Habari njema muuzaji bora  kuwahi kutokea,

Hongera na karibu sana kwenye mwendelezo wa makala zetu za ushawishi kutoka kwenye programu yetu ya CHUO CHA MAUZO.

Kwenye jumamosi ya ushawishi tunaongozwa na kauli mbiu yetu inayosema HUPATI UNACHOSTAHILI BALI UNACHOSHAWISHI.

Wiki iliyopita tulifanikiwa kujifunza jinsi ya kuwabadili watu bila kuibua hasira au chuki kanuni ya tatu ambayo ni ongelea makosa yako kabla ya kumkosoa mwingine.

Na kwenye kanuni ya kwanza tulifanikiwa kuondoka na kitu kimoja ambacho ni;

Kabla hujamkosoa mtu kwenye kile ambacho amekosea na unataka arekebishe, elezea kwanza makosa yako kwenye eneo hilo.

Kwa kuanza na kuelezea makosa yako, inamfanya mtu aone anajitahidi na wewe humkosoi kumkomoa, bali unataka awe bora zaidi.

SOMA; Jinsi Ya Kuwabadili Watu Bila Kuibua Hasira Au Chuki Kanuni Ya Tatu

Habari njema ni kwamba leo kwenye jumamosi ya ushawishi, tunakwenda kujifunza jinsi ya kuwabadili watu bila kuibua hasira au chuki kanuni ya NNE ambayo ni TOA MAPENDEKEZO BADALA YA MAAGIZO.

Mpendwa muuzaji bora kuwahi kutokea,

Watu huwa hawapendi kupokea maagizo ya jinsi ya kufanya majukumu yao.
Je, unajua kwa nini?
Kwa sababu wanaamini wanajua wanachofanya, hivyo unapowapa maagizo, unaumiza nafsi zao kwa kuashiria hwajui wanachofanya.

Badala ya kuwapa watu maigizo ya fanya hivi au fanya vile, wewe wape MAPENDEKEZO ya jinsi gani wanaweza kuboresha zaidi kile ambacho wanafanya.

Kwa mfano, unaweza kutumia kauli zifuatazo kuboresha zaidi kile wanachofanya bila kuibua hasira au chuki na mtu.
Kauli kama; unaonaje ukifanya hivi, nadhani hivi inaweza kuwa vizuri zaidi n.k kutamfanya mtu awe tayari kufanya mabadiliko anayoyataka.

Kwa mfano, unapokuwa na mteja na unataka kupendekeza kitu, tumia njia hii utajenga ushawishi kuliko kumpa maagizo moja kwa moja kwa mfano. Badala ya kuchukua bidhaa hii ya kawaida, nadhani hii ya juu inaweza kuwa nzuri zaidi.

Kwa kumwambia hivyo mteja, ataona hujampa maagizo badala yake umempatia mapendekezo kitu ambacho hakitaumiza nafsi zao kwa kuashiria hawajui wanachofanya au wanachotaka kufanya.

Kwa kuwa wewe ni muuzaji bora kabisa kuwahi kutokea, kuwa mtu wa kutoa mapendekezo na siyo maagizo. Jua namna ya kuishi na watu kiushawishi kiasi cha kuwafanya wengine wajisikie vizuri kufanya kazi na wewe,  watu wakijisikia vizuri watajiona  salama, watakuamini na kuwa tayari kukupa fursa au dili nzuri.

Si unajua kauli mbiu yetu inavyosema, hupati unachostahili bali unachomshawishi. Hivyo wakati wote kuwa katika hali ya ushawishi. Washawishi watu kwa jinsi unavyoongea, namna unavyofanya mambo yako, mwonekano wako na mengine mengi yanayofanana na hayo.

Mwisho, unapompa mtu mapendekezo ya aina hii anakuwa tayari kuyafanyia kazi kwa sababu hujaumiza nafsi yake.
Mtu hawezi kuwa na hasira au chuki kama anavyokuwa nayo pale unapompa maagizo moja kwa moja.

Rafiki na mwalimu wako anayekupenda na kukujali katika mauzo,
Mwl.Deogratius Kessy

Mwalimu/Mwandishi/Mjasiriamali
Makamu Mkuu wa CHUO CHA MAUZO.
makamu@mauzo.tz, 📞0717101505//0767101504