Rafiki yangu mpendwa,
Watu huwa tunahangaika kwenye mambo tunayofanya na maeneo tunayoenda tukitafuta maisha mazuri.
Mtu unaona kwa shughuli unazofanya au eneo ulipo, huwezi kuwa na maisha mazuri. Hivyo unaamua kwenda eneo jingine na kubadili unachofanya ili kuwa na maisha mazuri.
Cha kushangaza sasa, hata unapobadili eneo au kile unachofanya, bado changamoto ulizokuwa unakutana nazo awali unaendelea kukutana nazo. Yaani ulifanya mabadiliko ili ukwepe baadhi ya vitu, matokeo yake umeendelea kuwa navyo.
Ukweli ni kwamba huwezi kujikimbia wewe mwenyewe, hivyo kama sababu ya kubadili unachofanya au ulipo ni kukimbia yale unayosababisha, bado utakuwa nayo.

Mwanafalsafa Marcus Aurelius kwenye kitabu cha kumi cha Meditations anatuonyesha jinsi ambavyo maisha mazuri yapo kila mahali, kwa kuanzia na hapo ulipo sasa.
Marcus anatuambia kuna machaguo matatu ambayo tunayo kuhusu maisha yetu. Moja ni kuyapokea maisha na kuyaishi kwa namna yalivyo. Mbili ni kujitenga na maisha yanavyoenda na kukaa mbali. Na tatu ni kuachana na maisha moja kwa moja, yaani kufa. Hapo unaona chaguo sahihi ni kwenda na maisha vile yanavyokwenda, maana hayo machaguo mengine hayaleti matokeo yoyote bora.
Kila kinachoendelea leo, kimewahi kutokea tena huko nyuma. Hakuna chochote kipya, maisha ni onyesho linalojirudia rudia, kinachobadilika ni wahusika tu. Kwa kujua hili inatuonyesha jinsi ambavyo maisha mazuri yanaanza na sisi wenyewe kwa pale tulipo kuliko kuhangaika na kwenda kwingine.
Mnyama anayechinjwa, huwa anarusha rusha mateke na kupiga kelele, lakini hilo huwa halizuii kuchinjwa kwake. Hivyo pia ndivyo ilivyo kwa watu wanaolalamika kuhusu maisha, malalamiko yao huwa hayabadili chochote. Huwezi kuwa na maisha mazuri kwa kulalamika, bali utakuwa nayo kwa kuchukua hatua kwenye yale ambayo hayajakaa sawa.
Kabla hujatafuta makosa ya wengine, jiulize kwanza ni makosa gani ambayo wewe unayafanya na yamefanana na hayo ya wengine. Huwa ni rahisi kuwakosoa wengine kwa yale wanayofanya, wakati sisi wenyewe tunafanya makosa kama hayo au yanayoendana na hayo. Kwa kutambua hata sisi tunakosea kama wao, itatupa unyenyekevu na kuangalia jinsi ya kujirekebisha wenyewe na kuwarekebisha wengine.
Kila kitu kinapita, hakuna kinachodumu milele. Ukiangalia watu wote mashuhuri na wenye mamlaka ambao wamewahi kuwepo hapa duniani na sasa hawapo tena, tena hata hawakumbukwi sana, unaona jinsi ambavyo maisha siyo vile tunavyoyachukulia. Huwa tunajipa umuhimu sana tunapokuwa hai, lakini hatujui jinsi umuhimu wetu unavyopotea baada ya kufa kwetu. Tunapaswa kujenga maisha mazuri kwetu kwa kufanya yale yaliyo sahihi na siyo kuhangaika na yaliyo nje ya uwezo wetu.
SOMA; Falsafa Ya Ustoa; Kuwa Mtu Mwema Kwa Vitendo Na Siyo Nadharia.
Usikubali mtu yeyote aweze kusema kwa usahihi kwamba wewe siyo mwaminifu na siyo mwema. Kama mtu yeyote anaweza kusema hivyo, unayo mamlaka ya kumfanya aonekane ni mwongo. Na utafanya hivyo kwa kuwa mwaminifu na kuwa mwema. Maisha mazuri ni kuchagua kuyaishi kwa usahihi, kwa kuwa mwaminifu na kuwa mwema. Hayo yapo ndani ya uwezo wako, hakuna wa kukuzuia kuishi maisha yako hivyo.
Chochote kinachokuzuia, kinakuimarisha zaidi kuliko kukudhoofisha. Viumbe wengine huwa wanadhoofishwa na vitu vinavyowazuia, kwa sababu hawana uwezo wa kufikiri na kuamua kwa utofuati. Lakini sisi binadamu tunao uwezo wa kufikiri na kuamua, hivyo tunapozuiwa na kitu chochote, tunakuwa imara zaidi. Usikimbie kitu kwa sababu ya magumu au changamoto unazokutana nazo, badala yake tumia uwezo wako wa kufikiri ili uweze kuvuka vikwazo hivyo na kufanya makubwa.
Rafiki, hayo ni ya msingi kuhusu kuwa na maisha bora kutoka kwenye falsafa ya Ustoa. Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA hapo chini tumekuwa na mjadala mzuri wa hili, karibu usikilize ili ujifunze na uweze kujenga maisha mazuri kwako ukianzia hapo ulipo sasa.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.