3544; Tiba ipo kwenye ujenzi.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Hali ya msongo na kuvurugwa imekuwa kubwa na kwa watu wengi kwenye zama hizi.
Watu wamekuwa wanavurugwa sana na kukata tamaa pale wanapokutana na changamoto wanazoshindwa kuzitatua.
Matokeo yake ni watu kuishia kuwa na maisha duni ambapo hakuna makubwa wanayofanya.
Tiba ya mambo yote hayo ipo kwenye ujenzi.
Mtu anapokazana kujenga kitu chochote ambacho ni kikubwa kuliko yeye, huwa anapata utulivu mkubwa.
Utulivu huo hautokani na changamoto kutokuwepo, bali unatokana na makubwa ambayo mtu anahangaika nayo kiasi kwamba madogo yanakosa nafasi kabisa.
Mambo mengi madogo madogo yanayowasumbua watu huwa yanapata nguvu pale mtu anapokuwa hana mambo makubwa anayohangaika nayo.
Pale mtu anapokuwa na mambo makubwa yanayomsumbua, changamoto ndogo ndogo huwa zinajitatua zenyewe bila ya kumsumbua kabisa.
Ndiyo maana tunasema tiba ya msongo na kuvurugwa ipo kwenye ujenzi wa kitu ambacho ni kikubwa kuliko mtu.
Kwenye kukazana kujenga kilicho kikubwa, umakini wote unakwenda kwenye mambo makubwa zaidi.
Kutokana na manufaa makubwa ambayo ujenzi wa kitu kikubwa yanakuwa nayo, kila mtu anapaswa kuwa anajenga kitu kikubwa sana.
Na moja ya vitu vikubwa kwa kila mtu kujenga ni biashara inayoweza kujiendesha yenyewe bila ya kumtegemea mtu moja kwa moja.
Kujenga biashara ya aina hiyo, ambayo itaweza kudumu kwa miaka mingi hata baada ya mtu kuondoka hapa duniani ni kitu kikubwa ambacho kitamtaka mtu kujitoa hasa.
Ni katika kujitoa huko ndiyo mtu anaacha kusumbuliwa na vitu vidogo vidogo ambavyo vimekuwa vinamvuruga na kumpa msongo.
Zaidi ya hayo, ujenzi mkubwa unampa mtu ukuaji na kumkutanisha na watu sahihi. Kunamletea mtu hali ya kuridhika kwa matokeo makubwa anayokuwa anayapata kwenye kile anachofanya.
Watu wengi huona kujenga vitu vikubwa ni kugumu na hivyo kubaki kwenye ujenzi wa vitu vidogo.
Lakini ukweli ni kutokujenga vitu vikubwa ndiyo kunamsumbua mtu kuliko kujenga vitu vikubwa.
Unapata usumbufu na msongo zaidi kwenye vitu vidogo kuliko vikubwa.
Rafiki, ni nini kikubwa kuliko wewe unachojenga, ambacho kinayanyima mambo madogo madogo nguvu ya kukusumbua?
Una mpango gani kwenye kujenga biashara kubwa ambayo itaendelea kuishi hata baada ya wewe kufariki?
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE
+255 678 977 007 | http://www.amkamtanzania.com
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe