Kila mtu katika maisha yake ya kila siku anao utaratibu unaomuongoza. Utaratibu huu upo “automatic” na mwingine anauweka mwenyewe.
Mfano: mara baada ya kuamka mapema asubuhi, wapo wanaowasha simu zao kuangalia ujumbe ulioingia (SMS) au simu zilizopigwa (Calls) usiku.
Wapo wanaochukua kitabu kusoma au kuandika. Wapo wanaowasha redio au TV kufuatilia taarifa za habari mbalimbali.
Baada ya hapo, hunawa uso, kupiga mswaki, kisha kwenda mezani kunywa chai. Wengine huanza na chai, kupiga mswaki na kuoga.
Huo ni utaratibu au mpangilio wa mtu wakati wa asubuhi anapoamka.

Tukija upande wa biashara, ili wateja wafuatiliwe vema na biashara iendelee kuuza, ni lazima kuwe na mpango mzuri wa shughuli zinazoenda kufanyika katika siku, wiki, mwezi na mwaka husika.
Mipango ni muhimu sana kwa ajili ya maendeleo ya kila muuzaji katika biashara. Hii ni kwa sababu “mpango mzuri wa mambo yanayoenda kufanyika unapunguza sababu zisizo za lazima””.
Ukisoma biblia utaona kuwa; Mungu alikuwa na uwezo wa kuumba kila kitu kwa siku moja. Lakini kwa kuwa alitambua umuhimu wa kuwa na mpango pamoja na mpangilio mzuri wa vitu na kutuonyesha kwamba yeye ndiye “Bwana wa Mipango” alifanya uumbaji kwa siku sita na kupumzika siku ya saba. (Mwanzo 1:1-31).
Hali hiyo inaonyesha dhahiri kuwa, kitu kinachofanyika kwa mpangilio maalumu kinafanyika kwa ufanisi mkubwa. Tofauti na kitu kinachofanyika pasipokuwa kimepangiliwa au kuwa kwenye mpango maalumu kiutendaji.
Kwenye ufuatiliaji wa wateja katika biashara uwepo wa mpango mzuri wa majukumu una faida zifuatazo;
Moja; Kuongeza ufanisi wa kazi.
Muuzaji aliyepangilia majukumu yake, uwezo wa kuyafanikisha ni mkubwa tofauti na asiyepangilia. Hii ni kwa sababu anaweka nguvu katika yale aliyopanga kufanya.
Mbili; Huduma nzuri kwa wateja.
Hii inatokana na uwepo wa “script” nzuri iliyopangiliwa muuzaji wakati wa mazungumzo na mteja pamoja na sera ya kampuni kuhusu kuwahudumia vema wateja.
Tatu; Kutimiza malengo husika.
Malengo yaliyoandikwa ni rahisi kutimizwa kuliko ya kutoa tu kichwani. Mfano, malengo ya mauzo ya kiasi kadhaa, simu kadhaa au utembeleaji hufanikiwa Kwa kuwekwe kwenye mpango mzuri.
Nne; Hupunguza sababu zisizo za lazima.
Wakati mwingine sisi wauzaji huwa tunajikwepa kwenye sababu baada ya kutotimiza jambo fulani. Huku tukisema, hatukujua au tumesahau, lakini kitu kikiwa kwenye mpango mzuri ni rahisi kukifanya kwa wakati.
Jinsi ya kuweka mipango mizuri na kufanikisha majukumu yako;
Moja; Angalia muda wako kwa siku, wiki, mwezi na mwaka husika.
Mbili; Ainisha namba za mauzo, simu, wateja wapya, tarajiwa, rufaa, au utembeleaji unaotaka kufikia kwa siku, wiki, mwezi au mwaka.
Wakati ndio huu kuweka mpango mzuri wa kufanya ufuatiliaji mkubwa ili kukuza mauzo na biashara kwa ujumla.
SOMA; 2780; Siyo muda, ni vipaumbele.
Kumbuka, “mpango mzuri wa vitu au majukumu unasaidia kuondoa sababu zisizo za lazima”. Weka mpango, fanyia kazi mpango wako. Hakika utauza sana.
Wako Wa Daima
Lackius Robert
Mkufunzi Msaidizi Chuo Cha Mauzo.
0767702659/ mkufunzi@mauzo.tz
Karibu tujifunze zaidi..