3553; Yana Mwisho.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Watu wengi wamekuwa wanaianza safari ya mafanikio wakiwa na shauku kubwa.
Lakini wengi wanaishia njiani kwa kukata tamaa na kuacha.
Kinachopelekea wengi hao kuishia njiani ni pale wanapokutana na magumu na changamoto ambazo hawakutegemea.
Na hata kama walitegemea, basi hawakuwa na maandalizi sahihi ya jinsi ya kukabiliana nayo.
Wengi wanafikia maamuzi ya kuacha kwa kuona kwamba mambo yataendelea kuwa mabaya na magumu milele.
Hawaioni kesho yenye matumaini, ndiyo maana wanakata tamaa.
Ukweli ni kwamba, hakuna kitu ambacho hakina mwisho.
Mambo mazuri na mambo mabaya yote yana mwisho.
Mambo rahisi na mambo magumu yote yana mwisho.
Tukijua na kuamini hilo, hakuna kinachoweza kuturudisha nyuma.
Pale unapokutana na magumu na changamoto kwenye safari ya mafanikio, jikumbushe machaguo haya yaliyo mbele yako;
Moja ni kukata tamaa na kuacha kufanya. Chaguo rahisi lakini la kupoteza kabisa.
Mbili ni kuendelea mpaka mambo yawe rahisi au wewe uwe mgumu. Hili ni chaguo gumu, lakini lenya ushindi mkubwa.
Uzuri ni kwamba, hata iweje, kila kitu kina mwisho.
Ugumu una mwisho,
Maumivu pia yana mwisho.
Wewe usikubali kuishia njiani, endelea kwenda mpaka uufikie mwisho.
Rafiki, ni hali zipi za kukatisha tamaa ambazo ulishakutana nazo ila ukaendelea na mambo yakawa mazuri?
Jikumbushe hali hizo mara zote ili uendelee na mapambano bila kuishia njiani.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE
+255 678 977 007 | http://www.amkamtanzania.com
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe