Rafiki yangu mpendwa,

Uwekezaji ndiyo njia kuu ya kujenga na kutunza utajiri.

Watu huwa wanachanganya kipato kikubwa (rich) na utajiri (wealth) na maisha yao huwa magumu sana.

Huwa tunaona mara nyingi watu wenye vipato vikubwa wakiwa na maisha mazuri pale kipato kinapokuwa kinaingia. Lakini kipato kikifika ukomo, maisha yao yanakuwa magumu sana.

Hiyo ni kwa sababu wanakuwa hawajajenga utajiri kupitia uwekezaji, utajiri ambao unawazalishia kipato bila kufanya kazi moja kwa moja.

Kitu kingine ambacho watu huwa hawakijui ni kwamba faida kubwa ya uwekezaji inatokana na muda kuliko hata kiasi kinachowekezwa. Pale uwekezaji unapofanyika kwa muda mrefu bila ya kuingiliwa, ndivyo ukuaji wake unavyokuwa mkubwa na wa uhakika.

Kwa mfano kwenye soko la hisa, hatari huwa ziko hivyo;

Ndani ya mwaka mmoja, hatari ni 50 kwa 50, yaani asilimia 50.

Kwa miaka mitano, hatari ni asilimia 30.

Miaka kumi, hatari ni asilimia 10 mpaka 20.

Miaka 20 hatari ni chini ya asilimia 10.

Na miaka 25 na kuendelea, hatari ni karibu na sifuri. Yaani hatari inakuwa ndogo sana ya kupoteza. Japo hakuna uwekezaji ambao hauna hatari kabisa, lakini unapokaa kwenye uwekezaji kwa muda mrefu, uhakika wa kupata faida unakuwa mkubwa.

Licha ya uhakika huo mkubwa wa kupata faida kadiri mtu unavyokaa kwenye uwekezaji, bado wengi huwa wanashindwa kukaa kwa muda mrefu. Wengi wamekuwa wanauza uwekezaji wao mapema sana na kushindwa kunufaika nao.

SOMA; #NjiaYaUtajiri; Tumia Mifuko Ya Pamoja Ya Uwekezaji Kujenga Utajiri Mkubwa.

Wengi huwa wanajipa sababu za kwa nini ni sahihi kwao kuuza uwekezaji huo, lakini nyingi huwa siyo sababu sahihi. Ili kuepuka kujidanganya na kuvuruga uwekezaji wako, unapaswa kujiwekea vigezo mapema vya wakati gani utauza uwekezaji wako.

Ili uweze kuwekeza kwa muda mrefu na kupata faida, unapaswa kujizuia usiuze mapema. Na ili kujizuia usiuze mapema, kuna nyakati tatu tu ndiyo unapaswa kuuza uwekezaji wako.

Usikubali kuuza uwekezaji wako kwa sababu nyingine yoyote isipokuwa nyakati hizo tatu. Ukiweza kuzingatia hili, utawekeza kwa muda mrefu na kupata faida kubwa.

Nyakati tatu za kuuza uwekezaji wako nimezielezea kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA hapo chini. Karibu ujifunze na kuchukua hatua ili uweze kujenga utajiri kwa uhakika.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.