3537; Rudia kinachofanya kazi.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Watu wengi wamekuwa wanakwama kufanikiwa kwenye maisha, siyo kwa sababu hawawezi kufanikiwa, bali kwa sababu wanachoka haraka sana.
Na siyo kuchoka ya kuishiwa nguvu za kufanya kitu, bali kuchoka ya kuona wanahitaji kufanya vitu tofauti.
Ukweli ni kwamba kwenye zama hizi watu wamekuwa wanapoteza muda na nguvu zao nyingi kukimbizana na vitu vipya.
Wanaacha vitu ambavyo tayari vinafanya kazi kwa uhakika na kwenda kwenye vitu ambavyo hawajajua kama vitafanya kazi kwao.
Mafanikio makubwa hayana hata mambo mengi sana.
Bali kuna ya msingi yanayopaswa kuzingatiwa.
Kwanza ni kujua nini ambacho kinafanya kazi kwako. Hapa utajaribu na kujifunza mengi mpaka kufikia yale yanayokupa matokeo unayotaka kupata.
Pili ni kurudia yale yanayofanya kazi. Hapa sasa ndiyo unapaswa kutulia na kufanya kwa ukubwa yale ambayo yanakupa matokeo unayoyataka.
Wakati unarudia kufanya yale yanayofanya kazi, kuna ya muhimu kuzingatia kama;
1. Kuendelea kujifunza na kuona mabadiliko yanayotokea ili uchukue hatua za kuboresha mapema.
2. Kujua vinavyokukwamisha kurudia kinachofanya kazi kwa ukubwa na kuvitatua ili urudie kufanya kwa ukubwa bila kuacha.
3. Kuepuka kutekwa na fursa mpya zinazojitokeza na kuonekana ni nzuri kuliko kile unachofanya.
Unapaswa kujua kwamba kile unachofanya sasa, kama kinakupa matokeo unayotaka, ndiyo fursa bora zaidi kwako.
Usihangaike na fursa nyingine yoyote inayokutoa kwenye hicho unachofanya.
Badala yake rudia kukifanya kwa ukubwa zaidi.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE
+255 678 977 007 | http://www.amkamtanzania.com
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe