Habari njema muuzaji bora kuwahi kutokea,
Hongera na karibu sana kwenye mwendelezo wa makala zetu za ushawishi kutoka kwenye programu yetu ya CHUO CHA MAUZO.
Kwenye jumamosi ya ushawishi tunaongozwa na kauli mbiu yetu inayosema HUPATI UNACHOSTAHILI BALI UNACHOSHAWISHI.
Wiki iliyopita tulifanikiwa kujifunza jinsi ya kuwabadili watu bila kuibua hasira au chuki kanuni ya 6 ambayo ni TAFUTA KITU CHA KUSIFIA
Na kwenye kanuni hiyo ya SITA tulifanikiwa kuondoka na kitu kimoja ambacho ni;
Hakuna kitu ambacho watu wanapenda kama kuthaminiwa, kusifiwa na kutiwa moyo kwenye kile wanachofanya. Hilo linapofanyika kwa ukweli kabisa kutoka ndani ya moyo wa mtu, anayelengwa anajua na anashawishika zaidi.
Huwa tunasikia kwamba watu wanakufa kwa kukosa chakula. Lakini nikuambie kitu, watu wengi zaidi wanateseka na njaa ya kukosa kuthaminiwa, kusifiwa na hata kutiwa moyo.
Kadiri unavyoonekana kukumbuka mambo muhimu ya watu, ndivyo wanavyokuamini, kuvutiwa na kushawishika na wewe. Hii ndiyo nzuri ya kujenga na kutunza urafiki na wengine. Wasaidie watu kuona mafanikio makubwa ambayo yapo mbele yao.
SOMA; Jinsi Ya Kuwabadili Watu Bila Kuibua Hasira Au Chuki Kanuni Ya Sita
Habari njema ni kwamba leo kwenye jumamosi ya ushawishi, tunakwenda kujifunza jinsi ya kuwabadili watu bila kuibua hasira au chuki kanuni ya SABA ambayo ni ; Mpe Mtu Sifa Kwenye Kile Unachotaka Awe
Mpendwa muuzaji bora kuwahi kutokea,
Kama kuna jinsi unataka mtu abadilike, mpe sifa ya kile ambacho unataka awe. Watu wanapopewa sifa fulani, huwa wanaishi kwa sifa hiyo.
Kwa mfano, mtu akipewa sifa ya uchelewaji au utoro basi ataishi kutunza sifa hiyo.
Kwenye mabadiliko unayotaka kwa mtu, mpe sifa ambayo atakazana kuiishi kila siku. Kama unataka awe msafi mpe sifa za msafi na atakuwa msafi.
Kama unataka mtu awe muuzaji bora, mpe sifa za kuwa muuzaji bora, kama unataka mtu awe vile unavyotaka awe mpe sifa hizo.

Angalia wateja wako unataka wawe na sifa gani, angalia watu unaohusiana nao, unataka wawe na sifa gani kisha wape zile sifa unazotaka wawe.
Kwa mfano, unaweza ukawapa sifa wale wateja wako ambao wanafanya manunuzi makubwa kwa siku, wiki na hata mwezi. Wewe unawajua wateja wako, wape sifa kwenye kile unachotaka wawe.
Ukimpa mtu sifa kama mtu makini au mtu anayejituma au mtu anayejali, habari njema ni kwamba mtu huyo atakazana kuishi hivyo ili kutunza sifa hiyo. Wale wanaosifiwa kwa mazuri wanayofanya, huwa mara nyingi wanapambana kuhakikisha wanalinda sifa ambazo tayari wamejijengea.
Yule ambaye anakosolewa naye atapambana kubaki na kile ambacho anakosolewa. Kwa mfano, mwanafunzi anayesifiwa kwa kufanya vizuri, ataendelea kufanya vizuri na yule anayekosolewa ataendelea kusimamia yale ambayo anakosolewa.
Tuwasifie watu kwenye yale mazuri tunayotaka kuyaona kwao. Kumbuka watu wanapenda msimamo, hivyo watafanya chochote kulinda msimamo wao. Wape watu sifa fulani na watahakikisha wanaiishi sifa hiyo.
Rafiki na mwalimu wako anayekupenda na kukujali katika mauzo,
Mwl.Deogratius Kessy
Mwalimu/Mwandishi/Mjasiriamali
Makamu Mkuu wa CHUO CHA MAUZO.
makamu@mauzo.tz, 📞0717101505//0767101504