Karibu rafiki,
Ipo wazi kwamba, chini ya jua vitu vingi vinaweza kufanyika. Ikiwa kuna kitu ungependa kubadili au kutengeneza upya katika maisha yako amini inawezekana.

Huenda ni kutengeneza wateja tarajiwa wengi zaidi, kupiga simu nyingi zaidi, kutembea wateja, kufuatilia, kuhudumia vizuri wateja, kufanya mauzo makubwa zaidi, kufanya tahajudi, kuamka asubuhi sana, kusoma vitabu au kufanya mazoezi zaidi.


Inawezekana kabisa. Kuwa unachotaka, ukiamua leo. Hii ni kwa sababu hakuna aliyezaliwa anajua kila kitu. Ni kupitia kujifunza na kufanya.

Muhimu tu, ni kuchagua kitu unachotaka kufanya na kuanza kukifanya mara moja.

Ukianza kukifanya utapata matokeo makubwa. Moja, yanaweza kuwa makubwa. Mbili, yanaweza kuwa  madogo kutegemea na juhudi au namna ya utendaji wako.

Kumbuka, kitu unapokifanya mara  kwa mara kinakuwa tabia na sehemu ya maisha yako.

Kanuni ya 21/90 inasema,”inachukua siku 21, kujenga tabia mpya na siku 90 kuifanya iwe tabia ya kudumu”.

Je, kuna tabia ungependa kutengeneza leo? Anza sasa. Fanya kwa siku 21, bila kuacha. Baada ya hapo endelea kufanya kwa siku 90, itakuwa sehemu ya maisha yako.

Mambo ya kuzingatia kujenga tabia inayodumu;

Moja; Weka mipango kuhusu hitaji lako.
Kuweka mpango au malengo ni sehemu ya kuiandaa akili na mwili kukupa ushirikiano.

Pia, ni kufungua milango ya kuona unakoelekea. Tony Robinson aliwahi kusema, “Kuweka malengo ni hatua ya kufanya visivyoonekana kuonekana”.

Unataka kuhudumia wateja wengi, weka idadi ya wateja unaotaka kuwahudumia kwa siku, wiki na mwezi.

Mbili; Chukua hatua za haraka kufanyia kazi mpango wako.
Unapochukua hatua inakusaidia kujua namna nzuri kuboresha.

Una mpango wa kupiga simu 100 anza leo. Kupitia kufanya utafundua kuna namna unahitaji kuboresha “script” yako au eneo lingine.

Tatu; Fokasi kwenye kitu unachotaka.
Huwezi kufanya kila kitu kwa wakati mmoja, lazima uchague baadhi na ufanye.

Kama kitu ni kikubwa kifanye katika hatua ndogo ndani ya muda husika. Baadaye itakuwa sehemu ya maisha yako.

Nne; Jitoe kisawa sawa.
Pamoja na kuwa na fokasi, lakini kama haupo tayari kujitoa kutimiza wajibu wako, hutaweza kufanikiwa kujenga tabia mpya.

Tupo kwenye dunia yenye kelele, usumbufu na mwingiliano wa vitu vingi ndiyo maana unahitaji kujitoa sana kupambania kitu ulichochagua ambacho ni kuuza zaidi.

Tano; Rudia, rudia tena.
Tabia mpya  inajengwa kwa kurudia kitu mara kwa mara.

Mfano, mtoto mdogo anapofikia hatua ya kusimama, haanzi tu mara moja na kusimama. Anajaribu sana kusimama huku akianguka mara nyingi.  Mwishowe anafanikiwa kusimama. 

Kurudia inafanya akili ione uwezekano na itenge nafasi ya kukifanya kitu husika kwa ubora.

Hatua za kuchukua leo; Usifanye kitu mara moja ukaacha, hutoona matokeo.  Mfano mzuri upo kwenye kujenga mwili.

Huwezi kula mara moja ukaacha, lazima ule mara kwa mara ili mwili uwe imara.

Hali hii ndivyo ilivyo kwenye utendaji wetu. Simu zipigwe mara kwa mara, rufaa ziombwe mara kwa mara, utembeleaji ufanyike mara kwa mara. Mwishowe mwili mzima na viungo vyake vitakupa ushirikiano. 

Wako Wa Daima

Lackius Robert Mkufunzi  Wa Mauzo Na Mwandishi.

0767702659/ mkufunzi@mauzo.tz

Karibu tujifunze zaidi.