3546; Usiadhibu wengi kwa kosa la wachache.

Kutoka mezani kwa Kocha,

Rafiki yangu mpendwa,

Kwenye maisha, biashara na shughuli nyingine tunazofanya, huwa tunajiwekea taratibu mbalimbali.
Lengo la taratibu hizo huwa ni kurahisisha utekelezaji wa majukumu mbalimbali yanayohusisha watu wengine.

Lakini huwa inatokea kwa baadhi ya watu hao wengine kwenda kinyume na taratibu tulizoweka.
Pale hilo linapotokea huwa ni rahisi kujibu kwa kuboresha taratibu tulizoweka ili kuhakikisha wengine hawarudii kwenda kinyume nazo.

Zoezi hilo la kubadili taratibu tunazokuwa tumeweka kwa sababu baadhi ya watu wanaenda kinyume nazo ni kuwaadhibu watu wengi kwa kosa la watu wachache.

Unaweza kuona kufanya hivyo ni kuondoa mianya ya watu kwenda kinyume na taratibu sahihi ulizoweka.
Lakini matokeo yake ni kupunguza wale ambao wangefanya kwa usahihi.

Kila unapozifanya taratibu za ufanyaji wa jambo kuwa gumu kwa sababu kuna wachache wanazikiuka, unawapoteza wengi zaidi ambao wangeweza kufanya kwa usahihi.

Kwa mfano kwenye biashara yako unaweza kuwa umeweka utaratibu wa wateja kurudisha walichonunua kama hakijawafaa kama walivyotegemea.
Kwenye utekelezaji wa hilo, aadhi ya wateja wakawa wanarudisha vitu ambavyo hujawauzia wewe.

Hapo unaweza kuona suluhisho ni kuondoa kabisa huo utaratibu. Kwamba uache kuruhusu wateja kurudisha walichonunua kwa sababu baadhi wanatumia hiyo fursa kufanya udanyanyifu.

Hapo unakuwa umewaadhibu wengi ambao walikuwa wanaitumia fursa hiyo kwa usahihi kwa sababu ya wachache wanaoitumia kwa ubadhilifu.

Matokeo yake ni unawakosa hao wazuri ambao walikuwa wananunua kwa sababu ya uhakikika wa kurudisha na pia unawakosa wale wasio sahihi ambao pia wanaona hawana cha kunufaika nacho.

Badala ya kukimbilia kuwaadhibu wengi kwa sababu ya makosa ya wachache, waadhibu hao wachache.
Wachukulie hatua wale wachache wanaoenda kinyume na utaratibu ulioweka, huku ukiendelea kuacha utaratibu uwanufaishe wale wanaoutumia vizuri.

Ni kazi ya ziada kuwaadhibu wachache wanaovunja taratibu kuliko kudadili utaratibu mzima.
Lakini tunajua kwenye mafanikio yoyote, njia rahisi haijawahi kuleta matokeo makubwa kadiri tunavyotaka.

Tuweke taratibu sahihi kwa matokeo tunayoyataka na pale wachache wanapovunja taratibu hizo tusizibadili, badala yake tuwashughulikie hao wachache ili wasivuruge taratibu tulizoweka.

Hilo na kwa kila eneo la maisha yetu na watu wote tunaojihusisha nao.
Zingatia taratibu unazoweka ili ziweze kuwa na manufaa kwa watu sahihi na kwako.
Huku wale wasiokuwa sahihi kupata adhabu kali pale wanapojaribu kujinufaisha isivyo sahihi kwa kwenda kinyume na utaratibu.

Rafiki, ni taratibu zipi umewahi kuzibadili kwa wengi kwa sababu wachache walikuwa wanazitumia vibaya?
Nini ulichojifunza na unafanyaje ili hilo lisijirudie tena?

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE
+255 678 977 007 | http://www.amkamtanzania.com

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe