3508; Jivuruge kabla ya kuvurugwa.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,

Mabadiliko makubwa huwa yanayokana na kuvurugwa.
Kunakuwa na vitu ambavyo vinaenda vizuri kabisa, lakini kunatokea hali ya kuvurugika na mambo yanabadilika sana.

Kwa bahati mbaya sana, hali ya kuvurugwa huwa inaletwa na watu wa nje na siyo wa ndani.

Yaani wale ambao wananufaika na mambo vile yanavyoenda huwa siyo wanaoyavuruga.
Kwa sababu hakuna anayependa kuvuruga kitu kinachomnufaisha.

Matokeo yake ni watu wa nje ndiyo wanavuruga.
Wale ambao hawanufaiki na mambo yanavyokwenda ndiyo huwa wanavuruga.
Na kupitia kuvuruga huko ndiyo wanapata nafasi ya kunufaika pia.

Tatizo pia linakuja kwa wale wanaovuruga na kupata nafasi, wanajisahau mpaka wanakuja tena kuvurugwa na wengine.

Kama unataka kupiga hatua kubwa kwenye kile unachofanya na kubaki juu, unapaswa kujivuruga wewe mwenyewe kabla hujavurugwa na watu wengine.

Unachopaswa kufanya ni kuhakikisha kila wakati unajiuliza mtu wa kukuvuruga atapitia wapi.
Angalia kila upande wa kile unachofanya na uone fursa za kuvurugwa zilizopo.
Kisha tumia fursa hizo kujivuruga wewe mwenyewe.

Ukishaona nafasi ambayo watu wanaweza kuitumia kukuvuruga, jua siyo wewe mwenyewe unayeiona. Wapo wengi wanaoiona, hivyo unapaswa uwahi kujivuruga wewe mwenyewe kuwazuia wengine wasifanye hivyo.

Ukijivuruga wewe mwenyewe unakuwa na urahisi kwa sababu tayari wewe una uelewa mkubwa kwenye kile unachofanya.

Na ukishachelewa kujivuruga ukajikuta umeshavurugwa na wengine, huwa ni vigumu sana kubaki kwenye nafasi uliyokuwepo.

Salama yako haipo kwenye kuomba wengine wasikuvuruge, bali ipo kwenye kujivuruga wewe mwenyewe kabla wengine hawajafanya hivyo.

Rafiki, je ni maeneo gani unayoona kuna fursa ya watu kukuvuruga kwenye hicho unachofanya sasa? Unajivurugaje mwenyewe ili usiwape wengine nafasi hiyo?
Karibu ushirikishe kwenye maoni hapo chini ili kuhakikisha huvurugwi na wengine.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe