Habari njema wauzaji bora kuwahi kutokea.

Karibuni kwenye mfululizo wa masomo yetu ya programu ya CHUO CHA MAUZO, yenye lengo la kutujenga kuwa wauzaji bora na kufanya mauzo makubwa.

Mkakati wetu mkuu kwenye CHUO CHA MAUZO ni kutengeneza wateja tarajiwa na kuwafuatilia wateja mara zote. Kwa kufanya hayo mawili, kufanya mauzo makubwa inakuwa ni matokeo ya uhakika.

Kila biashara inapaswa kutumia fursa mbalimbali zinazopatikana kuweka vizuri rasilimali zinazoiwezesha kufikia wateja wengi zaidi na kufanya mauzo makubwa.

Na kila muuzaji ndani ya biashara anapaswa kutumia rasilimali zote zilizopo kwenye biashara kufikia wateja wengi na kufanya mauzo makubwa.

Moja ya rasilimali inayoweza kutumika vizuri kwenye biashara ni mavazi au sare za watu wote waliopo kwenye biashara.

Kwa kuwa watu lazima wavae mavazi, ni fursa kwa biashara kutumia nafasi hiyo kujenga imani na kujitangaza zaidi.

Kila biashara inapaswa kuwa na sare maalumu ambazo watu wote waliopo kwenye biashara wanazivaa wakati wote wa kazi. Hilo linakuwa na manufaa ambayo tutayaona kwenye somo hili.

MAANDALIZI YA SARE BORA.

Kwa kuwa sare ndiyo kitu cha kwanza kinachoonekana, zinapaswa kuandaliwa vizuri ili ziweze kuacha alama kwa wote wanaoziona. Katika kuandaa sare bora, yafuatayo yanapaswa kuzingatiwa.

1. Sare zinapaswa kuwa na alama za biashara, kuanzia nembo (logo) na rangi za biashara. Hiyo inafanya mtu aweze kuhusianisha sare na biashara.

2. Ubora wa vitambaa vinavyotumika uwe mzuri ili ziwe na mwonekano mzuri muda wote na kutokuharibika mapema.

3. Sare ziweze kuitambulisha biashara hata kama ni kwa mbali na siyo mpaka mtu asogee karibu ndiyo aweza kuijua biashara.

4. Sare ziwe za aina tofauti, mfano mashati, tisheti, kofia n.k.

5. Iwe ni sera ya biashara kwamba kila aliyepo kwenye biashara anapaswa kuvaa sare muda wote anaokuwa kwenye maeneo ya biashara.

Hayo yanapaswa kuzingatiwa kwenye maandalizi ya sare za biashara ili ziweze kuleta tija.

SOMA; Tumia Alama (Logo) Na Kadi Za Biashara Kufikia Wateja Wengi Zaidi.

FAIDA ZA SARE.

Matumizi ya sare kwenye biashara yana faida nyingi, baadhi ya faida hizo ni kama ifuatavyo;

1. Wafanyakazi kwenye biashara kuaminika na watu ambao wanawajua kwa mara ya kwanza. Pale mtu anapokuwa na sare za biashara fulani, anaaminika kama mhusika wa biashara hiyo.

2. Kuleta unadhifu kwa watu waliopo kwenye biashara, kwa sababu mavazi ya wote wanafanana.

3. Kuleta hali ya usawa na ushirikiano baina ya wafanyakazi, kwa sababu mavazi ya wote yanakuwa sawa hivyo hakuna matabaka.

4. Kuongeza uzalishaji na ufanisi kwa sababu watu hawatumii muda mwingi kufikiria nguo za kuvaa ili waonekane vizuri. Kwa kuwa wote ni sare, basi mtu anajua cha kuvaa bila hata ya kujiuliza mara nyingi.

5. Kutumika kama zawadi kwa wateja wanaofanya vizuri kitu kinachowachochea kufanya vizuri ili wapate zawadi.

MATUMIZI YA SARE KUKUZA MAUZO.

Sare zina matumizi makubwa kwenye kukuza mauzo ya biashara, kupitia kuwafikia wateja wengi, kuaminika na kuwashawishi kununua. Matumizi ya sare kwenye kukuza mauzo ni kama ifuatavyo;

1. Kuvaliwa wakati wote ambao watu wapo kwenye biashara ili wateja kuweza kuwatambua na kuwaamini.

2. Kuvaliwa nyakati ambazo watu wanatoka nje ya biashara ili kuitangaza biashara kupitia mwonekano wa sare.

3. Kutoa zawadi ya sare kwa wateja wanaofanya vizuri ili kuwasukuma wafanye vizuri lakini pia wanapovaa wanawafikia watu wengi zaidi ambao nao wanaijua biashara.

4. Kuvaliwa wakati wa usakaji wa kuwatembelea wateja kule walipo ili kuaminika ni watu kutoka kwenye biashara husika na siyo matapeli.

5. Kuvaliwa wakati wa matukio ya kijamii au kimichezo ambapo watu wanakutana na watu wengi kwa wakati mmoja na hivyo kutambulika kwa haraka.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kwa nguvu hii ya sare kwenye timu na mauzo, kila biashara inapaswa kuwa na sare na wafanyakazi wote kwenye biashara wanapaswa kuvalia sare kulingana na utaratibu uliowekwa kwenye biashara.

Hilo litaiwezesha biashara kuwafikia wateja wengi zaidi na kuweza kufanya mauzo makubwa zaidi.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.