Habari njema matajiri wawekezaji,
Karibuni kwenye mfululizo wetu wa masomo ya programu ya NGUVU YA BUKU, programu inayoendeshwa kwa msingi kwamba KILA MTU ANAWEZA KUWA TAJIRI na kupitia programu hii tunatekeleza hilo kwa vitendo.
Kwenye somo hili unakwenda kujifunza jinsi unavyoweza kusukumwa na matumizi yako kufanya uwekezaji mkubwa na kufikia uhuru wa kifedha.
Kadiri mtu anavyofanya uwekezaji mkubwa na kwa muda mrefu, ndivyo anavyojiweka kwenye nafasi nzuri ya kufikia uhuru wa kifedha kwa uhakika.
Lakini wengi wamekuwa wanakwama kufikia uhuru wa kifedha kwa sababu wanashindwa kuwekeza. Na kikubwa kinachowafanya washindwe kuwekeza ni matumizi wanayokuwa nayo kwenye kipato wanachoingiza.

Swali tunalopaswa kujiuliza ni je hatuwezi kuyatumia hayo hayo matumizi yakatusukuma kufanya uwekezaji mkubwa zaidi?
Kujibu swali hilo tuangalie kwanza kile ambacho tayari kinatokea. Ambacho tayari kinatokea ni kipato kinapoongezeka, matumizi nayo pia yanaongezeka. Yaani hilo ni jambo ambayo huwa linatokea lenyewe bila hata ya kuhitaji nguvu kubwa. Pale kipato kinapoongezeka, matumizi nayo huwa yanaongezeka kuendana na kipato hicho.
Kama hilo linawezekana, yaani ongezeko la kipato linapelekea ongezeko la matumizi, ina maana tunaweza kufanya kinyume chake pia. Kufanya kinyume chake ni kufanya matumizi yakusukume kuongeza kipato na kuwekeza zaidi.
Hapa unachofanya ni kusukumwa na matumizi unayokuwa nayo ili uongeze kipato na kufanya uwekezaji mkubwa zaidi.
Tumekuwa tunajifunza kwamba tunapaswa kudhibiti matumizi yetu yasizidi kipato. Na hilo linatulazimisha tuzingatie matumizi ya msingi kwanza kabla ya kufanya matumizi yasiyokuwa ya msingi.
Matumizi ya msingi ni yale ambayo maisha hayawezi kwenda bila ya kuyafanya. Mfano chakula, mavazi, malazi, afya na elimu. Na unapoangalia, matumizi hayo ndiyo yanachukua sehemu kubwa ya kipato tunachoingiza.
Pamoja na matumizi hayo ya msingi, huwa tuna matumizi mengine ambayo siyo ya msingi sana, lakini huwa tunapenda kuyafanya. Hayo ni matumizi ambayo maisha yetu yanaweza kwenda hata tusipoyafanya, lakini tukiyafanya tunajisikia vizuri. Haya ni matumizi kwenye vitu ambavyo tunapenda lakini maisha hayakwami bila ya kuwa navyo.
Ni hayo matumizi ndiyo tunaweza kuyatumia kufanya uwekezaji zaidi na kufikia uhuru wa kifedha mapema.
Jinsi ya kutumia matumizi unayopenda kufanya uwekezaji ni kufuata hatua hizi mbili;
Hatua ya kwanza ni kuamua kwamba utafanya matumizi yote unayopenda kufanya bila ya kuzuiwa na chochote. Utakazana kuongeza kipato chako ili uweze kukidhi matumizi hayo. Yaani hutayapata kwa kukopa, bali kwa kuongeza kipato chako.
Hatua ya pili ni kuhakikisha unawekeza kiasi hicho hicho cha matumizi kabla ya kufanya matumizi hayo. Yaani ukishakuwa umeamua kufanya hayo matumizi, unawekeza kwanza kiasi hicho ndipo unafanya matumizi. Yaani hapa inabidi uwe na mara mbili ya kile unachotaka kutumia, ili uwekeze na kufanya matumizi.
Kwa mfano kama sasa una simu inayofanya kazi vizuri tu, lakini kuna simu nyingine ambayo umeipenda zaidi na kuamua kuinunua, kama simu hiyo inauzwa laki 5, unawekeza kwanza laki 5 kisha ndiyo unanunua simu hiyo. Hapo ina maana unapaswa kuwa na milioni moja.
SOMA; Mpango Wa Usimamizi Wa Fedha Binafsi (Personal Finance Management Plan)
Tumia njia hii kwenye matumizi yote ambayo siyo yale ya msingi kabisa ambayo yanakwamisha maisha usipoyafanya. Kama huwezi kuwekeza kiasi hicho hicho kabla ya kuwekeza, hupaswi kufanya hayo matumizi.
Rafiki, hii siyo kanuni mpya, bali huwa ipo sana kwenye eneo la USIMAMIZI WA FEDHA BINAFSI, ambapo inaeleza kama kitu huwezi kununua kwa fedha taslimu na mara mbili, basi bado hujaweza kumudu kitu hicho. Yaani kama umekutana na kitu kizuri na kujiambia unataka kukinunua, swali la kwanza ni je unaweza kununua kwa fedha taslimu na siyo mkopo? Kama jibu ni ndiyo unaenda kwenye swali la pili ambalo ni je unaweza kununua mara mbili kwa fedha hizo taslimu? Kama kuna hapana kwenye swali lolote hapo, hupaswi kufanya matumizi hayo.
Hapa tumeigeuza kanuni hiyo kwenda kwenye vitendo, hatujiulizi tu kuhusu kununua taslimu au kununua mara mbili, badala yake tunawekeza kabisa kiasi kile kile cha matumizi kabla hatujafanya matumizi hayo. Kwa njia hii hata ukifanya matumizi ya anasa, hutakuwa na majuto, kwa sababu unajua kiasi hicho hicho umeshakiwekeza.
Hii inaenda hata kwenye matumizi ya starehe, kunywa vitu kama soda, pombe na starehe nyingine siyo matumizi ya msingi. Maisha yako hayataathirika kwa namna yoyote ile kama usipofanya matumizi hayo. Lakini uko huru kufanya matumizi hayo, kama tu utawekeza kiasi hicho hicho kabla ya kuwekeza.
Kama umejichokea na kusema unahitaji kwenda kufanya mapumziko mahali fulani, jua kabisa kiasi gani unaenda kutumia kwenye mapumziko hayo, kisha wekeza kiasi hicho hicho kabla ya kufanya mapumziko yako.
Swali ni vipi kama unaweza kumudu matumizi hayo tu lakini huwezi kuwekeza kiasi hicho hicho? Jibu lipo wazi, hicho kiasi kiwekeze na achana na hayo matumizi. Kama unayataka sana matumizi, pambana uweze kupata mara mbili ili uwekeze na kutumia. Kama umeshindwa kupata mara mbili, kipaumbele ni uwekezaji kabla ya matumizi.
Weka hii kuwa sheria ya maisha yako, ainisha matumizi ya msingi ambayo ndiyo utayafanya kwenye kila kipato chako na hayo yasizidi kipato hicho. Matumizi mengine yote ambayo hayajaingia kwenye hayo ya msingi, hakikisha unawekeza kwanza kiasi hicho hicho cha matumizi unayotaka kufanya ndiyo uyafanye.
Hata kama ni michango ya misaada au sherehe unatoa kwa watu wengine, hakikisha umewekeza kiasi hicho kwanza kabla ya kutoa mchango. Na kama huwezi kufanya vyote, basi wekeza kile ulichonacho, au hicho ulichopata gawa mara mbili, nusu wekeza na nusu ndiyo utoe.
Ukiweza kuzingatia hili kwa uaminifu mkubwa, utaweza kukuza uwekezaji wako kwa kiasi kikubwa sana na hilo litapunguza muda wa kufika kwenye uhuru wa kifedha.
SOMA; STAAFU NA UHURU WA KIFEDHA.
MJADALA WA SOMO.
Karibu kwenye mjadala wa somo hili, jibu maswali yafuatayo kama sehemu ya uthibitisho wa kusoma, kuelewa na kwenda kufanyia kazi.
1. Umeelewaje kuhusu kusukumwa na matumizi kufanya uwekezaji mkubwa zaidi?
2. Orodhesha matumizi yako ya msingi ambayo ni ya lazima kufanya ili maisha yako yaweze kwenda.
3. Orodhesha matumizi ambayo umekuwa unayafanya, ambayo hata usipoyafanya maisha yako yataendelea kwenda.
4. Unaenda kujiwajibishaje kuhakikisha unawekeza kwanza kabla hujafanya matumizi yasiyo ya msingi?
5. Karibu kwa maswali, maoni, mapendekezo, mrejesho na ushuhuda kuhusu somo hili na programu nzima ya NGUVU YA BUKU.
Shirikisha majibu ya maswali hayo kama sehemu ya ushiriki wako kikamilifu kwenye programu hii ya NGUVU YA BUKU.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE.
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.