Habari njema muuzaji bora kabisa kuwahi kutokea,

Karibu sana kwenye mwendelezo wa makala zetu za ukamilishaji ambazo ni mwendelezo wa makala kutoka kwenye programu yetu ya  CHUO CHA MAUZO.

Hongera sana kwa kuendelea kujifunza na kuchukua hatua kwa haya unayoendelea kujifunza hapa.

Leo ni jumatano ya ukamilishaji tukiongozwa na kauli mbiu yetu inayosema ABC ALWAYS BE CLOSING-MARA ZOTE KUWA UNAKAMILISHA WATEJA.

Kama kauli mbiu inavyosema, mara zote unapaswa kukamilisha wateja na wewe pia unapaswa kukamilisha wateja. Na kukamilisha ndiyo wajibu wako namba moja kwenye biashara yako.
Wajibu wako namba moja ni kuuza na unapokuwa umemuuzia mteja maana yake umemkamilisha.
Hivyo basi, kila wakati wageuze wateja tarajiwa uliokuwa nao na waweze kununua na kuwa wateja kamili.

Ukamilishaji ndiyo kitu muhimu sana kwenye mauzo kwa sababu ndiyo kitu pekee kinacholeta fedha kwenye biashara kupitia kile unachouza iwe ni bidhaa au huduma.

Kwenye somo letu lililopita tulijifunza mbinu mbili za uhakika za ukamilishaji wa mauzo nayo ni mbinu namba 39 na 40.
Kwenye mbinu namba 39 tulijifunza ukamilishaji wa kufikiria zaidi namba 5
Na kwenye ukamilishaji wa namba 40 tulijifunza ukamilishaji wa kurudia uwasilishaji au maonyesho.

SOMA; Mbinu Mbili Za Uhakika Za Ukamilishaji Wa Mauzo 39-40

Na kwenye ukamilishaji wa kufikiria zaidi namba 5 mbinu namba 39 tulijifunza kwamba mteja akikuambia nahitaji kufikiria zaidi, mwambie naelewa, na mimi kama mteja, nimewaho kusema hivyo, wakati ambapo a)sikutaka kumkabili muuzaji b) sikutaka kumwangusha, c) kulikuwa na mambo sijayaelwa. Ipi sababu yako?

Leo kwenye jumatano ya ukamilishaji tukiongozwa na kauli mbiu yetu inayosema ABC ALWAYS BE CLOSING-MARA ZOTE KUWA UNAKAMILISHA WATEJA, tunakwenda kujifunza mbinu nyingine mbili za uhakika za ukamilishaji wa mauzo nazo ni mbinu namba 41 na 42

Zifuatazo ni mbinu mbili za uhakika za ukamilishaji wa mauzo ambazo tunakwenda kujifunza hapa;

41.Ukamilishaji wa kuomba msamaha.

Unatumia ukamilishaji huu pale unapokuwa umeshindwa kukamilisha mauzo kwa mara ya kwanza.

Unaomba msamaha kisha kutumia nafasi nyingine kukamilisha.

Kila mtu huwa anayajutia maamuzi yake, kwa kuomba msamaha kisha kuanza tena mchakato wa ukamilishaji mauzo, unakuwa na ushawishi zaidi.

Unamwambia mteja hivi;
“Naomba unisamehe kwa kushindwa kuelewana na wewe. Naomba kuuliza –
je ni kitu gani ambacho nimefanya?
Je ni kitu ambacho nimeshindwa kufanya? Niruhusu nikuandalie bidhaa yako kuliko uende nyumbani hujanunua au ukaanze tena mchakato huu mahali pengine.”

Sina uhakika kama itakufaa lakini tumia msamaha kurudisha mahusiano yaliyopotea na kukamilisha mauzo.

  1. Ukamilishaji wa kukataa kuamini.

Pale mteja anapokupa pingamizi la kutaka kukutoroka na kutonunua, hupaswi kukubaliana naye kirahisi, kwa pingamizi lolote analokupa kama ni bei au lolote lile.

Pale mteja anapokupa pingamizi la kukataa kununua bila sababu ya msingi, mwambie;
“Sitaki kuamini kwamba hutakwenda kukamilisha hili. Ni bidhaa/huduma sahihi kwako, bei ni bora na najua unaitaka. Tukamilishe hili, weka sahih yako hapa au kinachofuata baada ya hapa ni wewe kukamilisha malipo ili uende ukafurahie bidhaa au huduma yako.”

Unapaswa kutumia ukamilishaji huu ukiwa na shauku na hamasa kubwa, ukiwa na imani isiyoyumbishwa kwamba ndicho kitu mtu anataka na sahihi kwake.

Watu huwa hawawezi kufanya maamuzi peke yao, wanahitaji msaada.

Wajibu wako kama muuzaji ni kumsaidia kufanya maamuzi sahihi kupitia kile unachouza iwe ni bidhaa au huduma. Wewe ndiyo unaijua biashara yako kwa kina hivyo msaidie mtu afanye maamuzi sahihi kwani asipofanya maamuzi sahihi na wewe upo, baadaye akija kupata changamoto atakuja kukulaumu wewe kwa sababu wewe ndiyo unaijua biashara yako na kwa nini ulimwacha mpaka akafanya maamuzi ambayo siyo sahihi?

Mchukulie mteja wako kama vile mtoto wako anayeumwa, hata kama hataki dawa huwezi kumuacha afe, utapambana kwa kila namna kuhakikisha anakunywa dawa hata kama hataki.

Ni wajibu wako wa kimaadili kuuza na kumsaidia mteja kufanya maamuzi kadiri ya kile unachouza iwe ni bidhaa au huduma.

Kutoka kwa muuzaji mwenzako, rafiki anayekupenda na kukujali,

Mwl.Deogratius Kessy