Habari njema muuzaji bora  kuwahi kutokea,

Hongera na karibu sana kwenye mwendelezo wa makala zetu za ushawishi kutoka kwenye programu yetu ya CHUO CHA MAUZO.

Kwenye jumamosi ya ushawishi tunaongozwa na kauli mbiu yetu inayosema HUPATI UNACHOSTAHILI BALI UNACHOSHAWISHI.

Wiki iliyopita tulifanikiwa kujifunza jinsi ya kuwafanya watu wakubaliane na mawazo yako kanuni ya TISA ambayo ni wahurumie wengine kwa mawazo na matakwa yao.

Na kwenye kanuni ya nane tulifanikiwa kuondoka na kitu kimoja ambacho ni wewe kama muuzaji bora kuwahi kutokea, unatakiwa kujua kwamba sehemu kubwa ya watu unaokutana nao, wana kiu ya huruma, wape huruma na watakupenda na kukukubali na mwisho kukubaliana na wewe kwenye kile unachomshawishi.

Na hapa tuliondoka na kitu kimoja kwamba kila binadamu anataka zaidi huruma kwa mfano, watoto huwa wanaonesha vidonda vyao na hata mara nyingine kujiumiza ili wapate huruma. Hata watu wazima, huwa wanaeleza matatizo yao, kuonesha majeraha yao au kuelezea magonjwa waliyonayo ili kupata huruma ya wengine.
Kama unataka kuwashawishi watu wengine wakubaliane na wewe, iwe ni kwenye mauzo au hata mahusiano wakubaliane na wewe, wahurumie kwa kile wanachopitia.
Wape muda wa kuwasikiliza, vaa viatu vyao na watajisikia vizuri sana.

SOMA; Jinsi Ya Kuwafanya Watu Wakubaliane Na Mawazo Yako Kanuni Ya Tisa

Habari njema ni kwamba leo kwenye jumamosi ya ushawishi, tunakwenda kujifunza jinsi ya kuwafanya watu wakubaliane na mawazo yako kanuni ya KUMI ambayo ni TUMIA NIA NJEMA YA WENGINE

Mpendwa muuzaji bora kuwahi kutokea,

Mara nyingi, kila mtu unayekutana naye huwa anajichukulia kuwa wa juu na mwema kuliko wengine, kwa vipimo vyao wenyewe.

Mwandishi Dale Carnegie anamnukuu J.P. Morgan ambaye alisema, kila mtu huwa ana sababu mbili za kufanya kitu, sababu inayoonekana nzuri kwa wengine na sababu halisi.
Hiyo sababu halisi ndiyo nia ya ndani kabisa inayomsukuma mtu afanye anachofanya, japo huwa haiweki wazi.

Ukiona mtu anajisukuma kufanya kitu bila kuambiwa, jua hiyo ndiyo nia ya njema ya mtu. Na mtu akiwa ni mtu wa sababu kila siku, huyo ni mtu wa sababu nzuri.
Anatafuta sababu nzuri ambayo akikuambia itaweza kuonekana kama nia njema kumbe siyo ili tu kuonekana kama mtu mwenye nia njema. Na ukitaka kujua mtu mwenye nia njema ya kufanya kitu na yule asiyekuwa na nia njema wape tu muda. Ni kama vile Warren Buffett anavyosema mawimbi yakitulia, ndiyo tutajua nani anayeoga uchi.
Hii ikiwa na maana kwamba, wape watu muda na utajua nia zao za kweli za kutaka kufanya kitu kadiri ya muda.

Kama unataka kuwashawishi watu wakubaliane na wewe, kama unataka watu wabadilike, lenga kwenye sababu halisi kwao kufanya kitu, ijue nia njema kwao kufanya kile wanachofanya.

Unapotaka kuwashawishi wateja wako, jua nia zao njema kufanya kile wanachofanya. Na kwenye biashara ni rahisi, ukitaka kujua nia njema ya mtu kufanya kile anachofanya, muulize tu, uliwezaje kuanza biashara yako au kile anachofanya iwe anauza bidhaa au huduma. Kupitia swali hilo litakusaidia kupata nia njema kabisa ya mtu na kisha kutumia nia njema yao na kumshawishi na kumuuzia kile unachouza iwe ni bidhaa au huduma.

Uzuri ni kwamba, kuna vitu ambavyo kila mtu kwenye jamii, huwa anakubaliana navyo. Mfano, kupinga mauaji, kujali watoto na kusaidia wengine.  Hivyo basi, pale unapotaka kuwashawishi watu kufanya kitu, tumia sababu hizo zinazoibua nia njema kwa wengine.

Mpendwa muuzaji bora kuwahi kutokea, unafikiri kwa nini picha nyingi za kuomba misaada huwa zinatumia watoto au watu walio kwenye majanga. Ni kwa sababu, unapoona watu wa aina hiyo, inagusa ndani yako na unakuwa tayari kuchukua hatua.

Dale anatuambia Lord Northcliffe wakati wa uhai wake, kulikuwa na gazeti ambalo lilikuwa linatumia picha yake ya zamani ambayo hakuipenda. Alijua akimwandikia mhariri kumtaka asitumie picha hiyo ndiyo atakuwa amechochea moto zaidi. Hivyo alichofanya, alimwandikia barua, mhariri akisema, tafadhali msichapishe tena picha hiyo, kwa sababu mama yangu huwa haipendi”

SOMA; Jinsi Neno Kwa Sababu Linavyoweza Kukuongezea Ushawishi Na Mauzo

Tangu hapo picha hiyo haikuchapwa tena, kwa sababu watu wanamheshimu na kumpenda mama, ni nia njema iliyoko kwa kila mtu.

Watu wamekuwa wanatumia watoto, wagonjwa, walemavu na wengine wenye mahitaji kama njia ya kuwashawishi wengine kukubaliana nao.
Na wengi hukubali kwa sababu ya nia njema iliyo ndani ya kila mtu ya kuwasaidia wenye uhitaji.

Mwisho, tumia kila nia njema iliyo ndani ya mtu kuweza kuwashawishi watu na kukubaliana nao.
Jua nia njema ya kila mteja wako,iliyoko ndani yake na itumie hiyo kukubaliana naye.
Kila mteja ana nia njema kabisa iliyo ndani yake, hivyo ijue kwa kuwa mdadisi kwa kuuliza maswali.

Rafiki na mwalimu wako anayekupenda na kukujali katika mauzo,
Mwl.Deogratius Kessy

Mwalimu/Mwandishi/Mjasiriamali
Makamu Mkuu wa CHUO CHA MAUZO.
makamu@mauzo.tz, 📞0717101505//0767101504