Rafiki yangu mpendwa,

Kuzaliwa kwenye familia tajiri au inayojiweza kifedha huwa ni bahati nzuri na bahati mbaya kwa wakati mmoja.

Watu wengi wamekuwa hawaelewi hili na hivyo kujikuta wakishindwa kujenga maisha sahihi kwao.

Upande wa bahati nzuri ya kuzaliwa kwenye familia tajiri, kila mtu anaweza kujua hili kwa urahisi.

Mtu anapata mahitaji yote ya msingi kwenye maisha, hasa upande wa elimu. Kwa familia kujiweza, mtu anapata elimu nzuri na hiyo inakuwa msingi mzuri kwenye maisha.

Lakini pia kwenye kuanza maisha, anayezaliwa familia inayojiweza anakuwa na mahali pazuri pa kuanzia kuliko wa familia masikini. Kama ni kazi anaweza kupata fursa nzuri zaidi za kazi. Na kwa upande wa biashara, anaweza kupata mtaji wa kuanza biashara kwa urahisi zaidi.

Kupata elimu nzuri na kuwa na mahali pa kuanzia kwenye kujijenga binafsi ni faida kubwa mbili za kuzaliwa kwenye familia inayojiweza.

Tukienda upande wa bahati mbaya au hasara ya kuzaliwa kwenye familia inayojiweza, tunaona mambo ambayo yanawakwamisha wengi wanaotokea familia hizo.

Kitu cha kwanza kabisa ni kutokujua shida au kukosa na hivyo kuwa dhaifu kukabiliana na changamoto za maisha. Kwa sababu mtu amekua akipata kila anachotaka, anakuwa hajui uhalisia wa dunia kwamba huwa kuna kukosa. Ni mpaka mtu anapokuwa mtu mzima ndiyo anakuja kukutana na uhalisia wa dunia ambao unamuumiza sana. Kwa sababu dunia haimpi kila anachotaka kwa namna anavyotaka, inakuwa rahisi kwao kukata tamaa.

SOMA; Ngazi Ya Juu Ya Usimamizi Wa Kujenga Utajiri; Staafu Na Uhuru Wa Kifedha.

Kitu cha pili ni kutegemea misaada ya wazazi mpaka kwenye umri wa utu uzima. Huwa ni hali ya kawaida kukuta mtu aliyezaliwa familia tajiri akiendelea kupewa fedha za matumizi na wazazi wake hata baada ya kuwa anajitegemea na ana familia. Wengi hupewa nyumba za kuishi, magari ya kutembelea na hata kulipiwa ada za shule kwa watoto wao. Hilo linawafanya wabweteke na kuona maisha ni rahisi. Ni mpaka pale wazazi wanapokuwa hawapo tena ndiyo wanakutana na uhalisia wa maisha ambao unawaumiza sana.

Kitu cha tatu ni kukosa ile njaa na hasira ya kufanikiwa. Wazazi ambao wameweza kujenga utajiri, mara nyingi wanakuwa walianzia kwenye maisha ya umasikini. Hayo yaliwapa njaa na hasira ya kujisukuma mpaka kufanikiwa. Lakini wanapopata utajiri, huwa hawataki watoto wao wapitie yale ambayo amepitia wao na hivyo kuwanyima njaa na hasira ya mafanikio. Watoto hao huishia kupata mafanikio ambayo ni madogo kuliko aliyoweza kupata wazazi wao.

Rafiki, swali lako litakuwa ni mtu anawezaje kuondokana na bahati mbaya hizo za kuzaliwa familia inayojiweza? Hilo ni swali ambalo nimelijibu kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA hapo chini. Fungua kipindi hicho ujifunze na kwenda kuchukua hatua ili uweze kujenga utajiri mkubwa kuliko waliojenga wazazi wako.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.