3472; Hamu na uwezo.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Mafanikio huwa ni jadi kwa mtu ambaye ana hamu kubwa ya kupata ushindi na uwezo mkubwa wa kufanya kazi.
Hizo ni rasilimali kubwa mbili ambazo lazima ziwepo kwa mtu ili aweze kupata mafanikio makubwa.
Hamu kubwa ya mafanikio ndiyo inamfanya mtu kuwa na matamanio makubwa na kupata msukumo wa kuchukua hatua zinazohitajika ili mafanikio yaweze kupatikana.
Safari ya mafanikio huwa ni ngumu na yenye changamoto mbalimbali, hamu na matamanio ndiyo vinamsukuma mtu kuendelea licha ya hizo changamoto anazokutana nazo.
Mafanikio yoyote yale ni matokeo ya mtu kuweka kazi kubwa na kwa muda mrefu. Ndiyo maana uwezo mkubwa wa kufanya kazi ni hitaji muhimu sana kwa mafanikio makubwa.
Kazi inapaswa kufanyika kubwa, kwa muda mrefu na kwa kasi na viwango vikubwa. Haitoshi tu kufanya kazi muda mrefu, lazima huo ufanyaji uwe na tija, yaani juhudi zinazowekwa ziweze kuzalisha matokeo makubwa.
Watu wengi wanafanya kazi sana lakini bado hawafanikiwi, kwa sababu kazi wanazokuwa wanafanya hazina tija.
Wanafanya kazi za kawaida kwa kasi ambayo ni ndogo na viwango vya chini.
Wanachoshwa sana na hizo kazi, lakini hawapigi hatua.
Ukichukua tu kwamba lazima ufanye kazi kubwa na ukashindwa kujua kazi hiyo inapaswa kuwa na tija, utajichosha sana na bado hutapiga hatua kubwa.
Ukiwa na hamu kubwa ya mafanikio lakini ukakosa uwezo wa kuweka kazi kwa usahihi, unaishia kuwa na uraibu wa hamasa za mafanikio.
Utajihamasisha sana, lakini hakuna mahali utaenda. Utajua kila siri na kila msingi wa kufanikiwa, lakini bado hutafanikiwa.
Ni sawa na kukanyaga mafuta kwenye gari ambayo umekanyaga breki pia. Kelele zitakuwa nyingi, lakini matokeo sifuri.
Ukiweza kufanya kazi kubwa na kwa viwango vizuri lakini ukakosa hamu ya mafanikio, utajikuta unafanya mambo mengi sana na bado usifanikiwe.
Kila linalokuja mbele yako utaruka nalo na mwisho wa siku hakuna hatua kubwa unazoweza kuonyesha umepiga.
Kuwa na hamu kubwa ya mafanikio na uwezo mkubwa wa kufanya kazi vinafanya ufanikiwe kwa uhakika.
Vitu hivyo viwili vinawafanya watu wakuamini na kuwa tayari kushirikiana na wewe kwa namna ambayo ina manufaa makubwa kwako.
Wewe ndiye wa kuamua kama utafanikiwa au la. Amua kwa usahihi ili uweze kupata matokeo sahihi.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe