzo pale zinapofanyiwa kazi kwa uhakika.

Namba 10 za kufuatilia na kupima kwenye mauzo ili kuyakuza ni kama ifuatavyo;

1. SIMU ZILIZOPIGWA.

Simu ndiyo njia kuu ya kuwasiliana na wateja. Kupiga simu kwa wateja ni njia muhimu ya kuweza kufanya mauzo makubwa zaidi.

2. WATEJA WALIOTEMBELEWA.

Kukutana na wateja ana kwa ana kuna nguvu kubwa ya kuwashawishi kuliko tu kuwasiliana nao. Kuwatembelea na kukutana na wateja ni namba muhimu inayopimwa kwenye mauzo.

3. WATEJA WAPYA TARAJIWA WALIOTENGENEZWA.

Kutengeneza wateja wapya kila wakati ni hitaji muhimu kwenye kukuza mauzo. Kila muuzaji anapaswa kuwa anatengeneza wateja wapya tarajiwa, hivyo namba hiyo ni muhimu kuipima.

4. WATEJA TARAJIWA WALIOGEUZA KUWA WATEJA KAMILI.

Wateja wanakuwa kamili pale wanapokubali kununua. Hivyo kazi kubwa ya mtu wa mauzo ni kuwageuza wateja kutoka kuwa tarajiwa kwenda kuwa kamili. Wateja waliogeuzwa ni namba muhimu ya kufuatilia kwenye kukuza mauzo.

5. IDADI YA WATEJA TARAJIWA WALIOFUATILIWA.

Siyo wateja wote tarajiwa watageuzwa mara moja kuwa kamili, kuna ambao watachukua muda kufuatiliwa. Hivyo mtu wa mauzo anapaswa kuwa na ufuatiliaji endelevu wa wateja wote tarajiwa anaokuwa nao. Hii ni namba muhimu kufuatilia ili kuwageuza wateja tarajiwa wengi zaidi.

6. IDADI YA WATEJA KAMILI WALIOFUATILIWA.

Kwa kuwa wateja wameshanunua haimaanishi kwamba wataendelea kununua, kwa sababu wanawindwa na wauzaji wengine, hivyo ni rahisi kupotea. Kuzuia hilo ufuatiliaji endelevu unapaswa kufanyika kwa wateja wote kamili. Hii ni namba muhimu kufuatilia ili kuwabakisha wateja kwenye biashara kwa muda mrefu.

7. IDADI YA WATEJA WALIONUNUA.

Hii ni idadi ya wateja ambao wamefanya manunuzi. Ni namba muhimu kupima ili kuona kama wateja wanaongezeka au kupungua. Pia itakupa wastani wa manunuzi kwa kila mteja kitu ambacho ni muhimu kujua.

8. MAUZO KAMILI YALIYOFANYIKA.

Hiki ni kiasi cha mauzo kwa fedha ambacho kinakuwa kimefanyika. Hii ndiyo namba kuu kwenye mauzo, ambayo wengi huwa wanaiangalia. Namba hii inakuwa vizuri pale namba nyingine zinapofanyiwa kazi vizuri.

9. MAUZO YA ZIADA YALIYOFANYIKA.

Wateja wanapofanya manunuzi, huwa wanakuwa na mpango wao kwenye manunuzi wanayofanya. Kupitia manunuzi hayo, huwa kunajitokeza fursa ya kuwauzia vitu vya ziada. Namba hii inapima uwezo wa muuzaji kuwashawishi wateja kufanya manunuzi ya ziada, kitu kinachoongeza zaidi mauzo.

10. WATEJA WA RUFAA WALIOPATIKANA.

Wateja wa rufaa ni wateja wanaopatikana kupitia wateja kamili waliopo kwenye biashara. Hao huwa ni wateja rahisi kuwageuza kwa sababu wameshaambiwa na watu wao wa karibu. Ni namba muhimu kupima ili kuweza kupata wateja wengi wa rufaa ambao watageuzwa kwa urahisi kuwa wateja kamili.

Kwenye sura 10 za kitabu hiki unakwenda kujifunza namba hizo 10 kwa kina na kujua umuhimu wa namba husika, jinsi ya kupima namba hiyo na jinsi ya kuifanya namba hiyo kwa ukubwa zaidi ili kuweza kukuza mauzo. Jifunze kwa kina namba hizo 10 na uzifanyie kazi ili uweze kuwa muuzaji bora na kufanya mauzo makubwa zaidi.

Karibu Upate Kitabu Cha MAUZO NI MCHEZO WA NAMBA.

Kama unataka kukuza mauzo ya biashara yako kwa uhakika, basi hakikisha unapata kitabu hiki cha MAUZO NI MCHEZO WA NAMBA. Kitabu hiki kitakwenda kuleta mapinduzi makubwa kwenye biashara yako kama utakifanyia kazi. Wasiliana sasa na namba 0678 977 007 uweze kupata nakala yako ya kitabu.

Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA hapo chini nimegusia kwa kifupi namba zote 10 za mauzo. Uangalie, ujifunze na kwenda kuchukua hatua ili kukuza mauzo yako.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.