3514; Ambayo tayari unayajua.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Kinachowazuia watu kupata mafanikio wanayotaka ni kujua na kufanya.
Yaani mtu anakuwa hajui jinsi ya kupata anachotaka au kama anajua basi hafanyi.
Kwa zama tunazoishi sasa, zama za maarifa na taarifa, kujua siyo kikwazo sana.
Watu wengi tayari wanajua mengi juu ya kile wanachotaka.
Tatizo kubwa lipo kwenye kufanya.
Kuweka kwenye vitendo yale ambayo tayari mtu anayajua imekuwa ni kikwazo kikubwa.
Sababu kubwa ya watu kutokufanya ni mazoea na hofu ya kujaribu vitu vipya.
Ni rahisi kwa watu kuendelea kufanya yale waliyozoea kuliko kufanya vitu vipya ambavyo hawana uhakika wa matokeo.
Kama ungefanya yale yote ambayo tayari unajua jinsi ya kuyafanya ila huyafanyi, ungekuwa mbali mara 10 zaidi ya hapo ulipo sasa.
Unasubiri mpaka ujue zaidi, wakati hayo unayoyajua sasa bado hujayafanyia kazi hata kwa kiwango kidogo.
Kadiri unavyoendelea kujua vitu vingi na huchukui hatua, ndivyo unavyozidi kuhofia kuchukua hatua.
Kila unapojiambia kuna kitu hujajua ndiyo maana hupati matokeo unayotaka, jiulize kama yote unayoyajua umeshayafanyia kazi.
Jibu litakuwa ni hapana na hivyo tayari unajua ni wapi pa kuanzia.
Rafiki, ni yapi unayojua unapaswa kuyafanya ili ufanikiwe ila bado huyafanyi kwa viwango vya kutosha?
Shirikisha kwenye maoni hapo chini ili ujikumbushe kutekeleza badala ya kuendelea kusubiri na kujichelewesha.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe