3510; Wengine wanavyokuchukulia.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Kujali sana watu wengine wanakuchukuliaje ni moja ya vikwazo vya mafanikio.
Pale unaposhindwa kufanya kile unachojua unapaswa kufanya ili kupata matokeo unayotaka kupata kwa sababu hutaki watu wakuchukulie kwa namna fulani, jua unajikwamisha mwenyewe.
Kufanya au kutokufanya mambo kwa lengo la kusaridhisha watu wengine ni kuchagua kujikwamisha wewe mwenyewe.
Kwa sababu watu wengine wanakuchukuliaje wewe siyo jambo ambalo una udhibiti nalo.
Watu wataamua wakuchukulieje kwa mitazamo yao wenyewe.
Badala ya kuigiza kuwa mtu wa aina fulani ili kuwaridhisha watu, ni bora kuchagua kuwa wewe halisi.
Hiyo ni kwa sababu maisha ya maigizo huwa ni magumu sana na siyo halisia ambayo unaweza kujivunia nayo.
Ukiweza kutokujali wengine wanakuchukuliaje na ukawa na maisha huru kwako, utaweza kufanya makubwa sana.
Utanufaika kwa kuwa wewe halisia siyo kwa sababu kila mtu atakubaliana na wewe, bali kwa sababu utakuwa huigizi maisha.
Haijalishi unafanya nini kwenye maisha yako, kuna watu watakukubali na wengine watakukataa.
Ni bora kuchagua kuwa halisi kwako mwenyewe ili wale wanaokukubali wawe halisi pia.
Maisha ya maigizo huwa yanawavuta watu wasio sahihi kwako na hivyo kukuzuia kupata mafanikio makubwa unayoyataka.
Puuza kabisa wengine wanakuchukuliaje na chagua kuwa na maisha halisi kwako. Hivyo ndivyo utakavyoweza kuwavuta watu sahihi kwako na kufanya makubwa.
Rafiki, ni kwa namna gani kuhangaika na wengine wanavyokuchukulia kumekukwamisha kufanya makubwa kwenye maisha yako?
Shirikisha kwenye maoni hapo chini ili uishi maisha huru na halisi kwako na ufanye makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe