Habari njema muuzaji bora kuwahi kutokea,
Hongera na karibu sana kwenye mwendelezo wa makala zetu za ushawishi kutoka kwenye programu yetu ya CHUO CHA MAUZO.
Kwenye jumamosi ya ushawishi tunaongozwa na kauli mbiu yetu inayosema HUPATI UNACHOSTAHILI BALI UNACHOSHAWISHI.
Wiki iliyopita tulifanikiwa kujifunza jinsi ya kuwabadili watu bila kuibua hasira au chuki kanuni ya Nane ambayo ni ; Wape watu moyo na onesha kosa ni rahisi kusahihisha.
Na kwenye kanuni hiyo ya NANE, tulifanikiwa kuondoka na kitu kimoja ambacho ni;
Watie watu moyo kwamba wanaweza kuwa bora zaidi ya hapo walipo sasa.
Na kwa kosa ambalo mtu amefanya, usiegemee sana kwenye ubaya na ukubwa wa kosa, badala yake egemea kwenye njia za kusahihisha kosa hilo.
Kwa kufanya hivyo, watu wanapata matumaini kwamba wanaweza kufanya vizuri na pia kuona kosa walilofanya linarekebishika.
Kwa namna hii, utaweza kujenga ushawishi kwa watu bila kuibua hasira au chuki.
SOMA; Jinsi Ya Kuwabadili Watu Bila Kuibua Hasira Au Chuki Kanuni Ya Nane
Habari njema ni kwamba leo kwenye jumamosi ya ushawishi tunakwenda kujifunza jinsi ya kuwabadili watu bila kuibua hasira au chuki kanuni ya TISA ambayo ni; Wafanye Watu Wengine Kufurahia Unachopendekeza.
Kama unataka watu wawe tayari kufanya kile unachotaka wafanye, na wajitume kweli kwenye kukifanya, basi wafanye wafurahie kufanya kitu hicho.
Kifanye kuwa kitu muhimu au wape nafasi ya kipekee katika kukifanya na watakuwa tayari kukifanya kitu hicho vizuri.






Kama kiongozi, zingatia haya pale unapotaka watu wengine wafanye kile unachopendekeza wafanye;
1. Kuwa mwaminifu,usiahidi kitu ambacho huwezi kutekeleza. Usiangalie wewe unanufaikaje, bali angalia huyo unayemtaka afanye kitu.
2. Jua kwa hakika ni kitu gani unamtaka mtu huyo afanye.
3. Kwa mwenye kujali, jiulize ni kitu gani huyo anataka.
4. Jua manufaa ambayo mtu atayapata kwa kufanya kile unachotaka afanye.
5. Linganisha manufaa anayopata mtu na kile ambacho anataka.
6. Unapomwambia mtu afanye kitu hicho, elezea kwa njia ambayo inaonesha mtu huyo ananufaikaje kwa kufanya kitu hicho.
Kwa kuzingatia hatua hizi, utakuwa na ushawishi mkubwa kwa wengine, watakuwa tayari kufanya kile unachotaka wafanye kwa sababu wanajua watanufaika.
Na kwa kuwa watu ni wa binafsi, wanaojali mambo yao kuliko ya wengine, hakuna anayeweza kukataa kufanya kile kinachomnufaisha.
Rafiki na mwalimu wako anayekupenda na kukujali katika mauzo,
Mwl.Deogratius Kessy
Mwalimu/Mwandishi/Mjasiriamali
Makamu Mkuu wa CHUO CHA MAUZO.
makamu@mauzo.tz, 📞0717101505//0767101504