3476; Kuwa aliyeshindikana ili ufanikiwe.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,
Sehemu kubwa ya ugumu wa mafanikio huwa inatokana na ushindani wa wengine wengi walio kwenye safari hiyo pia.

Kadiri kunavyokuwa na watu wengi wanaotaka kitu fulani, ugumu wa kukipata kitu hicho huwa unaongezeka maradufu.

Kwenye kila safari ya mafanikio, ushindani huwa ni mkali sana kwenye hatua za chini.
Hiyo inasababishwa na wengi wanaokuwa kwenye hatua hizo za chini.

Njia pekee ya kushinda ushindani ili ufanikiwe siyo kushindana moja kwa moja, bali kushindikana.

Kushindana moja kwa moja ni kufanya kama wanavyofanya wengine. Hapo unakuwa umejiweka kwenye kundi kubwa la watu  na ushindani kuwa mkali.

Kushindikana ni kuwa kinyume na wengine wengi. Hapo unakuwa umejitofautisha kabisa na yale wanavyofanya wengine. Hiyo inafanya uwe mbele zaidi ya wengine.

Eneo rahisi sana ambalo unaweza kujitofautusha na kushindikana ni muda.
Watu wengi wanafikiri kwa muda mfupi na hata kile wanachojenga wanaangalia matokeo ya haraka.

Wakati wengine wanafikiria kwa miezi na mwaka, wewe unapaswa kufikiria kwa miongo.
Kadiri unavyofikiria kwa miaka mingi ndivyo unavyowaacha wengi wana nyuma.

Unapofikiri kwa muda mrefu, ushindani unakuwa rahisi kwa sababu wengi unakuwa umewaacha kabisa.

Kuweka juhudi kubwa sana kwenye kile ambacho mtu anafanya ni njia nyingine ya kushindikana.
Tunaishi kwenye zama ambazo wengi wanataka kupata mafanikio makubwa lakini hawapo tayari kuweka kazi.

Kitendo cha wewe kuwa tayari kuweka kazi kubwa, kinakutofautisha kabisa na wengi ambao hawapo tayari kuweka kazi kubwa.

Ukileta pamoja kufikiri kwa muda mrefu na kuweka juhudi kubwa ya kazi, unakuwa umetengeneza upekee ambao hayupo anayeweza kuufikia.

Uzuri hayo yote ni mambo yaliyo ndani ya uwezo wako kuyafanya, yafanyie kazi ili uweze kushindikana na ujenge mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe