Mara nyingi huwa napata nafasi ya kukutana na vijana wengi ambao ndio kwanza wanakuwa wamemaliza masomo yao ya chuo kikuu. Ni nafasi pia ambayo huwa naitumia kutaka kujua ni mipango gani wamejiwekea baada ya kumaliza masomo yao.
Ni mengi ambayo huwa ninayapata kutoka kwao, lakini kwa walio wengi kilio chao kikubwa huwa ni suala la ukosefu wa ajira. Kwa asilimia kubwa wengi wao ninao kutana nao ni lazima hugusia tatizo la ajira. Hiki ni kitu ambacho huwa kinaniuma sana kwa kusikia taarifa zile zile, tena mara kwa mara zikijirudia.
Kuna maswali mengi ambayo hubaki nikijiuliza tatizo ni nini hasa?kweli ni ajira au tatizo pia lipo kwa wahitimu wenyewe?Huwa nabaki najiuliza maswali yote hayo baada ya kugundua kwamba tupo kwenye taifa ambalo bado lina fursa nyingi sana kuzitumia.
Kama fursa hizi zote zipo nafasi ya vijana waliomaliza vyuo mbalimbali ya kujitengenezea ajira iko wapi?wengi kweli hukata tamaa na kujikuta wakilala na kusahau kuwa zipo fursa nyingi sana ambazo wangeweza kuzitumia kuwafanikisha bila wao kujua.
Lakini, unapokuja kuchunguza kwa makini, chanzo cha vijana wengi kukwama kufikia mafanikio unakuja kubaini wakati mwingine tatizo linaweza lisiwe ajira bali vipo vizuizi au mambo yanayomzuia kijana huyu kufikia mafanikio makubwa katika maisha yake.
Ni vizuizi au mambo hayohayo ambayo natamani kila kijana mwenye uchungu na mafanikio yake ayajue ili aweze kujikwamua hapo alipo na kuwasaidia wengine. Haina haja ya kukata tamaa, upo uwezo wa kufanikiwa mkubwa ndani mwako ikiwa utagundua mambo yanayokukwamisha kufanikiwa.
Sitaki kuona ukiendelea kuteseka na kuishi maisha magumu bila sababu wakati kila fursa ya mafanikio ipo katika hii Nchi. Acha kusingizia sana ajira kuwa ndilo tatizo pekee hasa linalokukwamisha. Bila kupoteza muda, ni vyema ukayajua mambo yanayomkwamisha kijana wa kitanzania  kufikia mafanikio makubwa, ili uchukue hatua.
1. Kutafuta mafanikio ya haraka.
Fikra nyingi za vijana wanaomaliza vyuo mbalimbali huwa zimejikita kwenye kutaka mafanikio ya haraka. Kwa hakika hili limekuwa tatizo kubwa ambalo kwa bahati mbaya wengi huwa hawalioni kirahisi, lakini limekuwa likipelekea mipango na malengo yao mengi kukwama. Kutokana na hili hujikuta wakiwaza njia nyingi za mikato za kupata pesa ikiwemo  hata rushwa na kusahau kutafuta mafaniko hatua kwa hatua.
Unapokutana na kijana kama huyu awe amesoma au hujasoma na unapokuja kumwambia kuwa maisha ni hatua na mipango kiukweli hawezi kukuelewa nini unachoongea. Hili ni moja ya tatizo kubwa sana linawakabili vijana wengi wa kitanzania na kupelekea kushindwa kupata mafanikio.
LAZIMA KUJIWEKEA MIPANGO IMARA YA MAFANIKIO YAKO.
2.  Kukosa mipango na malengo imara.
Kutokana na kukosa mipango na malengo imara hili limekuwa ni tatizo pia linalopelekea vijana wengi kushindwa kufanikiwa. Vijana wengi wamekuwa wakiishi kwa kuwa na mipango ya muda mfupi sana au hakuna kabisa. Kikubwa kinachowapoteza hapa ni kuangalia kwao mambo ya sasa ikiwemo starehe za muda mfupi.
Ni muhimu sasa kujua kwamba mafanikio yanahitaji malengo. Kama ajira kweli hakuna ni kitu gani kinachofanyika cha mbadala ili kupata kitu cha kukuingizia kipato? Vijana wengi wamekuwa wakiwaza tu ajira ajira na mwisho wa siku wanajikuta wakikosa kitu cha kufanya kabisa. Kwa hiyo kukosa malengo ni tatatizo linalowakwamisha vijana wengi kufikia ndoto zao.
3. Kukosa kujiamini.
Kama upo kwenye safari ya mafanikio halafu hujiamini, elewa kabisa huwezi kufikia mafanikio hayo. Mafanikio yoyote yale yanahitaji ujiamini wewe kwanza kuwa unaweza. Vijana wengi wanakosa kujiamini na matokeo yake hujikuta wakishindwa kuchukua hatua za kubadili maisha yao.
Na kutokana na tatizo hili la kutokujiamini hupelekea wao kushindwa kuzitumia fursa zilizopo nchini kama vile biashara ndogondogo za kujiajiri, kilimo cha kisasa na hata ufugaji wa kisasa pia. Kitu cha kujiuliza je, ni kweli ajira peke yake ndiyo chanzo cha kipato? Jibu bila shaka ni hapana. Tatizo kubwa linaloonekana hapa kumkwamisha kijana huyu wa Kitanzania kufanikiwa ni kutokujiamini kwake.
4. Kukosa mtaji.
Mbali na matatizo mengine binafsi ambayo yamekuwa yakimkwamisha kijana kufikia mafanikio, lakini swala la kukosa mitaji pia nalo ni tatizo kubwa sana. Vijana wengi wenye elimu ya juu na kawaida, wote kwa pamoja kilio ni hikihiki kwamba hakuna mtaji. Ni kweli wanakuwa wanatamani kufanya bishara fulani, lakini hakuna mtaji wa biashara hiyo.
Na hili ni jambo ambalo serikali na wadau wengine wanatakiwa kuliangalia kwa jicho la pili ili kuwasaidia vijana hawa kuweza kutoka walipo na kujenga taifa  imara lenye mafanikio. Lakini si hivyo tu hata vijana wenyewe wanaweza kuungana ili kupata mitaji na kuanza kuwekeza kwenye miradi ya kuwafanikisha.
Yapo mambo mengi ambayo yamekuwa kikwazo cha kumzuia kijana wa kitanzania kufanikiwa. Lakini kwa leo fanyia kazi kwanza mambo hayo machache ili yawe msaada kwako.
Tukutane wiki ijayo katika ukurasa huu kujifunza zaidi juu ya maisha na mafanikio.
Kwa makala nyingine nzuri pia tembelea DIRA YA MAFANIKIO kujifunza na kuhamasika kila siku.
Ni wako rafiki katika mafanikio,                      
Imani ngwangwalu,
Simu; 0713 048 035,
E-mail; dirayamafanikio@gmail.com

Blog; dirayamafanikio.blogspot.com