3445; Usipunguze, bali ongeza.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Kufanikiwa na kushindwa kwenye maisha ni vitu vya mpito tu.
Huwa havidumu milele mpaka sisi wenyewe tuchukue hatua za makusudi kuvifanya vidumu milele.
Hiyo ina maana kwamba, wale walioshindwa na wakabaki wameshindwa hivyo kwa muda mrefu, kuna hatua za makusudi walizochukua kuhakikisha wanabaki kwenye kushindwa.
Kadhalika kwa wale wanaofanikiwa na wakabaki kwenye mafanikio yao kwa muda mrefu, kuna hatua za makusudi wanazokuwa wamechukua na zikawafanya wabaki hapo.
Watu wengi wanaoanzia chini huwa hawaridhishwi na hali wanazokuwa wanapitia.
Hilo linawasukuma kuweka juhudi kubwa zaidi kwenye kila anachokifanya.
Juhudi hizo zinamlipa kwa kuweza kupiga hatua za mafanikio, anatoka chini na kwenda juu.
Na hapo ndipo tatizo linapoanzia,
Pale mtu anapoanza kupata matokeo mazuri, anaona tayari ameshamaliza kila kitu.
Anaacha kuweka juhudi kubwa alizokuwa anaweka kwa kudhani mafanikio aliyopata ndiyo ushindi wa kuduku.
Matokeo yake yamekuwa ni kupata anguko na kurudi chini kabisa.
Mafanikio, hasa ambayo ni madogo na ya wastani huwa ni sumu na kikwazo kwa mtu kupata mafanikio makubwa zaidi.
Hiyo ni kwa sababu watu huwa wanajifunza masomo yasiyokuwa sahihi kutoka kwenye mafanikio wanayokuwa wamepata.
Sababu namba moja ya wale waliofanikiwa kushindwa ni kuacha kufanya yale yaliyowafikisha kwenye mafanikio hayo.
Wanasahau masomo ambayo kushindwa kuliwafundisha na kuanza kujifunza masomo yasiyo sahihi kutoka kwenye mafanikio waliyopata.
Mafanikio hayajawahi kuwa mwalimu mzuri.
Kwani mafanikio yamekuwa yanatengeneza wanaoshindwa wengi zaidi.
Pale tu mtu anapoanza kuridhika na mafanikio aliyopata, hapo ndipo anapokarisha anguko.
Kwenye maisha, unapofanikiwa hupaswi kupunguza kasi ya yale uliyofanya na yakakupa mafanikio.
Bali unapaswa kuongeza kasi zaidi ili uzidi kupiga hatua za kimafanikio.
Mafanikio ni sawa na mashine ya mazoezi ya kukimbia, ukisimama unarudi nyuma na kuanguka. Ukienda na kasi yake unabaki pale ukipo. Na ili kwenda mbele, ni lazima uongeze kasi kuliko ya mashine yenyewe.
Kila unapofanikiwa, ongeza juhudi na kasi zaidi ili uendelee kufanikiwa.
Tofauti na hapo, utaanguka vibaya sana.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe