3551; Hukomoi bali unajikomoa.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Maisha tayari ni magumu, lakini ugumu huo unaweza kuvumilika na kutumiwa vizuri na wale waliodhamiria kweli kufanikiwa.
Tatizo kubwa linakuja pale watu wanapoamua kuzidisha ugumu huo wa maisha kwa yale wanayokuwa wanayafanya.
Moja ya vitu vinavyozidisha ugumu wa maisha ni pale mtu anapofanya kitu kwa kukomoa, halafu anaishia kuwa amejikomoa yeye mwenyewe.
Hilo hutokea sana kwa yale mambo ambayo mtu unalazimika kuyafanya kila siku au kufanya mara kwa mara.
Mtu anapofanya kwa kukomoa, anaishia kujikomoa yeye mwenyewe, kwa sababu siyo kitu cha mara moja.
Chukua mfano wa kula, ni kitu ambacho utakifanya kila siku kwa kipindi chote cha maisha yako.
Unapoamua kula kwa kukomoa, unaishia kujikomoa wewe mwenyewe.
Kama umeenda kwenye sherehe fulani, au umekutana na chakula kizuri na ukala kwa wingi kuliko kawaida, hakuna manufaa yoyote unayokuwa umeyapata.
Kwani siku inayofuata tumbo lako litakuwa tupu na utahitaji kula tena.
Lakini pia bado ulaji mkubwa unaokuwa umeufanya unachosha mwili na kuleta madhara ya kiafya.
Ulaji kupitiliza unajengeka kuwa tabia, inayopelekea uzito wa mwili kuwa mkubwa na hatimaye kukaribisha magonjwa sugu ambayo yanamtesa mtu.
Hivyo pia ndivyo ilivyo kwa mambo mengine yote yanayofanyika kwenye maisha yetu.
Pale kitu kinapokuwa cha kujirudia, hakuna namna tunaweza kukikomoa.
Tukijaribu kufanya tu kwa kukomoa, tunaishia kujikomoa sisi wenyewe.
Kilicho muhimu ni mtu ujue mchakato sahihi kwako kupata kile unachotaka, kisha kwenda na huo.
Mengine yote ambayo hayana mchango kwenye kile unachotaka hupaswi kuhangaika nayo kabisa.
Kwa mambo yote ambayo unayafanya kwa kurudia rudia, yafanye kwa kiasi kadiri inavyohitajika ili maisha yako yaweze kuendelea.
Usifanye chochote kwa kukomoa, kwa sababu utaishia kujikomoa mwenyewe kwa tabia isiyokuwa sahihi utakayokuwa umejijengea.
Kama tunavyojua, huwa tunajenga tabia, kisha tabia zinatujenga.
Kwa kufanya kwa kukomoa mambo yanayojirudia, tunajenga tabia mbaya ambayo inakuwa mzigo kwetu.
Rafiki, ni mambo gani ya kujirudia rudia ambayo umekuwa unayafanya kwa kukomoa na unaishia kujikomoa mwenyewe? Yaainishe hayo na kisha yafanye kwa kiasi kinachohitajika ili yasiwe kikwazo kwako kupata unachotaka.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE
+255 678 977 007 | http://www.amkamtanzania.com
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe