3437; Kuna mtu atakufanyia.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,
Kwa uvivu wako, kuna baadhi ya vitu unaweza kuamua kutokufanya kwenye maisha yako.
Na hapo utakuwa umetoa upenyo kwa wengine kukufanyia vitu hivyo.
Kwa bahati mbaya sana, hawatakufanyia kwa sababu wanataka unufaike, bali kwa sababu watanufaika zaidi wao.

Kama hautaweka malengo kwa ajili yako, watu wengine watakuwekea malengo. Lakini yatakuwa ni malengo ambayo yanawanufaisha wao.

Kama hautajiwekea vipaumbele kwenye maisha yako, watu wengine watakuwekea vipaumbele. Lakini vitakuwa ni vipaumbele vinavyowanufaisha wao.

Kama hautajisukuma wewe mwenyewe kufanya makubwa, wengine watakusukuma ufanye makubwa, ambayo yana manufaa kwao.

Na kama hautajipanga wewe mwenyewe, wengine watakupanga kwenye mikakati yao ya kufanikiwa.

Kumbuka ya kwamba hayupo mtu yeyote ambaye anafanya jambo lisilokuwa na manufaa kwake.
Kila mtu anaangalia maslahi yake binafsi, hivyo unapoona watu wanakufanyia mambo fulani, jua ina manufaa zaidi kwao.

Unaweza kuchagua kulaumu kwa nini watu wajiangalie wao wenyewe zaidi.
Lakini hilo halitakusaidia, hivyo ni bora uanze kujiangalia wewe mwenyewe.

Shika udhibiti wa maisha yako, kwa kuwajibika na kila kitu kwenye maisha hayo.
Hiyo ndiyo njia ya kuweza kunufaika binafsi na kila unachofanya.

Kama unachukua hatua lakini huwajibiki, jua ni hatua zinazowanufaisha wengine na siyo wewe.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe