Rafiki yangu mpendwa,

Kwenye maisha, kile kinachoitwa ni mafanikio ya haraka, huwa ni kazi iliyofanyika kwa muda mrefu bila ya kuonekana.

Kwa bahati mbaya sana, wakati watu wanaanzia chini kabisa na kupambana kufanikiwa huwa hawaonekani. Lakini wakishafanikiwa, wanaanza kusikika na kujulikana na wengi na mafanikio yao kuonekana ni ya haraka.

Hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye kujenga utajiri mkubwa kwenye maisha. Mtu anapokuwa masikini, huwa hazingatiwi na wengine, anapuuzwa kwa sababu hana chochote cha tofauti. Mtu huyo anapopambana na kupata utajiri, watu wanaanza kumjua na kutafuta kujinufaisha kupitia yeye.

Kila mtu unayemwona amejenga utajiri mkubwa, jua kwa hakika ameweka kazi kubwa sana na kwa muda mrefu mpaka kufika hapo. Wapo wengi waliotaka sana kupata utajiri, lakini hawakuwa tayari kuweka kazi na hivyo kushindwa kuupata.

Mwandishi Chris Hogan kwenye kitabu chake kinachoitwa EVERYDAY MILLIONAIRES ameonyesha jinsi watu wa kawaida kabisa walivyoweza kujenga utajiri mkubwa kwenye maisha yao na jinsi hata wewe unaweza kufanya hivyo.

Kitabu hicho ni matokeo ya utafiti uliofanywa kwa mamilionea zaidi ya elfu 10 na kuweza kupata taarifa nyingi sana kuwahusu. Utafiti huo uligusa kila eneo la matajiri, kuanzia mitazamo, fikra, shughuli wanazofanya, mahusiano, familia n.k.

Kupitia matokeo ya utafiti huo, Hogan aliweza ameweza kuainisha SIFA KUU SITA ambazo matajiri wanazo ila masikini wamekuwa hawana. Kupitia masomo haya utajifunza sifa hizo na hatua za kuchukua ili na wewe uweze kujenga utajiri mkubwa kwenye maisha yako.

SURA YA 9; WEKA KAZI (FANYA KILA KINACHOHITAJIKA)

Matajiri huwa wanatofautiana kwenye vitu vingi, kuanzia elimu, umri, aina ya kazi au biashara na mengine. Kote huko kila mtu anakuwa na njia yake inayotofautiana na ya mwingine. Lakini inapokuja kwenye KAZI, wote wanafanana. Haijalishi wanafanya nini, huwa wanaweka juhudi kubwa sana kwenye kazi kuliko watu wengine.

Matajiri huwa wanaanza kufanya kazi zao mapema, wanafanya muda wote na wanachelewa kumaliza kufanya kazi zao. Kipaumbele chao kikubwa kinakuwa kwenye kufanya kazi na hilo huwa linawalipa sana.

Kupitia utafiti uliofanywa na mwandishi, waliweza kuona matajiri wengi wametokea kwenye familia ambazo ni za wakulima. Na kupitia maisha ya kilimo, waliweza kujengewa nidhamu nzuri ya kazi. Kazi ya kilimo inahitaji mtu kuweka kazi sana na kwa muda mrefu. Ndiyo maana wale waliokulia kwenye familia zinazofanya kilimo, huwa wanajengewa uchapakazi tangu utotoni.

Matajiri wanakuwa tayari kuweka kazi kwa juhudi na muda mrefu kwa sababu huwa wanakuwa wanapenda kile wanachofanya na mchango wanaokuwa nao kwa wengine.

Kufanya kazi kwa juhudi siyo tu inaweza kukujengea utajiri, lakini pia ina faida nyingine kama ifuatavyo;

1. Inakujengea uvumilivu kwa sababu vitu vizuri vinachukua muda.

2. Inakuwezesha kupiga hatua, hata kama ni ndogo ndogo.

3. Inakupa hali ya kukamilisha, kwa kujisikia vizuri pale unapokamilisha jukumu.

4. Inakujengea hali ya kujiamini, kwa kujua unaweza kufanya.

5. Inaboresha kile unachofanya, kwa kuwa bora zaidi kwenye kukifanya.

6. Inakujengea unyenyekevu, kwa kuheshimu matokeo unayokuwa umeyapata kwa kuweka kazi.

Hatua za kuchukua;

Ifanye kazi kuwa rafiki yako muhimu kwenye maisha. Weka kipaumbele kwenye kazi na fanya kila kinachopaswa kufanyika ili kuleta matokeo yanayohitajika.

Usiishie tu kusema umefanya kila kinachowezekana, nenda zaidi ya hapo, fanya hata yasiyowezekana ili kupata matokeo unayoyataka.

SOMA; Fanya Kwa Kusudi Na Ongozwa Na Malengo Ili Kujenga Utajiri Mkubwa.

SURA YA 10; KUWA NA MSIMAMO (KOMAA NA KITU MPAKA KIKUPE MATOKEO).

Ubobezi na ubora ni matokeo ya kufanya kitu kwa muda mrefu bila kuacha. Kadiri mtu unavyorudia rudia kufanya, ndivyo unavyokuwa vizuri kwenye kufanya kitu na kuvutia matokeo mazuri zaidi.

Msimamo ndiyo sifa kuu inayoleta sifa nyingine pamoja. Msimamo ukikosekana, sifa nyingine haziwezi kuleta matokeo mazuri.

Kwa mfano hata mtu awe tayari kuwekeka juhudi ya kazi kiasi gani, kama hatakuwa na msimamo, atakuwa anaanza na kuacha vitu kila wakati. Atapoteza nguvu na muda mwingi na hatapata matokeo anayotarajia.

Kwenye safari ya kujenga utajiri, matokeo huwa yanachukua muda mrefu kupatikana. Kama mtu hana msimamo, hataweza kuwa na uvumilivu wa kutosha kusubiri matokeo.

Matajiri huwa wana msimamo kwenye mambo yote, siyo tu kwenye kujenga utajiri, bali mpaka kwenye mahusiano yao.

Msimamo unataka UVUMILIVU na MAPENZI. Unapopenda kitu na ukawa na uvumilivu, utaenda nacho kwa muda mrefu hata kama matokeo hayaonekani kwa haraka.

Faida kubwa ya uwekezaji huwa inatokana na riba mkusanyiko, ambayo ukubwa wake unategemea muda ambao imekua inajikusanya. Hivyo mafanikio ya uwekezaji ni kuwekeza kwa msimamo bila kuingilia uwekezaji huo.

Mahali pengine panapohitaji msimamo ni pale mambo yanapokuwa yanaenda vizuri. Wengi mambo yakienda vizuri, anaanza kutafuta njia za kubadili. Matokeo yake wanaharibu kabisa kile kilichokuwa kinaenda vizuri.

Pale mambo yanapokuwa yanaenda vizuri, endelea nayo kwa msimamo ili uendelee kuvuna matokeo mazuri zaidi. Usibweteke na kuona huhitaji tena kuweka juhudi, kuweka juhudi ni kitu endelevu.

Hatua za kuchukua;

Ukishaweka mchakato wako wa kujenga utajiri, kaa kwenye mchakato huo kwa msimamo bila kuacha. Utashawishika sana kuachana na mchakato huo, hasa pale matokeo yanapokuwa yanachelewa, lakini usikubali hilo. Endelea na mchakato wako na matokeo mazuri yatakuja.

Pale unapopata matokeo mazuri kutokana na mchakato ulioufuata, usijisahau na kurudi nyuma. Badala yake endelea na mchakato wako kama ulivyoweka na umekuwa unaenda. Utaendelea kuboresha zaidi lakini siyo kuacha mchakato kwa kuona umeshamaliza kila kitu.

Hapa tumejifunza sifa mbili kati ya sita walizonazo matajiri na zinawatofautisha na masikini. Karibu upate UCHAMBUZI KAMILI wa kitabu hiki cha EVERYDAY MILLIONAIRES kwa kubonyeza MAANDISHI HAYA.

Tumekuwa na mjadala mzuri wa uchambuzi wa kitabu hiki cha EVERYDAY MILLIONAIRE ambapo watu wameshirikisha yale waliyojifunza na hatua wanazochukua. Fungua hapo chini kujifunza zaidi kutoka kwenye kitabu na michango ya wengine.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.