Rafiki yangu mpendwa,

Karibu kwenye kipengele hiki cha #HadithiZaKocha ambapo nakushirikisha hadithi fupi yenye mafunzo muhimu, kisha wewe unang’amua mafunzo hayo na kuyashirikisha.

Kwenye somo hili tunakwenda kujifunza kutoka kwenye kisa cha Mbwa mwitu na Mbwa wa nyumbani.

Siku moja mbwa mwitu alikuwa akipita njiani na kukutana na mbwa wa nyumbani. Mbwa mwitu alikuwa amechoka na mwenye njaa, afya yake ilionekana dhoofu. Mbwa wa nyumani alikuwa ameshiba na kuonekana mwenye afya.

Mazungumzo yao yalikuwa kama ifuatavyo;

Mbwa wa nyumbani; “Habari za siku nyingi, unaendeleaje?”

Mbwa mwitu; “Nipo nabangaiza, maisha yamekuwa magumu sana, chakula kinapatikana kwa taabu.”

Mbwa wa nyumbani; “Pole sana kwa hayo unayopitia. Kwa nini usiungane na mimi, ukaja tukakaa wote kwa binadamu?”

Mbwa mwitu; “Kwani kukaa kwa binadamu kuna faida gani?”

Mbwa wa nyumbani; “Faida ni nyingi tu, unapewa chakula kizuri na mahali pa kuishi na wewe kazi yako ni kuwalinda tu usiku.”

Mbwa mwitu; “Aisee, kumbe maisha ndiyo rahisi hivyo?”

Mbwa wa nyumbani; “Ndiyo, huna haja ya kuteseka wakati maisha mazuri yapo.”

Mbwa mwitu alitafakari kwa kina na kuona jinsi ambavyo maisha yake yanaweza kubadilika. Katika tafakari yake, hasa baada ya kumwangalia mbwa wa nyumbani kwa karibu, aliona kitu ambacho kilimfikirisha zaidi. Maongezi yakaendelea kama ifuatavyo;

Mbwa mwitu; “Hiyo kamba iliyopo shingoni kwako kazi yake nini?”

Mbwa wa nyumbani; “Hii kamba ni kwa ajili ya binadamu kunifunga ili nikae pale wanapotaka nikae.”

Mbwa mwitu; “Kwa hiyo unaniambia pamoja na kupewa chakula kizuri, huruhusiwi kwenda kokote unakotaka kwa muda unaotaka?”

Mbwa wa nyumbani; “Ndiyo, muda mwingi nafungiwa sehemu moja na wanadamu.”

Mbwa mwitu; “Ni afadhali nibaki na njaa nikiwa huru, kuliko kushiba nikiwa kifungoni.”

Mbwa mwitu aliondoka haraka sana.

Rafiki, hicho ndiyo kisa cha Mbwa mwitu na mbwa wa nyumbani, karibu ushirikishe kwenye maoni hapo chini yale uliyojifunza kutoka kwenye kisa hicho na jinsi unavyoenda kufanyia kazi.

Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA hapo chini nimeelezea kisa hiki kwa ufupi, fungua uendelee kujifunza na uchukue hatua.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.